in , ,

MATEGEMEO NA MATUMAINI YA MPIRA TOKA SUNDERLAND KWETU TANZANIA YA KWELI?

“Hayakuanza leo. Maneno matupu hayatoshi. Tunachotaka ni utekelezaji na tumeshaanza kuyatimiza.” Dr Mukangara.

 

Wengi tumesikia ziara fupi mheshimiwa Rais Kikwete aliyoifanya klabu ya Sunderland AFC, kaskazini mashariki ya Uingereza takribani majuma mawili yaliyopita.
Ziara hiyo imejenga matumaini na maswali.
Matumaini kwamba moja ya matatizo makuu yanayohusu maendeleo ya mpira nchini yatatatuliwa. Tatizo gani? Tatizo la kuwekezea na kujenga vijana wenye vipaji toka ngazi za chini. Matumaini kwamba ufundi na ujuzi ambao wenzetu wanatuzidi utapikwa nchini Tanzania.
Matumaini kwamba mtoto mdogo au kijana mwenye kipaji akionekana mapema atakimbizwa chuo cha mpira chenye kila aina ya utaalamu utakaomjenga awe kama akina Didier Drogba (Ivory Coast), Lionel Messi, (Argentina) Andres Iniesta (Hispania) na Neymar da Silva Santos (Brazil).
Je matumaini haya ni njozi za mchana au la?
Matumaini haya yana misingi katika tabia ya Rais Kikwete mwenyewe aliyewaambia wanahabari waliomhoji baada ya ziara ya klabu ya Sunderland AFC kwamba zamani alikuwa mchezaji wa mpira wa kikapu. Kwamba anapenda mpira na anatambua Watanzania wanapenda mpira. Yalianzia toka Ellis Short tajiri mmiliki wa klabu ya Sunderland AFC alipoitembelea Tanzania na hatimaye kumwalika Rais wa nchi, Uingereza. Sunderland AFC itafundisha wachezaji chipukizi chuo kitakachojengwa Dar es Salaam na hatimaye nchi nzima. Chuo hicho kinatazamiwa kujengwa na Symbion Power, aliahidi Afisa wake mkuu, Paul Hinks.
Hayo ni baadhi ya matumaini ya msingi.
Lakini je, utekelezaji wake ukoje?

Kwanza tuangalie yalikoanzia. Tukumbushane mizizi ilipo. Klabu ya Sunderland haikukurupuka tu kuanza kusaidia Tanzania kuendeleza mpira kama alivyohimiza tajiri wa Kimarekani, Bw Ellis Short na mwenzie Paul Hinks.
Sunderland AFC si klabu kubwa kama Manchester United au Chelsea lakini ina mahusiano tayari Afrika. Mosi, mwezi Julai mwaka jana Sunderland AFC ilifanya mkataba wa kusaidiana na klabu bingwa ya Asante Kotoko toka Ghana. Makubaliano haya yaliahidi msaada wa kiufundi, mafunzo ya mpira, tiba na biashara.
Desturi hii ya ushirikiano na klabu za Kiafrika haukuanzia tu katika klabu ya Asante Kotoko. Unatokana na masuala ya kibiashara na mradi uitwao “Invest Africa” ambao lengo lake ni kuwekezea Afrika. Invest in Africa pia ina mahusiano na shirika la fadhila Nelson Mandela Foundation. Sasa hivi nchi zinazoendelea zinaliangalia bara letu kama uwanja muhimu wa kibiashara. Pili, kuna mtazamo unaowaona wachezaji wazuri wa kimataifa wanavyochanua toka Afrika akina Emmanuel Adebayo (Togo), Samuel Eto’o (Cameroon) na wachezaji wastaafu Nwankwo Kanu (Nigeria) na Jay Jay Okocha (Nigeria); hawa ni baadhi ya wachezaji walioipatia sifa Afrika, matajiri, walioshinda tuzo mbalimbali ikiwepo hadhi ya mataifa yao.
Hivyo mradi wa Invest Africa umechangia ushirikiano.
Margaret Byrne (aliyekuwepo wakati Rais Kikwete akiwa Sunderland) atakua sehemu ya ujumbe wa Sunderland AFC utakaotua Bongo mwezi Julai kuangalia shughuli hii ya ujenzi na mafunzo ya mpira itakavyokua. Alisema bibiye : “Mwaka jana Invest Afrika ilituhusisha na wahusika muhimu kama Symbion Power.”
Matembezi ya Bi Margaret nchini ni sehemu ya mpango mzima. Lakini la muhimu zaidi ni namna vyombo vyetu husika vitakavyofuatilia mpango huu. Je, Wizara husika itahusikaje?
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara alisema shughuli hii ya kuendeleza mpira na michezo Tanzania imefikia kilele baada ya hatua za muda mrefu. “Hayakuanza leo. Maneno matupu hayatoshi. Tunachotaka ni utekelezaji na tumeshaanza kuyatimiza.”
Ahadi ni deni.
Ikiwa Waziri ana moto na hisia za matumaini kama Rais na wawekezaji husika wa kigeni tutegemee mafanikio.
Kilichobakia sasa ni kurejea baada ya miezi michache na kutathimini yamefikia wapi. Na baada ya miaka michache, tutakapoanza kuwaona vijana wetu wakicheza vizuri, labda tutaanza kukubali kwamba kiu ya miaka 30 bila ushindi wowote wa michezo (hususani mpira) huenda imekidhiwa.

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Kaseja kiwango kimeshuka kweli?

WAWILI WACHAGULIWA KITUO CHA VIPAJI ASPIRE*