in , ,

Arsenal bado kileleni

*Man U sasa waamka, Man City safi

*Leicester wachoka, Liver wapigwa

Mwaka umewaanzia vyema Arsenal, Manchester United, Manchester City,
West Ham, Norwich, Sunderland na West Bromwich Albion, kwa kupata
ushindi kwenye mechi za kwanza kabisa za 2016 kwenye Ligi Kuu ya
England (EPL).

Arsenal wameendeleza pengo dhidi ya waliokuwa wakipumuliana nao –
Leicester ambao baada ya kichapo sasa wametoka sare, baadhi ya
wachambuzi wakiona utabiri unaanza kutimia kwamba wakati wa mechi za
msimu wa sikukuu wangeanza kuchoka.

Pamoja na kwamba hawakucheza vyema, Arsenal walifanikiwa kupata pointi
zote tatu mbele ya Newcastle kwa bao 1-0 lililofungwa na beki wa kati,
Laurent Koscielny na kocha Arsene Wenger akawatetea vijana wake kwamba
uchovu wa mechi nyingi ulikaribia kuizidi miguu yao.

Ameeleza kufurahi kufanya vyema kwa asilimia 75 katika mechi hizo za
msimu wa sikukuu, wakipoteza moja tu dhidi ya Southampton na sasa
wamefikisha pointi 42. Leicester waliambulia pointi moja baada ya
kubanwa na waliopanda msimu huu – Bournemouth kwa suluhu, tena
Bournemouth wakicheza mtu mmoja pungufu kwa nusu saa ya mwisho.

Leicester walishindwa kutumia fursa hiyo kuamsha tena mwendo wa
ushindi, ambapo licha ya wapinzani wao kubaki 10, vijana wa Claudio
Ranieri walipata penati, lakini safari hii mpigaji wao hodari, Riyad
Mahrez hakuamini macho yake kuona ikiokolewa kwa mikono miwili ya
golikipa Artur Boruc aliyetokea kuwa shujaa wa mechi.

Baadhi ya wachezaji wa  Watford, wakionekana kutengwa na jamii ya "Watford"
Baadhi ya wachezaji wa Watford, wakionekana kutengwa na jamii ya “Watford”

Penati ilitolewa na mwamuzi Andre Marriner baada nahodha wa
Bournemouth, Simon Francis kumchezea vibaya mpachika mabao mwingine
matata aliyetoka kapa mara kadhaa sasa, Jamie Vardy.

Manachester United waliamka baada ya kukosa ushindi kwa zaidi ya mwezi
mmoja katika mechi nane, wakawafunga Swansea 2-1, lakini bado
hawatafurahia sana kwa sababu mwenendo wa Swansea nao ni mbaya.

Hata hivyo, ni ushindi aliouhitaji sana kocha Louis van Gaal
anayedaiwa alikuwa amepewa mechi mbili tu kuhakikisha wanarudia
kushinda, vinginevyo angefutwa kibarua, naye akakiri kwamba alikuwa
anahofia kuchukuliwa hatua hiyo.

Kadhalika ilikuwa faraja kwa nahodha, Wayne Rooney aliyemaliza ukame
wake wa kufunga, bao hilo likiwa ni la tatu tu katika msimu wote ambao
umeingia mzunguko wa pili. Bao la kwanza lilifungwa na Anthony Martial
wakati la Swansea lilifungwa na Gylfi Sigurdsson. Man U wamefikisha
pointi 33 wakipanda hadi nafasi ya tano.

Katika mechi nyingine, wakicheza ugenini, Manchester City walifanikiwa
kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Watford waliowatesa kwa kutangulia
kupata bao lakini wakaja kusawazisha dakika ya 82 kupitia kwa Yaya
Toure na dakika mbili baadaye Sergio Aguero akatia bao la ushindi.

Watford walitangulia kupata bao kutokana na kona ya Ben Watson
iliyotiwa kimiani kimamosa na beki wa City, Aleksandar Kolarov. City
wamekuwa na wakati mgumu wa kupata ushindi kwenye mechi za ugenini.

Liverpool waliangukia pua kwa wababe West Ham waliowachakaza pia
kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza, Jumamosi hii vijana wa Jurgen
Klopp wakikubali kichapo cha mabao 2-0.

Andy Carroll kwa mara nyingine alisomeka kwenye kibao akiifunga timu
yake ya zamani hukuWest Ham wakiwavuka Liverpool kwenye msimamo wa
ligi, wakishika nafasi ya sita huku Liverpool wakianguka hadi ya nane.

West Ham wana pointi 32 huku Liver wakibaki na zao 30. Hii ni mara ya
kwanza kwa Hammers kuwapiga Liver katika mechi zote mbili za msimu
kwenye EPL katika kipindi cha miaka 52. Christian Benteke alikuwa
hovyo kabisa kimchezo dimbani.

Michail Antonio alimzidi maarifa Nathaniel Clyne na kuipata majalo ya
mapema ya Enner Valencia na kufunga bao linaloshika rekodi ya kuwa la
kwanza katika EPL kwa mwaka huu mpya, nayo ilikuwa ni katika dakika ya
10 tu ya mchezo.

Carroll aliyeweka rekodi ya kuwa mchezaji ghali zaidi wa Liverpool
akinunuliwa kwa pauni milioni 35 mwaka 2011, hakuwaonea huruma The
Reds, akatumbukiza mpira kimiani baada ya majalo ya Mark Noble.

Katika mechi nyingine, Norwich waliwashangaza Southampton kwa
kuwatandika 1-0 lakini pia Sunderland wakawavuruga vibonde wenzao,
Aston Villa kwa kuwafunga 3-1, na West Brom wakawashinda wagumu
wenzao Stoke 2-1.

Ushindi wa Sunderland unawapa matumaini kwamba huenda vijana hao wa
Sam Allerdyce watafanikiwa kukiepuka kikombe cha kushuka daraja, kwnai
sasa wamefikisha pointi 15 na watakuwa wanajaribu kupata ushindi zaidi
kuwapiku Newcastle, Swansea na labda Chelsea.

Bado Sunderland wapo nafasi ya 19 wakati Villa wanaoonekana kukata
tama wakiwa mkiani na pointi zao 15. Newcastle wanazo 17 wakiwa wa
tatu kutoka chini, Swansea 19 na Chelsea kabla ya mchezo wa Jumapili
hii pointi 21. Chelsea wanacheza ugenini kwa Crystal Palace wakati
Everton wanawakaribisha Spurs Jumapili hii.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

ALICHOFANYA BECKHAM 2015: KINADHIHIRISHA UWEZO WA MICHEZO KUINUA JAMII

Tanzania Sports

Chelsea wawafyatua Palace