in , , ,

ASANTE TFF NA MARCH, APRIL IBEBE MAY

Siku zinakimbia sana na hii yote ni kuonesha hakuna nafasi kwa siku
kurudisha nyuma muda. Muda unapopita huenda lakini hutuachia
kumbukumbu za furaha na huzuni katika maisha yetu.

Kama ilivyongumu kuzuia nyakati nyepesi na ngumu katika maisha ndivyo
ilivyo ngumu kuzuia siku kwenda mbele.

Siku zinapokwenda mbele hutoa tafasri ya kweli kuhusu maendeleo.
Maendeleo hupatikana kwa hatua za mbele, hakuna maendeleo
yanayopatikana kwa mtu yoyote kupiga hatua za nyuma, ndivyo zilivyo
siku ambazo huhesabika kwa kwenda mbele. Hakuna mawio yaliyoruhusu
siku kurudi nyuma. Kila hatua za siku hutuacha na kumbukumbu akilini
mwetu.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa kipindi cha Leodegar Chilla Tenga timu ya
Taifa iliwahi kushika nafasi ya 86 katika viwango vya dunia
vinavyotolewa na FIFA.

Furaha ilifunika nyuso zetu, tabasamu lilitawala kati yetu, imani
kubwa juu ya timu ya Taifa iliongezeka kwa kiasi kikubwa.

Hamasa ilikuwa kubwa sana kipindi kile, ni kipindi ambacho timu ya
Taifa iliungwa kwa kiasi kikubwa sana na viongozi wa serikali, TFF ,
mashabiki pamoja na wadau mbalimbali wa michezo.

Nguvu kubwa iliongezeka katika kikosi cha timu ya Taifa. TFF na
Watanzia walifanya jitihada kubwa sana ya kuwafanya vijana wa timu ya
Taifa kupigana kwa kiasi kikubwa sana. Uzalendo ulikuwa unatembea
kwenye mishipa ya damu ya wachezaji wa timu ya Taifa.

Imani ilijaa kwenye mioyo yao, waliona taifa ƙliko nyuma yao
likiwapigania na kuwaombea.

Ndiyo maana hawakuogopa vita yoyote iliyokuwa inakuja mbele yao. Kwao
ilikuwa kawaida kuibeba tembo mgongoni na kuitupa kwenye mto. Ndiyo
maana halikuwa jambo la kushangaza kwa Taifa Starz kuifunga timu kama
Burkinafaso.

Muda ulisogea na kukaribisha majira mbalimbali kwenye soka, upepo
ukawa mbaya tena hali ilianza kurudi nyuma tena .

Tukazidi kushuka tena kwenye viwango vya FIFA mpaka wengine walidiriki
kusema tunaporomoka.

Hii yote ilitoa nafasi ya neno halisi ya maendeleo, maendeleo huja na
changamoto ambazo ni chanya na hasi. Hakuna sehemu ambayo inahisia
moja kwenye maisha.

Kwenye maisha kama hujawahi kuonja furaha na huzuni kwa nyakati
tofauti ya maisha yako basi kaa ukijua hujaanza kuishi. Changamoto
hasi hazikwepeki katika maisha ndiyo maana wahenga walipata nguvu ya
kutuambia kuwa maisha ni kupanda na kushuka.

Ndicho kilichotokea kwetu, tulipanda mpaka nafasi ya 89 lakini
tulishuka mpaka nafasi ya 157 .

Imani kwa timu ya Taifa kutoka kwa Watanzania ilianza kupotea
taratibu. Hamasa ikaenda likizo, hakuna mtu aliyehamasika kwa kiasi
kikubwa tena kununua jezi ya timu ya Taifa na kwenda nazo uwanjani
kuishangilia timu ya Taifa.

Tukabaki kunyoosheana vidole na kusahau kabisaa madhara ya
kunyoosheana vidole wakati tukiwa shambani tunalima kwa pamoja.

Mzigo wa lawama haukukwepeka kwa TFF, TFF hakunyong’onyeshwa na lawama
walizokuwa wanatupiwa. Walichokifanya ni wao kukaa chini na kuwaza
jinsi gani ya kuondoa lawama zile .

Mabadiliko yalihitajika na ndicho kitu ambacho kilifanyika. Benchi la
ufundi lilibadilishwa ingawa wengi wetu hatukuunga mkono mabadiliko
yale.

TFF haikutetereka kwenye maamuzi yao, waliwaamini watu walioteuliwa
kwenye benchi la ufundi la timu ya Taifa. Wakapewa muda wa kukaa kambi
nzuri kwa muda ambao ungetosha kujenga mahusiano mazuri kwa wachezaji
na kikubwa zaidi wakawatafutia timu ambazo zilikuwa juu ya Tanzania
kwenye viwango vya FIFA.

Kuwaleta Botswana na Burundi ilikuwa shabaha kubwa sana kwa TFF kuipa
nafasi timu ya Taifa kupanda kwenye viwango vya FIFA endapo
wangezifunga.

Ni aibu kubwa sana kumwangusha mtu aliyekuamini umbebe katika mgongo wako.

Ndicho walichokifanya benchi la ufundi pamoja na wachezaji wa timu ya
Taifa. Waliwabeba vizuri TFF ambao kwa wakati huo wao pekee ndiyo
walionekana wapo nyuma yao kwa kiasi kikubwa.

Hawakuwaruhusu Botswana wapate ushindi Taifa, hamasa iliongezeka kwa
kiasi kikubwa sana kwa Watanzania baada ya mechi ile.

Mitandao ya kijamii ilipendezeshwa na jumbe nzuri za kuisifu timu ya
Taifa. “Kumbe inawezekana”! ndiyo kauƙiliyobaki kwenye vinywa vya
Watanzania baada ya mechi ile. Kitu ambacho kiliruhusu tena Watanzania
kupata nguvu ya kuishabikia timu yao ya Taifa mechi iliyofuata dhidi
ya Burundi, hawakuangushwa tena na wachezaji.

Mwezi wa nne FIFA haikuwaangusha Watanzania, ikawapandisha juu kwa
viwango 22 kutoka nafasi ya 157 mpaka nafasi ya 135. Shabaha ya TFF ya
kuwaleta Botswana na Burundi ikawa imefanikiwa kwa asilimia kubwa.

Huu ni upya mzuri kwetu sisi kurudi tena kwenye ile nafasi za mia bora.

Kuna faida kubwa sana ya kuwa kwenye mia bora katika nafasi za FIFA
kwani pamoja na kwamba tutapata nafasi ya kucheza mechi za kirafiki
kwa wepesi na timu kubwa zilizo nafasi za juu tofauti na kuwa nje ya
mia bora pia tutakuwa na nafasi ya kupangwa moja kwa moja kwenye hatua
za makundi ya kuwania kufuzu Afcon au World kubwa na kuepuka kuanza
safari hii kwenye hatua ya mtoano.

Ndiyo maana pamoja na kuwashukuru TFF na mwezi mechi, ila nawakumbusha
tena tufanye Kila linalowezekana mwezi huu wanne uubebe mwezi wa tano ili
tupande kwenye nafasi za juu zaidi.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NAFASI NZURI KWA MAKAMPUNI KUNUFAIKA KIBIASHARA NA SERENGETI BOYS

Tanzania Sports

NILICHOKIONA KWENYE MECHI ZA UEFA.