Mmiliki wa klabu ya Chelsea, Roman Abramovich amevuruga mipango ya kocha Jose Mourinho ya kutaka kipa wao mkongwe, Petr Cech ahamie nje ya England.
Badala yake, bilionea huyo wa Urusi ameamua kwamba Cech anayetaka kubaki London, akiwa na nia ya kukubali ofa ya Arsenal, aruhusiwe kutua Emirates.
Mourinho alikuwa anataka Cech asiuzwe kwa wapinzani wao wanaowania nao ubingwa msimu ujao, bali aende klabu nyingine kama Paris Saint-Germain (PSG) waliokwishaonesha nia ya kutaka kumsajili.
Watu wa ndani wa Chelsea wanasema kwamba Abramovich ameingilia kati mpango huo na kusema Cech aruhusiwe kwenda anakotaka, ikiwa ni kumpa heshima kwa kazi kubwa aliyowafanyia kwa miaka 11.
Cech, 33, raia wa Jamhuri ya Czech alishaeleza nia yake ya kubaki London ambako familia yake imeshapazoea tangu 2004 aliposajiliwa kutoka Renes ya Ufaransa. Akiwa an Chelsea, Cech ameweka historia ya kuwa kwenye vikosi vilivyotwaa mataji yote katika miaka tofauti, ikiwamo ubingwa wa Ulaya.
Mourinho aliweka mtego baada ya kusikia Arsenal wanamtaka Cech, ambapo alitaka wabadilishane na ama Alex Oxlade-Chamberlain au Theo Walcott ambaye bado hajaingia mkataba mpya wakati ule wa zamani unaenda ukingoni.
Hata hivyo, Arsene Wenger, hasimu mkubwa wa Mourinho hasa uwanjani, alikataa dili hilo na kusema angependa wamnunue Cech kwa fedha taslimu, zinazokadiriwa kuwa pauni kati ya milioni 10 hadi 14.
Habari zinasema kwamba Cech atahamia Arsenal baada ya kupewa uhakika kwamba akiwa na kiwango kikubwa ndiye kipa namba moja. Mazungumzo juu ya ukamilishaji wa dili hilo yanaelezwa kuendelea vyema na pia Cech na Arsenal watamalizana ndani ya muda mfupi.
Wachezaji, viongozi pamoja na wafanyakazi wa Arsenal wanadaiwa kwamba wameshajiandaa kumpokea mkongwe huyo wakati wowote kuanzia sasa Emirates, akitafuta uzoefu mpya baada ya zaidi ya muongo mmoja Stamford Bridge.
Huyu ni mkongwe wa tatu kuwapa mgongo Chelsea baada ya Frank Lampard na Didier Drogba ambaye alirejea msimu uliopita na sasa ameaga, akitarajia kwenda Marekani aliko Lampard au kwingineko ili acheze walau msimu mmoja tena.
Kuingia kwa Cech Arsenal kutawaweka katika wakati mgumu makipa waliopo – yule aliyekuwa namba moja kwa muda mrefu, Wojciech Szczesny ambaye msimu uliomalizika katika ngwe ya pili alienguliwa na kipa wa kimataifa wa Colombia, David Ospina.
Licha ya kuchukua hatamu langoni, bado inaelekea kwamab Ospina ambaye alicheza vyema na kufungwa mabao machache, si ajabu akaondoka na inadaiwa tayari Fenerbahce wameonesha nia ya kumsajili kwa pauni milioni nne. Alisajiliwa na Arsenal kwa pauni milioni tatu kutoka Nice ya Ufaransa miezi 12 iliyopita.
Ospina naye anaendelea kuwika kwenye michuano ya Copa America, ambapo aliwazuia Brazil kufunga hata bao moja kwenye mechi za Kundi C.
Hata hivyo, kuna uwezekano wa makipa wote watatu kubaki Emirates na kupigania namba kisha Januari ikifika kila mmoja atakuwa amejua hatima yake. Szczesny anachukuliwa kama mchezaji aliyekuzwa kwenye soka ya England, hivyo anapewa nafasi zaidi kubaki, ili kukidhi matakwa ya Chama cha Soka (FA) cha England juu ya idadi ya wachezaji ‘wazawa’.
Kocha Wenger alikerwa na kitendo cha Szczesny, 25, kudakwa akivuta sigara kwenye chumba cha kubadilishia nguo Januari, ambapo pia alifungwa mabao kadhaa ya kizembe ndipo akaamua kumuweka benchi, akimchezesha kwenye mechi za Kombe la FA tu.
Hali ya makipa ina mambo mapya Arsenal, ambapo kocha wa makipa, Tony Roberts anaondoka kwenda kujiunga na Swansea, ambako msimu uliopita kipa na rafiki yake mkubwa, Lukasz Fabianski alihamia baada ya kuwasaidia Arsenal kutwaa Kombe la FA walilotetea tena msimu uliomalizika.
Kuondoka kwa Roberts, kunaelezwa, kutatoa nafasi kwa Cech kuingia na uzoefu wake mkubwa, lakini pia pamoja na uwezekano wa kuwasili na Christophe Lollichon kutoka Chelsea.
Cech na Lollichon hawajapata kutengana katika kipindi chote cha ukipa wake, tangu akiwa Rennes kisha Chelsea, na kuna kila dalili kwamba watafanya tena kazi pamoja Emirates. Roberts alipata kufanya kazi chini ya Kocha Mwandamizi wa Makipa wa Arsenal, Gerry Peyton, lakini Lollichon anadhaniwa kwamba ndiye atakuwa akimpa mazoezi zaidi Cech.
Chelsea wanafikiria kujaza pengo la Cech kwa kumsajili kipa wa QPR, Rob Green, 35, au Asmir Begovic wa Stoke kwa ajili ya kuwa chaguo la pili nyuma ya Mbelgiji Thibaut Courtois.