Msimu uliopita aliyekuwa kocha wa Yanga, Nabi alifungwa 2-1 katika uwanja uleule ambao Migeul Gamondi amekubali kipigo cha kwanza tangu achukue mikoba ya mtangulizi wake…
HISTORIA inajirudia. Ni maneno mawili ambayo yanadhihirishwa kwa ushahidi kile kilichotokea katika dimba la Highlands Estate wilayani Mbarali mkoani Mbeya baada ya mabingwa watetezi Yanga kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ihefu FC. Ulikuwa mchezo maradadi uliotawaliwa na kasi kubwa, ubabe na ufundi pamoja na mbinu za nje ya uwanja.
TANZANIASPORTS katika thamini yake, mchezo huo ulikuwa wa presha kubwa kwa timu zote mbili. Ihefu FC wakiwa nyumbani chini ya Kocha Zuberi Katwila walikuwa na kibarua cha kuhakikisha wanalinda rekodi yao dhidi ya Yanga. Wakati Ihefu wakilinda rekodi, wenzao Yanga walitaka kufuta machozi kwa kuichapa timu hiyo ili kusawazisha matokeo ya msimu uliopita ambapo wakiwa chini ya kocha Nasredine Nabi kwa bao 2-1.
Timu zote mbili zilitawaliwa na presha ya kulinda na kufuta rekodi. Hata hivyo kwa mara nyingine tena Ihefu Fc wamefanikiwa kuwathibitisha kuwa wao ni wababe wa Yanga katika uwanja wa Highland Estaste. Yanga wakifahamu ugumu wa mchezo dhidi ya Ihefu walitangulia kupata bao na kuwapa changamoto wenyeji wao.
Hata hivyo Ihefu walitulia na kusawazisha bao hilo na kufanya mchezo kuwa 1-1. Kila timu ikiwa inatafuta bao la ushindi, Yanga walikuwa wameliandama lango la Ihefu kwa muda mrefu, lakini dakika 90 zilionesha wenyeji wakiibuka na ushindi wa mabao mawili.
GAMONDI KAMA NABI
Msimu uliopita aliyekuwa kocha wa Yanga, Nabi alifungwa 1-0 katika uwanja uleule ambao Migeul Gamondi amekubali kipigo cha kwanza tangu achukue mikoba ya mtangulizi wake. Haikuwa rahisi kwa Ihefu kupata ushindi huo mbele ya timu iliyoanza kuogopeka barani Afrika na ambayo imefika fainali ya Kombe la Shirikisho pamoja na kuwa bingwa mtetezi wa Ligi Kuu.
PANGUA YA GAMONDI
Kocha Miguel Gamondi alikipanga kikosi chake katika mfumo wa 3-4-2-1 huku akiwapa nafasi wachezaji wengine kama Shomari Kibwana,Zawadi Mauya,Skudu Makudubela na Salum Abubakari. Kocha Miguel Gamondi alikipangua kikosi chake na kuanza mechi na wachezaji wengi wanaokaa benchi. Upangaji wa kikosi hicho umedhihirisha kuwa Yanga wana kikosi kipana. Aliingia kwenye mchezo bila mastaa wake Max Nzengeli, Azi Ki,Mudathir,Yao, Khalid Aucho
IHEFU WAKALI WABABE WA KUKAMIA
Ushindi wa mabao 2-1 unaweza kuelezewa kuwa muhimu kwa klabu ya Ihefu FC. Tathmini ya TANZANIASPORTS inaonesha kuwa Ihefu FC wanapocheza dhidi ya timu ya Yanga au Simba wanatumia mbinu ya kukamia mchezo. Mtindo huo unafanywa pia na klabu ya Singida Big Stars na Maungo FC ambako hamasa na uchezaji wao unategemea amsha amsha waliyonayo.
Kiufundi Ihefu walikuwa na mbinu ya kushambuliaji kwa kushtukiza na kasi. Mara kadhaa walifanya hivyo lakini hawakuwa makini katika uamlziaji. Baadhi ya mashambulizi yalipangwa vizuri kuanzia eneo lao, lakini walipovuka katikati ya dimba walikuwa wanapiga pasi ndefu kwenda kulia au kushoto, ambako wachezaji waliopigiwa pasi hizo wanakokota kuingia eneo la hatari.
Ihefu FC hawakutaka kuingia kwenye mtego wa Yanga wa kutandaza soka chini, badala yake wao ilikuwa kukimbizana kwa kutumia pembeni. Kazi ya Ihefu ilikuwa kuwakimbiza mabeki wa Yanga wa pembeni na mbinu yao ilikuwa inazaa matunda mara kwa mara kwa sababu safu ya ulinzi ilikuwa na mabeki watatu, huku wale wa pembeni wakitumika kama mawinga (Wing Backs).
YANGA ALIKOSEA?
TANZANIASPORTS inathibitisha hapakuwa na makosa upande wa Yanga ambayo yanaweza kusema ndiyo kiini cha kufungwa kwao. Kwanza Ihefu hawajawahi kupoteza mchezo katika dimba lao wanapocheza na Yanga ndani ya dakika 90. Mabingwa watetezi Yanga ahwajawahi kushinda katika dimba la Highlands Estate licha ya kucheza vizuri mechi zake. Ihefu FC kabala hawajapanda Ligi Kuu waliwahi kucheza mchezo wa Kombe la FA kwa njia ya matuta katika uwanja wa huo. Msimu uliopita akiwa na kikosi kamili walishindwa kuibuka na ushindi kwenye uwanja huo pia.
‘WAARABU WA LIGI KUU’
Mchezo huo ulitawaliwa na matukio mengi ya kustaajabisha huku wachezaji wa pande zote wakigombana mara kwa mara. Ihefu FC walikuwa wakiongoza kwa kujiangusha na kuhitaji huduma ya matibabu. Katika kipindi cha pili, matukio matano ya wachezaji wa Ihefu yalihusisha kuomba huduma ya kwanza, lakini mara walipofikishwa nje ya uwanja waliinuka kana kwamba hawajaumia. Ilikuwa mechi ambayo matukio ya ugomvi ni kawaida. TANZANIASPORTS inaweza kuthibitisha kuanzia dakika 70 ya mchezo, wachezaji wa Ihefu walikuwa wakitumia mbinu ya kujiangusha ili kupoza mashambulizi. Mbinu hiyo hutumiwa zaidi na timu za Misri,Morocco,Algeria,Tunisia hasa zile za Kiarabu kama njia ya kupunguza kasi ya wapinzani wao.
FUJO ZA MASHABIKI WA YANGA
Baadhi ya mashabiki wa Yanga walikuwepo upande wa kusini mwa uwanja wa Hinglands Estate walimtupia chupa za maji golikipa wa Ihefu FC ambaye alikuwa amelala chini mara baada ya kuokoa moja ya hatari langoni mwake. Mashabiki hao walichukizwa na tabia ya kipa huyo kupoteza muda, lakini pia waliudhika kwa matokeo kwani timu yao pendwa Yanga ilikuwa nyuma. Hali hiyo iliwalazimu baadhi ya wachezaji wa Yanga kwenda kuwaomba mashabiki hao waache kurusha chupa na vitu vingine ndani ya uwanja ili kuleta utulivu. Maombi ya wachezaji wa Yanga yalisikilizwa na mashabiki ambao walitulia.
VURUGU ZA MABENCHI YA UFUNDI
Benchi la ufundi la Yanga lilionekana kukerwa na uchezeshaji wa mwamuzi wa mchezo pamoja na tabia ya kujiangusha ya Ihefu FC. Mara kadhaa watu wa benchi la ufundi walikuwa wakizozana na waamuzi wa akiba pamoja na wale wa Ihefu. Vurugu hizo zilisababisha baadhi ya viongozi benchi la ufundi la Yanga kulimwa kadi za njano. Hali kadhalika Khalid Aucho alifanyiwa madhambi wakati akiokota mpira ili kurusha uwanjani baad aya kutolewa na mchezjai wa Ihefu. Aucho alisukumwa na kuanguka chini, lakini mwamuzi wa kati na akiba hawakuchukua hatua zozote za kutoa adhabu kwa waliomfanyia madhambi Aucho.,
ZUBERI KATWILA vs MIGUEL GAMONDI
Kocha wa Mamelodi Sundowns, Rulani Mokwena amewahi kusema, “ninaangalia mechi nyingi sana Ligi Kuu England nchi nyingine. Lakini Ligi ya England naitumia kuiba mbinu kisha nawafundisha wachezaji wangu. Naangalia namna Sofiane Amrabat anachezesha upande wa kushoto wakati yeye ni kiungo. Lakini Amrabat anapangwa kule kama kivuli tu, huwa anaingia ndani eneo la kiungo kila mara. Anakaa kama beki timu ikishambuliwa, lakini anakuwa kiungo timu inaposhambulia. Anakuwa mlinzi kupitia kiungo. Jones Stones naye beki wa kati lakini anacheza kiungo. Wapo wengi, wanaonekana hivyo naiba mbinu.”
Kauli ya kocha Rulani Mokwena inaweza kuturudishia mbinu za makocha wawili wa Ligi Kuu Tanzania, Zuberi Katwila na Cedric Kaze linapokuja suala la kucheza dhidi ya mpinzani mwenye uwezo mkubwa kuwazidi. Huenda Zuberi Katwila aliiba mbinu za kocha wa Namungo Cedric Kaze. Kwenye mchezo kati ya Namungo na Yanga, kocha Cedric Kaze alitumia mbinu ya kujaza viungo wengi katikati ya dimba ili kuvuruga mbinu za Yanga. Katika mchezo ule ingawa Namungo walifungwa dakika za mwisho, lakini mbinu hiyo iliwasaidia kupunguza mashambulizi ya Yanga.
Kama ilivyokuwa kwa Kaze, naye Zuberi Katwila alitumia mbinu ya kuvuruga mifumo ya mashambulizi ya Yanga kwa kujaza viungo wengi katikati ya dimba. Hicho ndicho kilichofanyika katika akili ya Katwila, ambayo iling’amuliwa baadaye na Miguel Gamondi akiwa amechelewa na ndiyo maana kipindi cha pili aliingiza majembe yake ya nguvu kukabiliana na ukuta wa Ihefu.
Comments
Loading…