Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati Azam FC wameondolewa kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupokea kipigo cha 3-0 kutoka kwa Esperance ndani ya dimba la Olymique de Rades huko jijini Tunis usiku huu.
Esperance walifanya mashambulizi kadhaa ya hatari kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo lakini golikipa Aishi Manula alifanya kazi ya ziada na kuwafanya Azam wamalize kipindi hicho cha kwanza bila kuruhusu bao.
Dakika tatu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Esperance wakapata bao la kuongoza kupitia kwa kiungo wao Saad Bguir aliyeunganisha mpira wa adhabu uliochongwa na Ben Youssef.
Ndani ya dakika ya 62 ya mchezo mabingwa hao mara mbili wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakaongeza bao la pili lililowekwa wavuni na mshambuliaji wao Haithem Jouini.
Kuwa nyuma kwa mabao mawili kuliwafanya Azam wazidi kupambana kujaribu kutafuta angalau bao moja ambalo lingeufanya mchezo uamuliwe kwa mikwaju ya penati.
Matumaini ya Azam yakazima ndani ya dakika ya 82 ya mchezo pale Ben Youssef alipowaongezea Esperance bao la tatu akipokea pasi kutoka kwa Haithem Jouini aliyepachika bao la pili.
Mwamuzi wa akiba akaongeza dakika nne baada ya kumalizika kwa dakika 90 za mchezo lakini Azam walishaonekana kukata tamaa kwa kuwa walikuwa wanahitaji mabao mawili ili waweze kusonga mbele.
Matokeo haya yanawafanya Esperance kuibuka na ushindi wa jumla wa 4-2 na baada ya kuwa walipokea kipigo cha 2-1 kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa ndani ya dimba la Chamazi siku kadhaa zilizopita.
Ushindi huo unawapeleka Esperance kwenye raundi ya mwisho ya mtoano watakayocheza dhidi ya moja kati ya timu zitakazoondolewa kwenye raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Wakivuka kwenye hatua hiyo wataingia kwenye hatua ya makundi.