*Balotelli apata bao la kwanza EPL
Mzunguko wa 25 wa Ligi Kuu ya England umeanza kwa Arsenal kushinda, Mario Balotelli akifunga bao la kwanza la EPL na Queen Park Rangers (QPR) wakipata ushindi wa kwanza ugenini.
Arsenal waliotoka kuloa 2-1 kwa washindani wao wa London Kaskazini mwishoni mwa wiki jana, walipambana kuwafunga Leicester 2-1 kwa mabao ya Laurent Koscielny na Theo Walcott.
Ushindi huo umewapandisha Arsenal juu ya Manchester United lakini wamecheza mechi moja zaidi na Arsenal walipata pigo kwa kuumia tena kiungo wao, Aaron Ramsey.
Kwa mara nyingine, kiungo Mjerumani, Mesut Ozil aling’ara na ndiye aliyetengeneza mabao yote mawili, na kipa David Ospina alifanya makubwa, ikiwa ni pamoja na kuokoa mabao ya wazi, hasa kipindi cha pili. Bao la wageni lilifungwa na Andrej Kramaric aliyekosa mengine.
LIVERPOOL WAWAZIDI NGUVU SPURS
Liverpool wamefanikiwa kuwafunga Tottenham Hotspur 3-2 katika mechi ambayo mwana mtukutu Mario Balotelli alifunga bao lake la kwanza la EPL huku Harry Kane akiendeleza makali kwa Spurs akifunga bao la 23 la msimu.
Ushindi ulikuwa muhimu kwa Liverpool wanaopambana kuingia kwenye nafasi nne za juu. Balotelli aliingia badala ya Daniel Sturridge na ndiye aliyefunga bao la ushindi kutokana na majalo ya Adam Lallana dakika saba kabla ya mechi kumalizika.
Bao la kwanza la Liver lilifungwa na Lazar Markovic lakini likasawazishwa na Kane kabla ya nahodha wa Liver, Steven Gerrard kufunga kwa penati.
Mousa Dembele aliwasawazishia tena Spurs lakini hatimaye Balotelli aliyenunuliwa kwa pauni milioni 16 kutoka AC Milan alifunga bao la ushindi.
QPR USHINDI WA KWANZA UGENINI
QPR wasio na kocha walipata ushindi wa kwanza ugenini baada ya kuwacharaza Sunderland 2-0 na kuondoka kwenye eneo la kushuka daraja.
QPR ambao kocha wao, Harry Redknapp alijiuzulu hivi karibuni akidai anaenda kufanyiwa upasuaji wa goti, walipata mabao yao kupitia kwa Leroy Fer na Bobby Zamora, wakihitimisha mfululizo wa kufungwa katika mechi 11 mfululizo, unaodhaniwa ndio ulimsababishia Redknapp kujiuzulu.
Katika mechi nyingine, Hull waliwafunga Aston Villa 2-0 na kuwashusha hadi nafasi ya 18, eneo la kushuka daraja.
Kocha Paul Lambert amesema kwamba watajitahidi kufanya kila wawezalo kujirekebisha na kueleza anaelewa jinsi washabiki wao walivyo na hasira na mwenendo wa timu.
Comments
Loading…