in , , ,

Antonio Conte Anamhitaji David Luiz Darajani

Antonio Conte tayari ameshathibitishwa kuwa meneja mpya wa Chelsea. Ataingia kazini mwezi Julai kukiandaa kikosi kwa ajili ya msimu ujao. Kocha huyo Muitaliano anafahamika kwa matumizi ya mfumo wa 3-5-2.

Walinzi, viungo na washambuliaji waliomo kwenye kikosi cha sasa cha Chelsea wana nafasi gani kwenye mfumo huo? Je analazimika kuingia sokoni kufanya manunuzi ya kutosha kusajili wachezaji wanaofaa zaidi kwenye mfumo huo?

Makala hii inajikita kuangalia namna mfumo wa 3-5-2 wa Antonio Conte unavyomhitaji mlinzi wa PSG ambaye Chelsea walimuuza takribani miaka miwili iliyopita kwa matajiri hao wa Ufaransa.

Mfumo wa 3-5-2 kama unavyojieleza unakuwa na walinzi watatu wa kati. Mfumo huu ulimpa mafanikio makubwa Conte akiwa na vilabu tofauti hasa Juventus kutoka 2011 mbaka 2014 akishinda taji la Ligi Kuu ya Italia kwenye misimu yote aliyokuwepo.

Ni Andrea Barzagli, Leonardo Bonucci na Giorgio Chiellini waliokuwa wakitumika kwenye karibu kila mchezo kwenye eneo la ulinzi. Leonardo Bonucci alikuwa akisimama katikati ya wenzie hao wawili.

Mlinzi anayesimama katikati ya wenzie wawili kwenye mfumo huu anahitaji kuwa na sio tu uwezo wa kucheza mipira ya juu bali pia anatakiwa kuwa na uwezo wa kupiga pasi na kuanzisha mashambulizi.

Hii ni kwa kuwa mara nyingi anahitaji kusogea mbele kidogo kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo inapotokea kiungo mkabaji anazidiwa na wapinzani. Ndivyo alivyokuwa akitumika Bonucci kwenye mfumo wa Conte.

Ni mlinzi gani wa kati aliyeko kwenye kikosi cha sasa cha Chelsea anayepaswa kucheza kwenye nafasi hii kwenye 3-5-2 ya Antonio Conte?

Majeruhi Kurt Zouma, John Terry, Matthew Miazga wana uwezo mkubwa wa mipira ya hewani lakini uwezo wao wa kupiga pasi na kuanzisha mashambulizi ni mdogo. Hivyo hakuna kati yao anayefaa kusimama katikati ya wenzie wawili kwenye 3-5-2.

Pengine Garry Cahill anapokuwa kwenye ubora wake unaotambulika anao uwezo wa kucheza mipira ya hewani na uwezo wa kutosha tu wa kupiga pasi na kuanzisha mashambulizi.

Ikiwa Conte hataona ulazima ama itashindikana kumrejesha nyota wa zamani wa Chelsea David Luiz anayeonekana kuweza kufaa mno kwenye nafasi hii basi hapana shaka Garry Cahill atakuwa chaguo sahihi.

Lakini kiuhalisia Chelsea itaweza kung’ara zaidi kwenye mfumo wa Antonio Conte ikiwa David Luiz ama mchezaji mwengine wa aina yake kama Javi Martinez wa Bayern atashuka darajani.

Luiz ni mmoja kati ya walinzi wenye uwezo mkubwa wa kuanzisha mashambulizi ya timu. Uwezo wake na mtindo wake wa uchezaji vinamfanya awe mmoja wa walinzi wanaofaa kwenye 3-5-2 ingawa hakuwahi kucheza kwenye mfumo huo.

Nafasi mbili nyingine za walinzi wa kati kwenye 3-5-2 zinawahitaji walinzi wepesi. Hii ni kwa kuwa mara nyingi walinzi hawa hujikuta wakipambana na mawinga wa timu pinzani ambao kwa kawaida huwa na uwezo mkubwa wa kuwasumbua walinzi.

Mlinzi mwenye wepesi wa kutosha na uwezo wa kubashiri maamuzi ya mpinzani ndiye anayehitajika kwenye nafasi hii. Ivanovic tuliyemzoea ana uwezo wa kucheza kwenye nafasi hii, yaani upande wa kulia wa Cahill ama Luiz endapo atasajiliwa.

Kwenye upande wa kushoto wa mlinzi wa kati Kurt Zouma ambaye kwa sasa ni majeruhi anaweza kucheza. Yeye pia anao wepesi wa kutosha na uwezo mkubwa wa kutabiri maamuzi ya mpinzani.

Hivyo kwenye sehemu ya walinzi watatu wa kati kwenye mfumo wa 3-5-2 wa Antonio Conte, nafikiri Kurt Zouma, Garry Cahill na Branislav Ivanovic watakuwa chaguo la kwanza iwapo hatasajiliwa mlinzi ama walinzi wengine wenye viwango.

Hata hivyo niseme tu Conte anamhitaji zaidi David Luiz. Kama bado angekuwepo kikosini angeweza kuwa mmoja kati ya wachezaji muhimu kwenye kikosi chake. Jitihada za kumrejesha darajani zinahitajika.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Rooney Hahitajiki Kwenye Kikosi cha England?!

Tanzania Sports

Barca, Bayern safi Ulaya