*Waungana na Man U, Man City na Chelsea Ulaya
*Spurs kilio licha ya kushinda, wanaostaafu waaga
Arsenal wamewazidi nguvu mahasimu wao wa London Kaskazini, Tottenham Hotspurs na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kuwazidi pointi moja kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England (EPL).
Mzunguko wa 38 na wa mwisho EPL Jumapili hii ulikuwa na msisimko mkubwa na hisia za aina yake katika viwanja mbalimbali, macho mengi yakielekezwa St. James’ Park ambako Newcastle United waliwakaribisha Arsenal na White Hart Lane ambako Sunderland walikuwa wageni wa Spurs.
Tofauti na walivyocheza hovyo mechi zilizopita na kukandikwa mabao mengi, Newcastle wa Alan Pardew walibadilika na kucheza kwa nguvu kana kwamba walikuwa wakiwania ubingwa au kuepuka kushuka daraja.
Arsenal nao hawakuanza vyema mechi, pakiwa na ulegelege katika kuzuia mipira, kuisukuma mbele na pia kutafuta mabao, wakiwa kama vile walishafuzu kwa nafasi waliyokuwa wakiitafuta, kwa jinsi ambavyo hawakuonesha haraka.
Hata hivyo, kwa asilimia kubwa msimu huu, mabao na ushindi wa Arsenal vimekuwa vikija katika kipindi cha pili, na timu imekuwa na mabadiliko makubwa tangu mechi yao ya marudiano dhidi ya Bayern Munich nchini Ujerumani, ambako Arsenal walishinda 2-0 lakini wakatolewa Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwani Emirates walifungwa 3-1.
Arsene Wenger aliendelea kumsotesha benchi nahodha wake, Thomas Vermaelen aliyekuwa akijaza beki ya kati siku zilizopita, na kuwachezesha Laurent Koscielny na Per Mertesacker ambao wamekuwa wakifanya vyema tangu mechi hiyo ya Ujerumani.
Alikuwa Mfaransa Koscienly aliyewapatia Arsenal bao pekee katika dakika ya 52 Jumapili hii, lililotokea kuwa na thamani kubwa. Mfaransa huyo alifunga katika nafasi finyu, kutokana na mpira wa adhabu ndogo uliochongwa na Theo Walcott.
Thamani ya bao hilo ilidhihirika baada ya Spurs kuzinduka mbele ya Sunderland, pale wageni walipunguzwa mchezaji mmoja kwa kadi nyekundu, hivyo Gareth Bale kufunga bao dakika ya 90.
Arsenal walikuwa mbele ya Spurs kwa pointi moja, hivyo The Gunners walihitaji ushindi wa aina yoyote ile kujihakikishia nafasi, wakati Spurs walitakiwa washinde kisha waombe Arsenal ama watoke sare au wafungwe.
CHELSEA SAFI, FERGIE, CARRAGHER WAAGA RASMI
Chelsea wanaomaliza kuwa chini ya kocha wa muda, Mhispania Rafa Benitez nao pia walikuwa wakitafuta kujihakikishia nafasi, lakini wakiwa na unafuu kimazingira.
Walifanikiwa kuwafunga Everton mabao 2-1, wafungaji wakiwa Wahispania wenzake Benitez, Juan Mata mapema dakika ya saba na Fernando Torres dakika ya 76, wakati Everton walipata bao lao kupitia Steven Naismith dakika ya 14.
Ilikuwa mechi ya mwisho kwa kocha David Moyes, ambaye msimu ujao anahamia Old Trafford kuchukua nafasi ya Alex Ferguson, na alikuwa amedhamiria kumaliza kwa kishindo, lakini mechi ilikuwa ngumu dhidi ya Chelsea, hivyo hakuambulia.
Katika mechi nyingine, Liverpool waliwapiga QPR 1-0 Anfield, na baada ya mechi hiyo, mchezaji aliyecheza hapo kwa miaka 23, Jamie Carragher aliagwa na kukabidhiwa tuzo kedekede katika hafla ya kuvutia.
Sir Alex Ferguson alimaliza miaka yake Manchester United kwa sare ya ugenini iliyohusisha mabao 10 kati ya timu yake na West Bromwich Albion wakati Norwich waliwachakaza Manchester City mabao 3-2 dimbani Etihad.
Southampton walitoshana nguvu na Stoke kwa bao 1-1; Fulham wakapata ushindi adimu wa 3-1 dhidi ya Swansea, Reading wakalazwa na West Ham United 4-2 wakati Wigan waliokwishashuka daraja walikwenda sare ya 2-2 na Aston Villa.
TAZAMA MSIMAMO WA MWISHO WA MSIMU
Kukamilika kwa mzunguko huo wa mwisho wa EPL, kumewaacha Manchester United wakiwa kileleni kwa pointi 89 na mkiani wakiwamo QPR walioambulia jumla ya pointi 25 tu.
Man City wameshika nafasi ya pili kwa pointi 78, 11 nyuma ya jirani zao United wakati Chelsea wamekuwa wa tatu kwa pointi 75 na Arsenal wakafunga pazia la nne bora kwa pointi 73.
Spurs wameendelea na kawaida yao ya kumaliza nyuma ya Arsenal kama ilivyokuwa misimu yote kwa miaka 18 ambapo hawajapata kumaliza nne bora, wakiwa na pointi 72.
Everton wameishia nafasi ya sita kwa pointi 63; Liverpool pointi 61, West Brom 49, Norwich 44 na Fulham pointi 43.
Stoke City waliopata kutishiwa kushuka daraja mizunguko miwili iliyopita wamemaliza katika nafasi ya 13 kwa pointi 42, wakifuatiwa na Southampton, Aston Villa na Newcastle wote wenye pointi 41.
Sunderland wamemaliza katika nafasi ya 17, juu tu ya mstari wa kushuka daraja wakiwa na pointi 39, Wigan wana pointi 36, Reading 28 na QPR 25.
Comments
Loading…