in ,

Balozi Kallaghe: Tunahitaji mipango ya muda mrefu michezoni

*Apendekeza wataalamu washauri kuboresha timu
*Aandaa hafla apongeza wachezaji kwa nidhamu
Na Israel Saria
Balozi wa Tanzania katika Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe amewasifu wanamichezo wa Tanzania walioshiriki Olimpiki kwa nidhamu waliyoonyesha.
Akitoa nasaha katika hafla aliyoiandalia timu na viongozi nyumbani kwake London jana, Mhe Balozi aliwashukuru kwa kuwa wastaarabu muda wote wa mashindano.
“Pamoja na matokeo yasiyo mazuri viwanjani, lakini sisi kama nchi, tunajivunia nidhamu na ustaarabu mliounyesha tofauti na wanamichezo wa baadhi ya nchi nyingine,” alisema bila kuzitaja kwa majina.
Mhe Balozi Kallaghe alitoa wito kwa wataalamu wa michezo kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya sababu za kufanya vibaya kwa Tanzania katika medani ya michezo kimataifa.
“Nakiri mapungufu katika suala zima la matokeo ambayo yamekuwa mabaya kwa timu yetu, na wala sina furaha kwa hili, lakini ifike mahali tuache kulaumu bila kutoa ushauri makini nini kifanyike ili kuleta mabadiliko katika suala zima la michezo.
“Nakutana na mabalozi wenzangu wa nchi za Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, hawa ni majirani zetu, wengine wanafanya vizuri wakati sisi hatufanyi vizuri, lakini jukumu la serikali ni kuweka mazingira mazuri ya kiutawala na kuviacha vyama vya michezo kushauri na kutengeneza mipango ya muda mrefu na mfupi ili kupata mafanikio yaliyo bora,” alisema Mhe Balozi Kallaghe.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na Balozi wa Rwanda katika Uingereza, Mhe Ernest Rwamucyo, aliyewaasa wanamichezo kutokata tamaa.

“Mazingira ya nchi zetu yanafanana, na ni wajibu wa viongozi wa vyama vya michezo kushirikiana, tuwe na mashindano mengi ya ujirani mwema. “Tukishindana mara nyingi ni lazima tutakuwa na wanamichezo wazuri, na ni vizuri tukachagua baadhi ya michezo ili kuweka mkazo zaidi kwa ajili ya kushindana katika ngazi za juu,” akasema Balozi huyo ambaye nchi yake kama Tanzania haikupata medali yoyote.
Mhe Balozi Kallaghe alieleza kwamba mfumo wa michezo kwa wote ni mzuri kwani hutoa nafasi kwa kila mtoto wa Kitanzania kushiriki michezo.
Hata hivyo, alitaka mkazo uwekwe zaidi kwenye  kutambua vipaji, kuviendeleza na kuvitunza. Changamoto ipo katika kuhakikisha vijana wenye vipaji wanapata nafasi ya kushiriki masomo na pia kuwa karibu na familia zao.
“Tanzania ni nchi kubwa na ina watu wengi ambao si rahisi kuamini hatuna wakimbiaji mahiri kama miaka ya nyuma… kwenye riadha hatuhitaji uwekezaji mkubwa huu ni mchezo wa mtu mmoja mmoja (individual sport), kwa hiyo hapa unazungumzia kukimbia nyikani au kwenye viwanja vya mipira ambavyo karibu kila mkoa na wilaya unavyo, kutokana na umaarufu wa mpira wa miguu.
“Tukiwa na walimu wazuri wa kuwasimamia hawa wanariadha nina imani tutafanya vizuri tu, na serikali kupitia vyama vya michezo inaweza kufikiria jinsi ya kuwa na mashindano mengi ya ndani au ya ujirani mwema,” akashauri Mhe Balozi Kallaghe.
Mapema mkuu wa msafara wa timu ya Tanzania, Hassana Jarufu, alimshukuru Mhe Balozi kwa msaada mkubwa alioutoa kwa timu, huku akikiri mapungufu ya kutouarifu ubalozi juu ya ujio wao.

Hali hiyo ilisababisha Mhe Balozi Kallaghe mwenyewe kuwatafuta, hatimaye kuwapata wakiwa kambini Bradford.
Jarufu alisema kufanya vibaya kwa timu kumechangiwa na mambo mengi, moja likiwa maandalizi duni.
Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ndiyo ilibeba mzigo wa kugharamia michezo ya majaribio ya mabondia nje ya nchi ili kuwasaidia kuinua viwango, kazi ambayo kwa kawaida ilitakiwa kufanywa na vyama vya michezo.
Akizungumzia uwajibikaji wa wachezaji, Jarufu alisema wengi wanajitoa zaidi kwa michezo ya mwaliko.
“Huko ndiko wanapopata fedha na ufadhili tofauti na huku, kwa hiyo hawajitumi kwa asilimia mia moja,” alisema Bw Jarufu.
Akizungumza katika hafla hiyo kwa aibu, mwanariadha Zakhia Mrisho aliomba radhi kwa matokeo mabaya.
Lakini, alionyesha bayana kwamba kuna kitu kisicho sawa ndani ya mfumo mzima wa maandalizi na hatimaye ushiriki wa timu ya Tanzania.
Mwishoni Mhe Balozi Kallaghe akizungumza nami, alitoa changamoto kwa sisi wataalamu wa michezo kutoa mapendekezo yetu kwa serikali, ili hatimaye suluhu la kufanya vibaya lipatikane.
“Bwana Saria, kwa kuwa umewahi kuwa kiongozi wa kitaifa wa mchezo wa Volleyball, na sasa uko hapa, ni vizuri ukafanya majumuisho ya yale ambayo wenzetu wanayafanya hapa na kuonanisha na sisi, ili kutafuta uwiano mzuri.
“Baadhi ya mambo yanahitaji busara na maamuzi tu wala si lazima tuwe na pesa nyingi. Kwa mfano, ukiangalia sehemu nyingi za wazi hapa Uingereza zina mashine za kufanyia mazoezi kwa wananchi wa kawaida, hivyo kutoa nafasi kwa wale wasio na uwezo wa kwenda Gym kufanya mazoezi bure na kwa wakati wao.
Sioni kwa nini hiki kitu kisifanyike nyumbani, kwa nyie mlioko hapa ni wajibu wenu kuwaambia watu wa nyumbani.
Kwa upande wangu, nilikubaliana na Mhe Balozi na kushauri wizara husika ifanye mpango wa kukusanya mawazo mengi mazuri yanayotolewa na wadau wa michezo kwenye mitandao ya jamii.
Baada ya kukusanya, wayafanyie kazi, kwani Watanzania wengi hawana pa kusemea zaidi ya kuingia kuandika na kuchangia mitandaoni.
Hata hivyo, tatizo ni kwamba hakuna kitengo au idara inayoyafanyia majumuisho maoni hayo wala kuyafanyia  kazi yale yenye msingi.
Katika hafla hiyo, wageni na wanamichezo walikula na kunywa, huku wakiburudika kwa miziki mizuri ya Kitanzania. Timu ya Tanzania inaondoka hapa leo kurejea nyumbani.
Pia watumishi wa kujitolea wa Olimpiki walishiriki katika hafla hiyo, ambapo mabolozi wote wawili walifurahishwa na kazi ya wafanyakazi hao ya kuwasaidia wageni kwenye Olimpiki jijini London.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Siri ya Uingereza kufanya vizuri Olimpiki

Salaam za Olimpiki …Na Gloria Mutahanamilwa