in , , ,

AZAM, YANGA ZANG’ANG’ANIANA TAIFA

 

Azam na Yanga zimeendelea kung’ang’aniana kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu bara msimu huu baada ya jioni hii kutoka sare ya 2-2 kwenye mpambano baina yao uliopigwa kwenye dimba la Uwanja wa Taifa.

Mpambano huo wa kukata na shoka ulizishuhudia timu hizo zikishambuliana kwa zamu kwenye dakika zote za mchezo huku matokeo ya vita hiyo ya panzi yakiwapa furaha kunguru Simba Sports Club.

Ni Ramadhani Singano aliyekuwa wa kwanza kuibua msisimko wa mchezo huo baada ya kupiga shuti lililogonga mwamba sekunde chache baada ya mpira kuanza.

Kazi nzuri ya Kipre Tchetche ikalazimisha makosa ya mlinzi wa kulia Juma Abdul aliyejifunga mwenyewe mnamo dakika ya 11 na kuiweka Azam mbele ndani ya Uwanja wa Taifa.

Hata hivyo dakika ya 29 ya mchezo ikamshuhudia mlinzi huyo wa Yanga akirekebisha makosa yake kwa kuifungia timu yake bao la kusawazisha baada kukutana na mpira uliojaribu kuondoshwa kwenye hatari.

Dakika sita kabla ya filimbi ya kuashiria mapumziko kupulizwa, Donald Ngoma akawaweka Yanga mbele kwa bao rahisi la kichwa baada ya majaribio kadhaa ya Amis Tambwe kushindwa kufua dafu kwa golikipa Aishi Manula.

Matokeo yalibaki vinara wa Ligi Kuu Bara Yanga wakiongoza 2-1 mbaka pale mwamuzi Kennedy Mapunda alipopuliza kipenga cha kuashiria mapumziko.

Dakika takriban ya 4 baada ya kipindi cha pili kuanza mshambuliaji Donald Ngoma alilazimika kutolewa nje ya uwanja baada ya kuumia.

Timu ziliendelea kushambuliana kwa zamu kwenye mchezo huo uliojaa msisimko huku kukiwa hakuna nafasi iliyoweza kuzaa bao mbaka pale nahodha John Boko alipoipatia timu yake bao maridadi la kusawazisha mnamo dakika ya 71.

Dakika mbili kabla ya dakika tisini za mchezo kumalizika Simon Msuva akachezea nafasi ya wazi ya kuipatia timu yake bao la ushindi akiwa uso kwa uso na golikipa aliyepangua shuti lake dhaifu.

Kwa matokeo hayo Yanga wanaendelea kushika usukani kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na alama 47 baada ya kucheza michezo 20.

Azam FC ambao pia wamecheza mchezo wao wa 20 hii leo wanabaki kwenye nafasi yao ya pili wakiwa na alama 47 sawa na vinara Yanga ila wakiachwa nyuma kwa idadi ya tofauti ya mabao.

Wekundu wa Msimbazi Simba walio kwenye nafasi ya tatu wakiwa wamekusanya alama 45 wao watatupa karata yao kesho kwenye mchezo wao wa 21 msimu huu dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam.

Vijana hao wa Jackson Mayanja wanahitaji alama tatu muhimu kwenye mchezo huo ili kujikita kileleni mwa msimamo huo angalau kabla ya Azam na Yanga kucheza viporo vyao.

 

 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

JE UMEFIKA WAKATI WA ARSENE WENGER KUFUNGA VIRAGO?

Tanzania Sports

Simba yarejea kileleni