WAKATI Yanga walipowakaribisha Kaizer Chifes kwenye mechi ya Siku ya Wananchi wengi wa mashabiki wa klabu hiyo ya Afrika kusini walivutiwa na umahiri wa Zawadi Mauya. Katika mitandao ya kijamii ya Kaizer Chifes kulikuwa na wimbi la maoni ya mashabiki wakihimiza viongozi wao kumsaka Zawadi Mauya ili kumsajili kikosini mwao. Mashabiki wa Kaizer Chiefs walipigia kelele jambo hilo kutokana na mechi hiyo kuoneshwa moja kwa moja kwenye Televisheni nchini mwao.
Wengi walimtazama Zawadi Mauya kipindi cha pili akiwa amevaa kitambaa cha unahodha. Hata hivyo mtokea benchi huyo hakuwa peke yake, kwani eneo analocheza lina ushindani mkubwa. Wakati Zawadi Mauya akiwakosha mashabiki wa Kaizer Chifes, hali ya mambo imezidi kuonga kwa hapo hapo Ligi Kuu Afrika kusini. Maelfu ya mashabiki wa klabu ya Chippa United wameshuhudia kipaji kutoka Tanzania kikichachafya kwenye kikosi chao. Ni kipaji cha Baraka Majogoro ambacho kimewavutia wengi.
MCHEZAJI BORA WA MECHI
TANZANIASPORTS inaendelea kufuatilia maendeleo ya nyota huyo aliyekipiga klabu za Mtibwa Sugar na KMC za Ligi Kuu Tanzania, Baraka Majogoro ameanza kuwika ndani ya kikosi cha Chippa United. Kana kwamba haitoshi nyota huyo hivi karibuni alichaguliwa mchezaji bota wa mechi (MOFM) dhidi ya Supersports United na kujibu maswali kwa lugha Kiswahili. Watangazaji waliduwazwa na uwezo wa nyota huyo kwani badala ya kutumia lugha ya Kiingereza aliamua kujibu maswali kwa lugha ya Kiswahili. Alikuwa amejawa na tabasamu.
Kila swali aliloulizwa na mtangazaji alijibu kwa Kiswahili. Kama ilivyo kawaida ya wachezaji wengi wa Kitanzania alitanguliza neno, “namshukuru Mungu” wakati alipotakiwa kuzungumzia mchezo huo. Chippa United waliibuka na ushindi katika mchezo wao dhidi ya Supersports United.
TANZANIASPORTS inafahamu kuwa bao la ushindi la Chippa United lilifungwa na mshambuliaji Elmo Kambindu raia wa Namibia ambalo lilikuwa la tatu kwake tangu kuanza msimu huu. “Baraka Majogoro amekuwa na kiwango cha kuvutia tangu amejiunga na klabu ya Chippa United. Kiungo huyo wa Tanzania amethibitisha kuwa mchezaji mwenye thamani msimu huu,” ameandika mwandishi wa habari za michezo Afrika kusini, Lorenz Kohler.
KIUNGO WA ULINZI
Baraka Majogoro aliwahi kujumuishwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki michuano ya CHAN wakati ikinolewa na kocha Ettiene Ndayiragije. Kocha Ettiene kwa sasa anaifundisha timu ya taifa ya nchini kwao Burundi. Baraka Majogoro ni kiungo wa ulinzi eneo ambalo Taifa Stars lina ushindani mkubwa. Katika nafasi hiyo kuna wachezaji waandamizi kama vile Mzamiru Yassin, Himid Mao,Mudathir Yahya,Salum Abubakar na Abdi Banda. Kwa mechi za hivi karibuni za Ligi ya Afrika kusini Baraka Majogoro amevutia hisia za mashabiki. Vyombo vya habari navyo vimeanza kumzingatia huku benchi la ufundi la Chippa United likimpa nafasi karibu kila mechi.
UFUNDI WA MAJOGORO
Anasifika kwa utulivu awapo dimbani. Ni mchezaji ambaye anapiga pasi ndefu na fupi. Anaweza kucheza nafasi ya kiungo mkabaji kwa ufasaha jambo ambalo baadhi ya wadau wa michezo wa Afrika kusini wadhani anafaa pia kucheza nafasi ya beki wa kati kutokana na kumudu nafasi hiyo dhidi ya Supersports United, hadi pale kocha wa Chippa United alipomtoa Mosele, ndipo Baraka Majogoro akarudi kwenye nafasi ya kiungo.
Tathmini ya TANZANIASPORTS, inaonesha kuwa Baraka Majogoro anaweza kuwafundisha mambo mengi ya kiufundi wachezaji wazawa wa Afrika. anaweza kukaba kwa ufasaha katika mtasrai na kutengeneza mashambulizi. Wakati wote awapo uwanjani anatoa pasi na kufungua nafasi kuomba mpira na ana uwezo mkubwa wa kugundua mipenyo inayoweza kutumika na wapinzani wao kuwaadhibu.
“Nilimwangalia kijana huyo wakati wa mechi dhidi ya Richards Bay kwenye uwanja wa Zwelithini wiki iliyopita, ni mchezaji mzuri ananikumbusha ubora wa mchezaji wetu mzawa Lebogang Mothibantwa. Majogoro anaweza kusoma mchezo vizuri sana, na kugundua nafasi za hatari zinazoweza kutumika na wapinzani wao. Kingine anaweza kupenyeza pasi nzuri eneo la hatari la adui. Pia anatibua mipango mingi ya adui wanapotafuta goli langoni,” mwandishi mmoja wa habari za michezo ameiambia TANZANIASPORTS.
Lakini Baraka Majogoro mwenyewe anafahamu kuwa yupo katika Soka la kulipwa na nafasi yoyote anaweza kupangwa.
HAJACHEZA SIMBA,YANGA
Ni nyota ambaye hajawahi kuzichezea timu kubwa za Tanzania za Simba, Yanga au Azam, lakini amecheza dhidi yao. Kabla ya kwenda Afrika kusini, Baraka Majogoro alikwenda kwenye majaribio na klabu hiyo wakati wa maandalizi ya msimu huko nchini Zambia kabla ya benchi la ufundi la Chippa kukubali kiwnago chake.
AIWINDA AFCON
Sifa nyingi anazomwagiwa nyota huyo bila shaka ni chachu ya yeye kuisaka nafasi ya kujumuishwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa kitakachokwenda kwenye michuano ya AFCON nchini Ivory Coast. Baraka Majogoro bila shaka yoyote anafuatiliwa na benchi la ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na kocha Adel Amrouche. Benchi la ufundi lina kibarua kigumu kuteua wachezaji 25 watakaokwenda kwenye fainali za AFCON ambazo zitashirikisha timu 24 kwa mara ya kwanza ikiwemo Tanzania inayoshiriki kwa mara ya tatu.
Comments
Loading…