PRESHA imeshuka. Hofu imetoweka. Huzuni imechukua nafasi kwa baadhi ya timu kwa dakika 90 tu zilizoamua hatima zao. Wikiendi iliyopita ilikuwa na dakika 90 ngumu kwa Top Four na zile zilizopigania kubaki Ligi Kuu. Zilikuwa dakika 90 za kukata shoka.
Timu 20 zilikuwa kwenye vita ya kubadilishana nafasi katika msimamo wa Ligi kuu England. Nafasi 4 za chini zilijaa presha, ingawa tayari vijana wa kishua Norwich walishaaga Ligi Kuu.
Nafasi nne za juu zilikuwa na presha pia, ingawa nafasi mbili zilishapata wenyewe. Wenye bahati wakapenya. Wenye nuksi wameshuka. Nini kilichojiri ndani ya dakika 90 za michezo ya wikiendi iliyopita? Makala haya yanaeleze jinsi dakika 90 zilivyokuwa za kibabe.
WABABE SITA EPL
Wote tunajua bingwa wa Ligi Kuu, lakini vichwa viliwauma makocha na wachezaji ndani ya dakika 90 za kumaliza Ligi. Kati ya timu 20, ni Liverpool, Manchester City na Norwich peke yao walizijua nafasi zao.
Liverpool wamekuwa namba moja. Manchester City wamekuwa namba mbili, halafu Norwich ndiyo hivyo tena, wameshuka daraja. Timu zingine zikaanza kugombania nafasi ya kuungana na Liverpool na Man City ili kushirika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Dakika 90 za michezo ya wikiendi zinaonesha vita ya wababe imewaibua Manchester United na Chelsea ambao wameungana na Liverpool na Man City katika nafasi nne za juu na kujihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Leicester City na Tottenham Hotspurs wamejihakikishia kushiriki Europa League msimu ujao. Man United waliibuka na ushindi 2-0 ugenini dhi ya Leicester City na kuwaondoa vijana wa Brendan Rodgers kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Chelsea kama wangepoteza mchezo wao dhidi ya Wolverhampton Wanderers ingekuwa balaa, lakini ushindi wa mabao 2-0 uliwafikisha kwenye pointi 63 sawa na Man United kwa tofauti ya mabao.
KITANZI CHA KUSHUKA DARAJA
Dakika 90 zingine zilikuwa za kujikoa kushuka daraja wikiendi iliyoisha. Ilikuwa mara ya kwanza kushuhudia mpambano mkali wa kubaki Ligi Kuu msimu ujao.
Hakuna timu iliyokuwa na uhakika hadi siku ya mwisho wa Ligi Kuu. Hii ni rekodi ya aina yake, ambayo ilishuhudiwa miaka sita iliyopita yaani msimu 2014-2015.
Katika msimu wa 2017-18 Swansea City ilihitaji ushindi wa mabao 10 ili kibaki Ligi Kuu, lakini lilikuwa jambo lisilowezekana kiuhalisia.
Dakika 90 za wikiendi iliyopita timu tatu zilitaka kujikoa kutoshuka daraja; Astona Villa, Watford na Bounemouth. Aston Villa walikuwa ugenini kupepetana na West Ham, wakati Watford walikuwa wageni wa Arsenal.
Villa na Watford zilihitaji sare ya aina yoyote ili kubaki Ligi Kuu, wakati Bournemouth ilihitaji pointi tatu ili kujikoa na kitanzi cha kushuka daraja mbele ya Everton na kuombea wapinzani wao wafungwa.
Haikuwa hivyo, Aston Villa walitoka sare ya 1-1 na West Ham, wakati Watford akacharazwa mabao 3-2 na kumaliza Ligi wakiwa nafasi ya 19. Bournemouth waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Everton, lakini haikusaidia kitu.
BINGWA WA FA
Dakika 90 zingine zinatarajiwa kuchezwa wiki jumamosi ijayo, kati ya Arsenal na Chelsea. Ikiwa Arsenal watashinda ubingwa wa FA nao watakuwa na nafasi ya kushiriki Europa League msimu ujao.
Taji la FA litawahakikishia Arsenal kuingia hatua ya makundi ya Europa League pamoja na timu iliyoshika nafasi ya tano na sita katika msimamo wa Ligi Kuu England, ambazo ni Leicester City na Tottenham Hotspurs (itakayoanza raundi ya kwanza).
Kama Chelsea watatwaa ubingwa wa FA, ambao tayari wamefuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya,nafasi ya kushiriki Europa League itakwenda kwa timu iliyoshika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu.
Kwa muktadha huo timu za nafasi ya tano na sita zinakwenda hatua ya makundi wakati timu iliyoshika nafasi ya saba inaingia Europa League kuanzia raundi za mchujo.
DAKIKA 90 ZA KUKOSA FEDHA
Kila timu inapewa zawadi ya fedha kulingana na nafasi yao wanayomaliza Ligi Kuu na tofauti yake ni pauni milioni 2 kwa nafasi.
Liverpool na Manchester City, zilishajihakikishia mgawo wao, tofauti na zingine ambazo nafasi zao zimebadilika kutoka chini kwenda juu au kutoka juu kwenda chini.
Kwahiyo kwa timu kushuka chini kuna kiasi fedha wamekikosa, naz ingine kupanda juu wamejipatia fedha nyingi zaidi kuliko wangekwua chini.
WASHAMBULIAJI ‘TOP FOUR’ WAMEFELI
Dakika 90 za wikiendi hazikuleta mabadiliko yoyote katika nafasi ya mfungaji bora wa msimu huu. Jamie Vardy wa Leicester City ametwaa tuzo ya mfungaji bora akiwa ametumbikiza wavuni mabao 23.
Huyu anakuwa mfungaji bora mwenye umri mkubwa, akiwa na miaka 33. Dann Ings ameshika nafasi ya pili. Nafasi ya tatu imekwenda kwa Pierre Emerick Aubameyang mwenye mabao 20. Wanafuatia Mohammed Salah (19), Raheem Sterling (19).
Kwenye msimamo wa Ligi hakuna timu iliyotoa mfungaji bora. Liverpool, Man City, Man United na Chelsea washambuliaji wao hawajafua dafu. Jamie Vardy anatoka timu iliyoshika nafasi ya tano, Leicester City.
Hii ni sawa na msimu wa 1999-2000 ambao Kevin Philips aliibuka mfungaji bora lakini timu yake haikuwa kwenye Top Four. Hii ina maana washambuliaji wa mabingwa wa Ligi msimu huu wamefeli.
Mshambuliaji wa mwisho kutwaa tuzo ya ufungaji bora huku timu yake ikiwa bingwa wa Ligi ni Robin van Persie miaka 7 iliyopita alipokuwa akiichezea Man United.
MIKONO YA KIBRAZIL
Wabrazil Ederson Moraes na Allison Becker wamekuwa wanashindana wenyewe kwa wenyewe. Msimu huu tuzo ya kipa bora imeenda kwa Ederson Moraes wa Man City.
Ederson amekuwa kipa wa kwanza wa Man City kutwaa tuzo hiyo tangu Joe Hart aliposhinda katika msimu wa 2014-15. Allison Becker alikuwa mpinzani wa karibu wa Edrrson, pamoja na mlinda mlango wa Burnley, Nick Pope.
Comments
Loading…