in , , , ,

Arsenal waenda kileleni UCL

Huku Martinelli akihakikisha ushindi dhidi ya Bayern Munich

Rafiki yangu mmoja, alinipigia simu jioni sana jana kabla ya mchezo, na kuniomba niende mpirani badala yake kwani baridi ilikuwa kali sana, nami nikamwambia hapana aisee, hii baridi ni noma, najuta, ningeenda tu….kwa tiketi ya bure na kwa matokeo haya…..

Mechi hii ilitangazwa kama pambano la vigogo wawili wa Ulaya, na kwa muda mwingi wa jioni ya jana kulikuwa na baridi sana, kaskazini mwa London ilionekana kama uko Lushoto. Mchezo wa kusisimua uliobadilika mara kwa mara uliona kijana chipukizi wa Bayern Munich, Lennart Karl, akifuta bao la ufunguzi la Jurrien Timber kutoka kona, kabla ya wachezaji wa akiba Noni Madueke na Gabriel Martinelli kukamilisha ushindi uliostahili kwa wenyeji. Arsenal wanaendeleza rekodi yao ya asilimia 100 kwenye Ligi ya Mabingwa na sasa wanapanda kileleni mwa kundi.

Harry Kane alikiri kabla ya mechi kuwa kufunga dhidi ya Arsenal “humpa furaha zaidi” kuliko timu yoyote nyingine. Lakini licha ya kuwa na magoli 27 msimu huu, hakupata nafasi yoyote muhimu huku Bayern, ambao pia walikuwa wameshinda mechi zao nne za mwanzo na hawajapoteza katika mechi 21 msimu huu, wakipewa somo. Kufuzu hatua ya mtoano sasa ni suala la muda tu kwa Arsenal.

Ingawa ilikuwa usiku wa kusahaulika kwa Myles Lewis-Skelly, aliyepata nafasi adimu ya kuanza lakini akateswa sana na Karl wa miaka 17, na Leandro Trossard kulazimika kutoka majeruhi kabla ya mapumziko, kurejea kwa nahodha Martin Ødegaard kutoka jeraha la goti lililomweka nje kwa mwezi mzima kulimpa Arteta sababu nyingine ya kutabasamu.

Kadiri wiki zinavyosonga, Arsenal wanaonekana zaidi kama timu ya ushindi. Huenda kauli ya Arteta kabla ya mechi kwamba bado wako “ulimwengu tofauti” na Bayern – mabingwa wa Ulaya mara sita – ikabaki historia wakidumisha kiwango hiki.

Jumapili wanakutana na Chelsea, walio nafasi ya pili kwenye Premier League, mtihani mwingine wa uthabiti wao. Ila kwa sasa, wanapita kila jaribio.

Arteta alisema: “Tumekuwa thabiti sana kwenye mashindano haya. Lakini huu ni mwanzo tu. Enerjia kwenye uwanja, kile timu inapokea na kurudisha, ubora wa mpira tunaocheza – ni ajabu. Tunapaswa kudumisha hili.”

Bayern walianza kwa mpango wa kupunguza makelele ya mashabiki waliokuwa bado na hamasa kutoka ushindi mkubwa dhidi ya Tottenham. Walimiliki mpira kwa dakika 20 za mwanzo huku Arsenal wakipata nafasi mbili tu kutoka mipira iliyokufa – zote zikaamuliwa kuwa offside. Hakukuwa na bahati ya pili walipoifumania kona iliyomkuta Timber, aliyeruka juu na kumzidi Manuel Neuer.

Goli hilo liliwasha moto kwa Arsenal huku Declan Rice na Martin Zubimendi wakichukua udhibiti wa kiungo. Bayern walirudishwa nyuma, na pasi mbovu ya Kane ikashangiliwa kwa dharau.

Lakini baada ya Eberechi Eze kukosa kumalizia nafasi nzuri, Bayern walipiga shambulizi la ghafla. Mpira mrefu kutoka Joshua Kimmich ulimkuta Serge Gnabry, ambaye akampasia Karl kufunga kwa ustadi – kijana huyo ambaye tayari amekuwa mfungaji mdogo zaidi wa Bayern kwenye mashindano haya msimu huu na kupewa matumaini ya kuitwa kikosi cha Kombe la Dunia cha Ujerumani.

Arsenal walionekana kuchanganyikiwa, na wangeweza kuwa nyuma kama Josip Stanisic asingepiga nje baada ya Lewis-Skelly kupoteza mpira tena.

Matatizo yaliendelea wakati Trossard akitoka uwanjani akichechemea. Alibadilishwa na Madueke. Arteta alisema: “Alisema amehisi kitu, hatukutaka kuhatarisha hali ya mchezaji wake”

Kochi wa Bayern Vincent Kompany, aliyevaa kaptura pana na hoodie kama anaenda NK DISCO, Dodoma, alionekana kuwa na wasi wasi kila kona ilipopigwa dhidi yao. “Hilo ndilo Arsenal wamebobea kuliko mtu yeyote,” alisema.

Merino alipiga kichwa kingine kikapita karibu na lango, kabla Kompany kuonyeshwa kadi kwa kupinga uamuzi baada ya Dayot Upamecano kumwangusha Madueke. Shinikizo lilizidi.

Saka hakuwa mwepezi kuipokea fulsa kwa haraka wakati Neuer alipookoa shuti la Rice kwa mguu na kuacha lango wazi. Hatimaye kosa la Upamecano liliwarudisha mbele Arsenal – alipomkabidhi Rice mpira, Riccardo Calafiori, aliyekuwa ameingia muda mfupi, akampasia Madueke kufunga kirahisi.

Bayern walitafuta bao la kusawazisha, lakini mpira mrefu wa Eze ulimkuta Neuer akiwa mbali na lango, na Martinelli, kwa kugusa kwa paja, akamzidi ujanja kipa huyo na kufunga kirahisi – akithibitisha kwamba Arsenal wana maana kubwa msimu huu.

Report

Written by Israel Saria

I have been involved with sports in Tanzania as a Volleyball Coach for many years—and was a Tanzania Amateur Volleyball Association (TAVA) leader. I studied sports management at Leipzig University in Germany and understand the science behind sports. That led me to work as a football pundit, with the BBC ( Swahili service) in London. That experience and exposure took me to covering the 2010, World Cup in South Africa. This provided me with a great insight into international level football commentary and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics.I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany, Italy, Belgium, Ireland, France, Kenya etc, and visited almost all of the key football stadiums across United Kingdom, and Europe.

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Ninawapenda wachezaji wakipigana: David Moyes

Tanzania Sports

Arsenal yatoshana nguvu na Chelsea