Aaron Ramsey: Kiungo wa zamani wa Wales na Arsenal atangaza kustaafu
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 ametangaza kumaliza rasmi kazi yake ya soka iliyoanza mwaka 2007. Katika kipindi hicho, alicheza mechi 551 kwa vilabu vya Arsenal, Cardiff City na Juventus, pamoja na kuichezea Wales mara 86 kimataifa.
Ramsey alikuwa hana klabu tangu alipoondoka Pumas UNAM msimu wa joto uliopita.
“Huu haukuwa uamuzi rahisi kufanya,” alisema katika taarifa aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii.
“Baada ya kufikiria kwa kina, nimeamua kustaafu soka. Imekuwa heshima kubwa kuvaa jezi ya Wales na kupitia nyakati nyingi za ajabu. Hili lisingewezekana bila mchango wa makocha wote niliowahi kufanya nao kazi na wafanyakazi wote walionisaidia kwa njia mbalimbali.
“Pili, asanteni kwa vilabu vyote nilivyobahatika kuvichezea. Asanteni kwa makocha na wafanyakazi wote walionisaidia kuishi ndoto yangu na kucheza katika kiwango cha juu zaidi.
“Na shukrani kubwa kwa mke wangu, watoto wangu na familia yangu yote. Bila nyinyi kuwa nami, yote haya yasingewezekana.”
Ramsey alikulia katika akademi ya Cardiff City na kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuichezea klabu hiyo akiwa na miaka 16 na siku 124 mwezi Aprili 2007.
Alijiunga na Arsenal mwaka 2008, ambapo alicheza mechi 369, akafunga mabao 64 na kutoa pasi za mabao 60, na kujijengea sifa kama mmoja wa viungo bora wa kizazi chake. Alishinda mataji sita na klabu hiyo, ikiwemo FA Cup tatu.
Baada ya miaka 11, alihamia Juventus mwaka 2019 kwa uhamisho wa bure, ambapo alishinda mataji matatu ikiwemo Serie A mwaka 2020.
Pia aliwahi kuchezea OGC Nice na Rangers kabla ya kujiunga na Pumas UNAM mwaka 2025.
Katika kipindi cha miaka 16 akiwa na timu ya taifa ya Wales, Ramsey alifunga mabao 21 na kutoa pasi 9 katika mechi 86. Alikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Wales kufika nusu fainali ya Euro 2016 na kufuzu Kombe la Dunia 2022.
Mechi yake ya mwisho kwa Wales ilikuwa Septemba 2024, na hajacheza mechi ya klabu tangu Septemba 2025.

