ENDAPO Arsenal itashindwa kuchukua ubingwa msimu huu utakuwa ni kitu cha kushangaza sana. Arsene Wenger anazo sababu nyingi mno za kutwaa ubingwa huo kuliko timu nyingine licha ya kufungwa na Chelsea wiki iliyopita bao 1-0 lililofungwa na Diego Costa.
Hebu tuone matokeo ya mechi za Arsenal dhidi ya Chelsea ambayo ilishuhudia beki Per Matersacker akifanya makosa mawili; kwanza kumwangalia mshika kibendera kama anaashiria Diego Costa ameotea, kisha akafanya kosa la kumchapa daruga.
TAZAMA MECHI HIZI:-
Ifuatayo ni orodha ya mechi ambazo Chelsea imewahi kuitibulia Arsenal katika misimu tofauti.
Chelsea 3-1 Arsenal (Februari 18, 1998)
Ilikuwa marudiano ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Ligi. Chelsea ilikuwa na hali mbaya kiasi cha kumtimua kocha wake Ruud Gullit zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kukwaana na Arsenal.
Gianluca Vialli aliyerithi mikoba ya Gullit kama kocha mchezaji alipindua matokeo na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 baada ya kuwa wamefungwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza.
Wafungaji wa Chelsea walikuwa Mark Hughes, Roberto Di Matteo na Dan Petrescu, huku bao la Arsenal likifungwa na Denis Bergkamp.
Tangia hapo ni kama vile Arsenal imepata gundu kwani haijawahi tena kupata bahati ya kutwaa taji la michuano ya Kombe la Ligi chini ya Arsene Wenger.
Arsenal 1-2 Chelsea (April 6, 2004)
Hii ilikuwa marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kabla ya mechi hiyo, Arsenal ilikuwa na rekodi nzuri ya kutopoteza mchezo wowote kati ya 17 waliyokuwa wamekutana na Chelsea kipindi cha nyuma, hivyo kuwa na uhakika wa ushindi.
Timu zilipokuwa zikiingia uwanjani matokeo yalikuwa yakisomeka 1-1 baada ya kuwa zimetoka sare ya idadi hiyo katika mechi ya awali, iliyopigwa katika dimba la Enirates.
Mechi ilipoanza, Arsenal walionekana kama wangeweza kuibuka na ushindi baada ya Jose Antonio Reyes kuifungia timu hiyo bao la kuongoza kipindi cha kwanza. Hata hivyo Frank Lampard alianza kufifisha matumaini ya vijana hao wa Wenger baada ya kuisawazishia timu yake bao kipindi cha pili na baadaye Wayne Bridge akaongeza jingine.
Arsenal 1-2 Chelsea (Aprili 18, 2009)
Ilikuwa ni mechi ya michuano ya Kombe la FA na Chelsea wakati huo ikiwa chini ya kocha huyu wa sasa Guus Hiddink ambaye alikuwa amepewa jukumu la kuinoa kwa muda.
Katika dimba la Wembley, Arsenal ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na jinsi timu yao ilivyokuwa na dalili zilianza kuonekana mapema baada ya Theo Walcott kufunga bao la kuongoza.
Wakati watu wakiendelea kusubiri kushangilia ushindi, Florent Malouda akasawazisha na baadaye kidogo Didier Drogba akaongeza la pili na kumfanya Hiddink kuibuka mbabe kwenye michuano hiyo ya Kombe la FA.
Arsenal 0-3 Chelsea (Novemba 29, 2009)
Ilikuwa mechi ya Ligi Kuu ya England, ambapo Arsenal ilikuwa ikipewa nafasi kubwa kwenye mbio za ubingwa lakini matokeo ya mechi hiyo ndiyo yaliyoinyong’onyeza kabisa baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-0.
Washika bunduki hao wa jiji la London waliamini kwamba kikosi chao chini ya Arsene Wenger kilikuwa na ubora wa kutosha kuweza kutwaa taji kwa msimu huo baada ya kulikosa kwa muda mrefu. Lakini Didier Drogba alipeleka maafa makubwa baada ya kufunga bao lake la kumi katika mechi tisa alizocheza dhidi ya Arsenal.
Chelsea 6-0 Arsenal (Machi 22, 2014)
Arsenal ilishuka dimbani huku ikimsindikiza kocha wake Arsene Wenger kusherehekea mechi yake ya 1000 ya kimashindano ndani ya kikosi hicho tangu alipoajiriwa.
Hata hivyo sherehe hizo ziliingia luba baada ya Chelsea kuitibua kwa kuwapa kipigo hicho cha mbwa mwizi cha mabao 6-0 ndani ya dimba la Stamford Bridge.
Matokeo ya mechi hiyo yalidhihirisha kwamba Arsenal haitapenda tena kukutana na Chelsea hasa linapokuja suala la kuwa na matarajio ya kusaka taji la ubingwa au kupata matokeo mazuri. Katika mchezo huo Chelsea waliweza kutumia dakika 17 tu kufunga mabao matatu na mwisho wa mchezo kikosi hicho chini ya kocha Jose Mourinho kilishinda 6-0.