Kibao kimegeuka;
Baada ya Arsenal kumaliza uteja kwa Chelsea kwenye Ngao ya Jamii kwa ushindi wa 1-0, wameurejelea uteja kwa nguvu ya mabao 2-0 waliyofungwa dimbani Stamford Bridge.
Mechi baina ya klabu mbili hizi ni kali na yenye kuvuta watu wengi ndani na nje ya nchi, lakini hii ya Jumamosi mchana ilikuwa na nguvu kubwa, hasa katika kuweka timu hizo mbili, kila moja kwa namna yake, kwenye mstari sahihi.
Chelsea waliingia uwanjani wakiwa na rekodi mbaya zaidi katika miaka zaidi ya 20 iliyopita katika Ligi Kuu ya England (EPL), lakini wakiliwazwa kwa ushindi mnono dhidi ya Macabi Tel Aviv kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL). Arsenal wakiwa vyema kwenye EPL lakini wakitoka kufungwa 2-1 na Dinamo Zagreb katika UCL.
Pengine kibao kilianza kugeuka kwa beki wa kati wa Arsenal, Gabriel Paulista kuzawadiwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza, baada ya kumpiga Diego Coasta, ambapo Arsenal wataona kwamba hawakutendewa haki kwa Costa kubaki uwanjani licha ya kufanya rafu kubwa dhidi ya Laurent Koscielny.
Iwe iwavyo, Arsenal wamepoteza mchezo wao wa kwanza wa ligi dhidi ya mahasimu wao wa London, Chelsea, kwa mabao ya beki Kurt Zouma na kiungo Eden Hazard, yaliyofanya safari ya kwanza kwa kipa Petr Cech Stamford Bridge kuwa chungu.
Lakini uzito wa hali yenyewe uliongezeka kwa kiungo mahiri wa Arsenal, Santi Cazorla naye kupewa kadi nyekundu dakika 11 kabla ya mpira kumalizika, ikiwa ni ya pili kwake kwenye mechi hiyo, baada ya kumchezea vibaya mchezaji wa zamani wa Arsenal, Cesc Fabregas.
Arsenal walidhani wangeweza kusawazisha dakika za mwisho, lakini ikawa kinyume kwa Hazard kutia bao dakika hizo, akisaidiwa na Loic Remy aliyeingia dakika ya 82 kuchukua nafasi ya Costa.
Ushindi huu ni muhimu kwa Jose Mourinho na vijana wake, kwani sasa wataondokana na tatizo walilokuwa nalo la kufanya vibaya, na huenda ndio mwanzo wa ndege yao kupaa, huku Arsenal ambao huchukua muda kuamka wakishalizwa, huenda wataanza kipindi kigumu.
Baada ya ushindi kwenye Ngao ya Jamii, Arsene Wenger angependa kuona akipata ushindi ambao ungekuja na pointi tatu muhimu kwa ajili ya kujiaminisha kwamba kweli The Gunners wapo kwenye ushindani wa kuwania ubingwa wa England.
Baada ya kutosajili mshambuliaji aliyehitajika sana, sasa Wenger atakabiliana na maswali mengi kutoka kwa wanahabari na washabiki, juu ya kisa cha kuacha mamilioni ya pauni benki badala ya kuendeleza timu.
Bado hajaeleza kisa cha kutomsajili kiungo aliyekuwa Southampton, Morgan Schneiderlin, ambaye amekuwa akimuwinda muda mrefu, akamwacha kwenda Manchester United huku akibaki na Francis Coquelin kama tegemeo lake kubwa kwenye kiungo cha ukabaji.
Matokeo haya sasa yanamwacha Mourinho akicheka hadi jino la mwisho, akijua kwamba udhia umeisha na kazi ya kuusaka ubingwa inaanza, huku Wenger akijua atamkosa Paulista na Cazorla kwenye mechi inayofuata ya EPL, pia atamkosa Olivier Giroud kwenye mechi ya UCL kwani naye alilambwa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Zagreb.
Hali hii ya kadi inatia shaka; hata kama wapo watakaosema waamuzi wanapendelea, ikichanganywa na rekodi ya Arsenal kuwa na majeruhi wengi karibu kila msimu, inaacha hofu kubwa ikiwa kweli wapo tayari sasa kuutafuta ubingwa wa England, au ni ushindi mdogo wa hapa na pale.