*Chelsea wazindukia Romania
*Man City na Man U kibaruani
Moto uliowashwa na Arsenal umeendelea kuteketeza wapinzani wake, baada ya usiku wa Jumanne hii kuwachapa Napoli 2-0.
Wakicheza mbele ya umati wa washabiki wao nyumbani Emirates, Arsenal wamekwea kwenye uongozi wa kundi lao la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Alikuwa ni Mesut Ozil aliyenunuliwa kwa dau la kuvunja rekodi msimu huu aliyefunga bao la kwanza dakika ya nane kabla ya kumtengenezea pande Olivier Giroud aliyetikisa nyavu dakika ya 15.
Baada ya mabao hayo Napoli wa Italia wanaofundishwa na kocha wa zamani wa Liverpool na Chelsea, Rafa Benitez walijaribu kuzinduka na kufanya mashambulizi, lakini yaliokolewa na Arsenal.
Pamoja na Napoli kukosa shabaha kwa wengi wa washabuliaji wake kupiga mipira juu, mingine ilikabwa vyema na mabeki na viungo wa Arsenal na michache kuishia mikononi mwa golikipa Wojciech Szczęsny.
Katika mechi ambayo hapakuwa na mchezaji yeyote aliyeoneshwa kadi ya nyekundu wala ya njano, kipa wa Napoli, Pepe Reina aliokoa hatari nyingi langoni mwake wala hana lawama kwa mabao mawili ya kifundi na kishindo ya Arsenal.
Washika Bunduki wa London walitamba zaidi kwenye kiungo, ambapo licha ya kutokuwapo Santi Cazorla ambaye ni majeruhi, Kocha Arsene Wenger alithubutu kumwacha mtaalamu Jack Wilshere kwenye benchi hadi kipindi cha pili, akiwaamini Ozil na Aaron Ramsey ambao walifanya kazi yake vyema.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Borussia Dortmund wa Ujerumani walizinduka na kuwafunga Marseille mabao 3-0. Katika mechi iliyopita, Dortmund walifungwa na Napoli wakati Arsenal waliwafunga Marseille wa Ufaransa.
Bayern Leverkusen watacheza na Real Sociedad; Juventus na Galatasaray waliopata kocha mpya katika Roberto Mancini; Real Madrid watawakaribisha FC Kobenhavn; Paris Saint Germain watavaana na Benfica; RCS Anderlecht wanacheza na Olympiakos wakati CSKA Moscow wanacheza na Viktoria Plzen.
Comments
Loading…