Msimu wa neema umeendelea kwa Jose Mourinho, baada ya Chelsea kuwafunga Sporting Lisbon 1-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), huku Manchester City wakibanwa.
Nemanja Matic alimpa furaha Mourinho aliyekuwa nyumbani kwao, baada ya kufunga bao kwa kichwa katika nusu ya kwanza ya mchezo na kutosha kuwaweka matajiri hao wa London kileleni mwa kundi lao la G.
Ilikuwa mechi muhimu kwa nahodha John Terry aliyecheza mchezo wake wa 100 katika UCL na bao la Matic lilitokana na mpira wa adhabu uliochongwa na kiungo wa zamani wa Arsenal na Barcelona, Cesc Fabregas.
Man City waliambulia pointi ya kwanza kwenye mashindano hayo, baada ya kwenda sare ya 1-1 na Roma katika dimba la Etihad. Nyota ilianza vyema kwa wenyeji pale Sergio Aguero alipofunga penati dakika ya nne tu ya mchezo.
Hata hivyo, Francesco Totti alisawazisha dakika 19 baadaye, ambapo Totti (38) ameweka rekodi ya kuwa mfungaji mwenye umri mkubwa zaidi kwenye mashindano ya Ulaya.
Man City wanatakiwa kupambana kiume kuvuka hatua ya makundi na kocha wao, Manuel Pellegrini alikuwa amesema mapema hawangependa kupoteza pointi, hasa wakiwa nyumbani, lakini mambo yalikuwa si rahisi.
Katika mechi nyingine, Paris Saint-Germain waliwafunga Barcelona 3-2, CSKA Moscow wakapoteza kwa Bayern Munich 0-1, Apoel Nic wakaenda sare ya 11 na Ajax, Schalke na NK Maribor wakatoshana nguvu 1-1, BATE Bor wakawafunga Athletic Bilbao 2-1 na Shakter Donetsk wakatoka sare ya 2-2 na FC Porto.
Comments
Loading…