Yanga wamevamia tena Asec Mimosas kwa kumsajili Kouassi Yao ambaye ni beki wa kulia. Usajili wa Kouassi Yao una maana vita ya namba kwa beki wa kulia itakuwa kali, kwani Yanga inao wachezaji watatu, Dickson Job, Kibwana Shomari na Djuma Shaban……
UPEPO mtamu wa mpira wa miguu unavuma toka nyumbani Tanzania. Ni upepo unaovutia barani Afrika huku makumi ya wachezaji na makocha wakitafuta fursa za kufanya kazi Ligi Kuu Tanzania. Hakika hii ni hatua nzuri kukuza soka letu na ukanda wa Afrika Mashariki.
TANZANIASPORTS imefuatilia kwa ukaribu hekaheka za usajili wa wachezaji kutoka nje ya Tanzania. Miamba ya soka Yanga na Simba wananyukana kuwinda saini za nyota wa kimataifa ili waje kucheza Ligi Kuu Tanzania. Miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa mstari wa mbele kwa nyota wake kutua Tanzania ni Ghana, Nigeria, Ivory Coast, DRC, Kenya na Uganda. Nchi ambazo hazijatikisa Tanzania ni zile za Kiarabu ambako soka nalo limeanza kunyemelewa na mastaa kutoka nchi nyingi za kigeni kuliko kutegemea nyota wao. Pengine hatuna idadi kamili lakini wanasoka kutoka Afrika magharibi,mashariki,kusini wameelekea kaskazini.
Miongoni mwa vilabu vinavyoshangaza katika miaka ya karibuni ni Asec Mimosas. Hii ni miamba ya soka kutoka Ivory coast. Ni miamba ambayo imetikisa kwenye mashindano karibu yote ya CAF. Unapotaja jina la Asec Mimosas unawataja nyota kama Yaya Toure ambaye alikipiga klabu hiyo ya kwao na imefanikiwa kuwatoa nyota wengi kwenda barani Ulaya.
Unapozungumzia Asec Mimosas ni kuiweka daraja moja na vilabu kama Raja Casablanca (Morocco), Enyimba (Nigeria), Esperance(Tunisia), Club Africain (Tunisia), Mamelodi Sundowns (Afrika kusini), Orlando Pirates (Afrika kusini), JS Kabylie (Algeria), TP Mazembe (DRC), DC Motema Pembe (DRC), Ismailia (Misri), Zamalek (Misri), Al Ahly (Misri), Etoile Du Sahel (Tunisia), Nkana Red Devil(Zambia), Power Dynamos (Zimbabwe) na nyinginezo. Kama unaangalia historia za vilabu hivi utaona vina ukongwe kwenye soka la Afrika. vingi ni vile ambavyo vimechuana vilivyo kwenye mashindano ya CAF.
Ni timu zinazopewa heshima kubwa kutokana na kile walichofanya kwenye soka. Mastaa wengi miaka ya nyuma toka nchi kama Nigeria walitamani kwenda kujiunga na Asec Mimosas au timu kama hizo zilizotajwa hapo juu kama njia ya kuelekea ulaya. Wengi waliamini ukipita Esperance kama Julius Aghahowa basi safari yako ya Ulaya inakuwa nyepesi. Ukongwe wa Asec Mimosas umejengwa na heshima ya soka maridadi. Utamaduni wao wa kucheza mpira uko wazi, pasi nyingi, fupi kutawala mchezo na kuwapa nafasi wachezaji wanaoneshe vipaji. Utamaduni wao wa soka ni kivutuio sana.
Hata hivyo mambo yamebadilika kwa kasi kubwa. Asec Mimosas ni kama vile ilivyokuwa wakongwe wenzano Club Africain, Etoile Du Sahel, Esperance, Power Dynamos zilipoteana kwenye mashindano ya CAF. Asec Mimosas iliyokuwa inatetemesha kwenye kwa mchezo mzuri kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam sio hii ya sasa. Kwa sasa Asec Mimosas imekuwa kama akademi ya Yanga na Simba za Tanzania.
Wakati zamani Yanga na Simba zilikuwa zinatetemeshwa ndani ya dimba kwa kuzidiwa mchezo, lakini sasa Asec Mimosas imezidiwa vyote viwili, fedha na mchezo uwanjani. Rekodi za misimu mitano sasa Asec na wakongwe wenzake hawajafua dafu ukiwaacha Raja, Al Ahly na Mamelodi Sundowns ambao wamekuwa wakifukuta mara kwa mara. Lakini Asec Mimosas imekwenda chini katika mahsindano ya Afrika. ingawaje Asec Mimosas ni mabingwa wa biashara ya wachezaji barani Afrika, na inachukuliwa kama kisima cha kuzalisha vipaji na vilabu vingi vya Ulaya.
Mawakala sehemu mbalimbali duniani wanaitazama Asec Mimosas kama sehemu sahihi ya kuvuna vipaji. Sasa, Yanga na Simba nao wameingia kwenye vita vya wababe kwa kusajili wachezaji tegemeo wa Asec Mimosas. Walianza watani wao jadi Yanga ambao walimsajili Stephanie Aziz Ki, kiungo mchezeshaji mwenye mashuti makali. Ni miongoni mwa vipaji vizuri kuzalishwa na Asec Mimosas.
Kana kwamba haitoshi, Yanga wamevamia tena Asec Mimosas kwa kumsajili Kouassi Yao ambaye ni beki wa kulia. Usajili wa Kouassi Yao una maana vita ya namba kwa beki wa kulia itakuwa kali, kwani Yanga inao wachezaji watatu, Dickson Job, Kibwana Shomari na Djuma Shaban ambao wanaweza kutumikia nafasi hiyo. Uzuri ni kwamba Dickson Job anacheza nafasi zote za beki na kiungo mkabaji, sawa na Kibwana Shomari anayemudu beki wa kulia na kushoto, wakati Djuma Shaban anaweza kuchezeshwa winga wa kulia. Akiwa Vita FC alionesha hilo.
Watani wao wa jadi Simba nao wamekamilisha usajili wa Kramo Aubin kwenye dirisha hili akitokea Asec Mimosas. Hapo ndipo utaona kuwa wachezaji watatu tegemeo wa Asec Mimosas wamesajili na timu za Ligi Kuu Tanzania. Ubabe wa Asec Mimosas ni kama vile umepitwa na wakati, huku vilabu vya Tanzania vilivyokuwa vinyonge zamani sasa vinawanyoa wakongwe ndani na nje ya uwanja.
Zamani Simba na Yanga zilikuwa zinapigwa pigwa na wakali wa Afrika magharibi, lakini sasa nazo zinawachapa uwanjani na kiuchumi. Kivutio kikubwa cha Ligi Kuu ni ile hali ya timu kuwa na uwezo wa kuwalipa mishahara minono wachezaji wa kigeni, hivyo nao huvutiwa kuja kucheza soka Tanzania. Isingekuwa rahisi miaka ile kwa wachezaji hao kuja Tanzania, lakini sasa mambo yamebadilika. Asec Mimosas nao wamekuwa kama akademi ya Yanga na Simba kuvuna wachezaji.
Comments
Loading…