*Watoa £milioni 40 na pauni 1 kumtwaa Suarez
*Watumia kipengele kilichomsajili, aitaka Arsenal
Arsenal wameonyesha nia yao ya kutaka kumsajili mpachika mabao wa Liverpool, Luis Suarez, ambaye sasa amesema anataka kuzungumza nao.
Arsenal wametumia kifungu cha mkataba wake kwa kutoa dau la pauni milioni 40 na pauni moja.
Hiyo ni historia kwa klabu hiyo inayonolewa na Arsene Wenger, lakini bado Liverpool wamekataa dau hilo, ambalo ni la pili kutoka Arsenal msimu huu wa usajili.
Pamoja na kukataa kwao, ilikuwa lazima Suarez aelezwe juu ya dau, kwa sababu kuna kifungu kwenye mkataba wake kinachosema hivyo, na anaweza kushinikiza mazungumzo yaanze sasa.
Dau la kwanza lilikuwa la pauni milioni 30, ambalo Liverpool ililikataa mara moja na kusema kwamba mchezaji huyo raia wa Uruguay mwenye umri wa miaka 26 hauzwi.
Baada ya dau la sasa, Liverpool wamekasirika na kudai kuwa thamani ya mchezaji wao huyo tegemeo ni pauni milioni 55, na kwamba kuongeza zaidi ya pauni milioni 40 hakumwondoi Suarez kwao.
Suarez mwenyewe tayari ameripotiwa akisema kwamba anataka kuanza mazungumzo na Arsenal, kwani alishasema tangu awali angependa kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Suarez amesema anataka kuzungumza na Arsenal, kwani anaamini tayari wametoa dau linaloweza kutengua mkataba wake Anfield, lakini Liverpool wanatafsiri tofauti kipengele hicho.
Walichofanya Arsenal safari hii ni kutoa ofa ya pauni milioni 40 jumlisha pauni moja, hesabu ambazo zinatengua kipengele kinachomweka Suarez Anfield, na kutaka mazungumzo yaanze.
Arsenal wameweka nguvu zao kwa Suarez baada ya mpango wa kumchukua Gonzalo Higuain wa Real Madrid ulioonekana kama ulikaribia kukamilika kutibuka baada ya Carlo Ancelotti kuteuliwa kufundisha klabu hiyo badala ya Jose Mourinho.
Kifungu cha mkataba wa Suarez kinasema lazima mchezaji huyo ajulishwe ikiwa dau limefika au kuzidi pauni milioni 40. Real Madrid nao wanadaiwa kumtaka mchezaji huyo, lakini kwa kumzuia Higuain kuondoka, huenda wasiendeleze dau kwake.
Walipowasilisha dau la pauni milioni 30, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Arsenal, Ivan Gazidis alijulishwa na mwenzake wa Liverpool, Ian Ayre kwamba wala wasingefikiria dau la pauni milioni 40. Wakati huo, Arsenal walikuwa tayari kuongeza pauni milioni 5 ili ziwe 35.
Suarez ndiye mfungaji bora wa Liverpool msimu uliopita na wa pili katika Ligi Kuu ya England (EPL) na amejiunga na wenzake siku moja iliyopita akitoka kupeperusha bendera ya nchi yake pamoja na likizo fupi.
Liverpool wanamchukulia Suarez kuwa mchezaji mzuri kuliko Fernando Torres aliyeuzwa Chelsea Januari 2011 kwa pauni milioni 50. Kocha Brendan Rodgers amekuwa akisisitiza kwamba Suarez atabaki Anfield.
Rodgers alikuwa akimfananisha Suarez na raia mwenzake wa Uruguay, Edinson Cavani aliyeuzwa
Paris Saint-Germain ya Ufaransa kutoka Napoli ya Italia kwa pauni milioni 55.6.
Comments
Loading…