in , ,

AFCON 2013 mwendo wa pole

*Ethiopia wawazuia Zambia, Nigeria kimya B’Faso

Michuano ya 29 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) imeingia siku ya tatu, huku bado msisimko ukiwa chini.

Siku ya kwanza ya mashindano hayo ilishuhudia suluhu, kwani mechi mbili hazikuzalisha hata bao moja, lakini siku ya pili ilizalisha mabao matano.

Jumatatu hii ilikuwa siku ya tatu, mechi za kundi C, ambapo mabingwa watetezi, Zambia walipepetana na Ethiopia wakati wakongwe Nigeria wakipimana ubavu na Burkina Faso.

Ikumbukwe kwamba, Ethiopia ilikuwapo katika michezo ya kwanza kabisa ya AFCON miaka 31 iliyopita, hivyo ugeni wake wa siku hizi unatokana na kupotea kwake hapa katikati.

Ni kwa sababu hiyo, na ile ya ubingwa wa Zambia ilivuta hisia za wengi kwamba Zambia wangeibuka na ushindi.

Kinyume na matarajio hayo, Ethiopia hata walipoadhibiwa na kubaki 10 uwanjani, walifanikiwa kukomboa bao la Zambia na kufanya mechi kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Wazambia wenyewe hawakuamini kwamba Adane Girma angetikisa nyavu zao dakika ile ya 65, lakini ndiyo maajabu ya mashindano.

Ulikuwa mchezo uliojaa matukio, hasa katika kipindi cha kwanza, Zambia ikiwapa shinikizo kali mabeki wa Ethiopia walioonekana kupwaya.

Saladin Seid alishindwa kufunga akiwa kwenye nafasi nzuri, kisha akakosa pia mkwaju wa penati. Ni baada ya hapo, golikipa wa Wahabeshi hao, Jemal Tassew alipewa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya Chisamba Lungu, umbali wa yadi 40 kutoka langoni.

Matarajio ya wengi yalianza kuonekana kweli, pale Collins Mbesuma alipowapatia Zambia bao la kuongoza mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Zambia walitarajia kuongeza bao kipindi cha pili, waliporejea wakiwa na mchezaji mmoja kuliko wapinzani wao, na pia bao moja juu, lakini ndoto zao zilizimwa kwa goli la Girma.

Katika mechi ya pili, Nigeria nao walipata pigo la mchezaji mmoja kutolewa kwa kadi nyekundu na hatimaye kuhitimisha mchezo kwa sare na Burkina Faso.

Nigeria walitangulia kupata bao katika dakika ya 23 kwa Emmanuel Emenike kuingiza wavuni mpira wa Ideye Brown, lakini Burkina Faso hawakuacha kuliandama lango, hadi mkwaju wa mwisho wa mchezo ulipotinga wavuni.

Nigeria walishaamini wamemaliza kazi kwa kuondoka na pointi tatu, lakini dakika ya nne ya nyongeza baada ya 90 za kawaida iliwagharimu.

Walichezea hovyo krosi fupi na dhaifu ya Jonathan Pitroipa, kwani iliwapita mabeki wawili wa Nigeria na kumfikia Alain Traore aliyeukwamisha mpira wavuni bila ajizi.

Katika mechi za kwanza za kundi A Jumamosi iliyopita, wenyeji Afrika Kusini walitoka suluhu na Cape Verde kama ilivyokuwa kwa mchezo kati ya Angola na Morocco.

Mechi za awali za kundi B zilichezwa Jumapili, ambapo Ghana ilimenyana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kutoka sare ya mabao 2-2.

Wafungaji wa Ghana walikuwa Emmanuel Agyemang-Badu na Kwadwo Asamoah waliowaacha Kongo nyuma kwa tofauti hiyo.

Hata hivyo, beki ya Ghana ilielekea kukatika kadiri mechi ilivyosonga mbele, ambapo Wakongomani walifanikiwa kupenya na kupachika mabao ya kusawazisha kupitia kwa Tresor Mputu na Dieumerci Mbokani.

Katika mechi ya pili Jumapili, mchezaji wa zamani wa Barcelona, ambaye ni nguzo ya Mali, Seydou Keita alifunga bao lililowazamisha Niger waliocheza kufa na kupona kutafuta heshima.

Jumanne hii kila nchi itakuwa imeshuka dimbani mara moja, kwani ni Ivory Coast ya Didier Drogba na Togo ya Emmanuel Adebayor, huku Tunisia na Algeria wakioneshana kazi.

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Chelsea wawararua wanyonge Arsenal

Toure, Gervinho waibeba Ivory Coast