Kila mshabiki wa mpira na wengine pia hushangaa na kutokubali kiasi kikubwa cha fedha ambacho hulipwa wachezaji wa ligi mbalimbali za Ulaya.
Mishahara ya wachezaji wanane wanaoongoza, inaanzia paundi za Uingereza laki mbili elfu kwa juma. Hizi ni zaidi ya dola milioni moja na nusu kwa mwezi. Wachezaji hawa matajiri ni Wayne Rooney (£300,000), Lionel Messi (£292,000), Cristiano Ronaldo (£288,000), Robin Van Persie (250,000), Yaya Toure (£230,000), Luis Suarez (£220,000), Sergio Aguero (£220,00) na David Silva (£200,000).
Anayeongoza (Wayne Rooney) ni mchezaji wa ligi ya England. Wengine wote ukiacha Ronaldo na Messi pia huchezea timu zilizoko Uingereza.
Ligi kuu ziko Spain, Italia, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi na Uingereza. La Liga (Primera Division) ya Spain inadaiwa kuwa na fedha na ushabiki mkubwa unaofikia watazamaji zaidi ya milioni kumi na nusu kila msimu. La Liga imeshinda vikombe vingi zaidi kupitia timu za Real Madrid na Barcelona. Bundesliga ya Ujerumani inayo watazamaji zaidi ya milioni kumi na tatu. Wastani wa wachezaji wa kigeni Ujerumani, Italia, Spain, Ufaransa na Uholanzi ni wanasoka 25. Kiasi hicho ni kikubwa zaidi katika Premier League ya England yenye wastani wa wachezaji 30 toka ugenini na michezo inayowasukuma sana wachezaji. Ni mambo haya mawili yaliyoifanya timu ya England kutoshinda vikombe vyovyote vya kimataifa toka mwaka 1966 ilipochukua kombe la dunia.
England imetoa majina makubwa ya David Beckham, Wayne Roooney, Steve Gerard, Theo Walcott na kijana Raheem Sterling aliyetingisha Brazil, lakini haijafanya vizuri. Kocha wa Ujerumani , Joachim Low, alipohojiwa Brazil, alitaja moja sababu kuu za England kuzubaa ni kuwapa kipaumbele wachezaji wa kigeni. Ligi ya England imejazana wageni wenye majina makubwa, yaani Didier Drogba, Mario Balotelli na Eddie Hazzard. Hali hii haisaidii mpira wa England.
Tatizo la pili, ambalo limeongelewa miaka mingi na makocha ni mwenendo mzima wa michuano ya ligi ya England (Premier League). Wachezaji wa nchi nyingine huwa na mapumziko wakati wa kiangazi (Julai-Agosti) na baridi kali (Novemba na Desemba). Mapumziko haya huwafanya wachezaji wawe na nguvu na wanapoitwa kuchezea timu zao za kitaifa hutoa mchango wa kufaa.
Kocha aliyeongea sana ni Arsene Wenger wa Arsenal. Alipohojiwa Ijumaa iliyopita kabla ya mechi ya timu yake na Liverpool, Wenger alikiri wachezaji wake wageni hawajazoea desturi ya mechi msimu wa Krismasi kama Wajerumani Mesut Ozil, Per Metersacker, Lukas Podolski au mshambuliaji wa Chile- Alexis Sanchez. Kocha Wenger alisema ni kawaida kupumzika na familia sikukuu ya Krismasi, lakini siyo katika ligi ya England. Wachezaji hucheza kustarehesha watu siku za mapumziko.
Wenger aliwataka wachezaji wake wawe na moyo na akili tulivu na kusisitiza kuwa wakimudu kukipita kipindi hicho watafanya vizuri mwanzo wa mwaka ujao. Wenger anaonyesha kuwa michezo si tu ufundi wa mwili, bali pia akili timamu, kujituma na nidhamu. Fikra hii inaonyesha namna ambavyo kipato kikubwa wanachokipata wanasoka na wanamichezo wengine kinavyofidia kujitolea kwao mhanga. Wanasoka hucheza katika mvua, matope na ajali za wachezaji waliopigwa na radi katika mvua, kuumia au hata kufa uwanjani ni nyingi sana, kitakwimu katika mpira.
Comments
Loading…