in , , , ,

Arsenal wawatimulia vumbi Dortmund


Chelsea, Barcelona wapata ushindi mzuri

 
Ligi ya Mabingwa Ulaya imeingia patamu baada ya matokeo mchanganyiko kwenye mechi za usiku wa kuamkia Alhamisi hii.

Washika Bunduki wa London – Arsenal wanaoongoza Ligi Kuu ya England, waliwanyanyasa Borussia Dortmund nyumbani kwao Ujerumani kwa kuwafunga bao 1-0.

Hiyo ilikuwa kulipiza kisasi baada ya wenyewe kufungwa Emirates mabao 2-1 kwenye mechi ya awali wiki mbili zilizopita na sasa Arsenal wanaendelea kuongoza kwenye kundi lao.

Dortmund walicheza vyema mbele ya maelfu ya washabiki wao, lakini Arsenal hawakuonesha papara ya kushambulia, bali walihakikisha ulinzi na kiungo kizuri.

Kipa wao, Wojciech Szczesny alionesha kiwango cha hali ya juu kwa kuzuia hatari za mabao kutoka kwa Marco Reus na Jakub Blaszczykowski na kuwaridhisha washabiki 3,500 waliosafiri kutoka London kuwaunga mkono.

Arsenal walipata bao lao muhimu katika dakika ya 62 kupitia kwa mchezaji aliye kwenye fomu sasa, Aaron Ramsey, aliyefuatia kichwa cha Olivier Giroud karibu kabisa na goli baada ya Mjerumani Mesut Ozil kuwachotea mpira safi. Hiyo ilikuwa baada ya gonga nzuri za Tomas Rosiscky na Ramsey kuliendea lango la wenyeji wao.

Nusura Ramsey aongeze bao la pili muda mfupi tu baadaye, lakini kwa hilo moja, walionekana kutosheka na kocha wa Dortmund, Jurgen Klopp akasema Arsenal wanaweza kufika mbali.

Wanakuwa timu ya kwanza ya Uingereza kushinda katika uwanja wa Dortmund wa Westfalenstadion na wanaendeleza rekodi yao ya kutofungwa katika mechi 14 za ugenini. Mwaka jana waliwafunga Bayern Munich nyumbani kwao Allianz Arena.

Mechi walizobakia nazo Arsenal ni dhidi ya Marseille katika uwanja wa Emirates Novemba 26 kisha wakawakabili Napoli Desemba 11 nchini Italia.

Arsenal wanashika nafasi ya kwanza kwa pointi tisa wakifuatiwa na Napoli wanaofundishwa na Rafa Benitez wenye idadi hiyo hiyo ya pointi, kisha Dortmund wamebaki na pointi zao sita huku Marseille wakiwa hawana pointi.
 
ETO’O AWANG’ARISHA CHELSEA
 
Mchezaji wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o aliyesajiliwa msimu huu ameonesha cheche zake baada ya kuwafungia Chelsea mabao mawili dhidi ya Schalke 04.

Katika dimba la Stamford Bridge, Eto’o alitumia makosa ya kipa Timo Hildebrand aliyekuwa akichezea mpira kwenye eneo lake, akamzonga na kufunga kirahisi bao la kwanza.

Wajerumani hao walianza vizuri na nusura wapate mabao mara mbili lakini Julian Draxler na Adam Szalai walipiga mipira nje.

Eto’o alifunga bao la pili baada ya kupokea pasi ya Willian kuachia mkwaju mkali kabla ya mshambuliaji mwingine aliyezoeshwa benchi, Demba Ba kuandika bao la tatu.

Huu ulikuwa ushindi wa 100 kwa Chelsea katika historia ya mashindano ya Uefa na kwa kundi lao unawaacha wakiongoza kwa tofauti ya pointi tatu na iwapo watashinda mechi ijayo dhidi ya Basel watajihakikishia kusonga mbele kwenye 16 bora.

Eto’o alichezeshwa badala ya Fernando Torres aliyeumia na ushindi huu umekuja baada ya Chelsea kushangazwa na kipigo kutoka kwa Newcastle cha 2-0 kwenye EPL.
 
KICHEKO TIMU ZA HISPANIA
 
Timu mbili za Hispania, Atletico Madrid na Barcelona zimejihakikishia kuvuka hatua hii, ambapo Madrid waliwapiga Austria Vienna 4-0 na Barca wakawashinda AC Milan kwa mabao 3-1.

Hata hivyo, bao la kwanza la Barca lililopatikana kwa penati, lilionekana kama uonevu kwa Milan, kwa sababu Neymar alikuwa kama alijiangusha akifananishwa na Ashley Young alivyofanya usiku wa Jumanne kwenye mechi dhidi ya Real Sociedad na kuzaa penati iliyoota mbawa.

Katika mechi nyingine, Basel walikewenda sare ya 1-1 na Steua Bucharest; Zenit wakatoka 1-1 na Porto, Napoli wakawapiga Marseille 3-2 na Ajax wakawashinda Celtic 1-0.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Arsenal 1 -Dortmund 0

Ashley Young ashutumiwa kujirusha