Mbao FC iliwahi kuwa na mshambuliaji hatari sana aliyewahi kuitwa Habib Kiyombo, Habib Kiyombo ambaye kuna nyakati tuliwahi kusikia kuwa yupo Mamelodi Sundown ya nchini Afrika Kusini.
Macho yangu hayajawahi kumuona akiwa na kwenye kikosi cha miamba hiyo mikubwa ya nchini Afrika Kusini. Hata muda huu ukiniuliza ni wapi alipo Habib Kiyombo swali hili nitalirudisha kwako tena kwa kukuuliza yuko wapi Habib Kiyombo?
Mbao FC ya jijini Mwanza iliwahi kuwa na Said Said Jr. Moja ya washambuliaji wakubwa sana, Said Said Jr kwenye story yake kuna swali ambalo linafanana na swali la Habib Kiyombo, yuko wapi Said Said Jr?
Washambuliaji wawili mahiri ambao Watanzania wengi tunakosa majibu ya swali sahihi na kubwa la wapi walipo mpaka sasa hivi kwa sababu tuliwaona ni msaada mkubwa kwenye timu yetu ya taifa.
Wakati ukiwa bado unajiuliza kuhusu mahali walipo Said Said Jr na Habib Kiyombo akili yako unatakiwa uipe mtihani mkubwa wa kujiuliza ni wapi alipo Wazir Jr.
Najua swali hili litakuwa na jibu jepesi kuwa Wazir Jr yupo Yanga SC. Wazir Jr hayupo Yanga SC. Watanzania tunatakiwa kuhoji kwa nguvu zote ili tupate kujua ni wapi alipo Wazir Jr kwa sababu ni moja ya hazina kubwa katika timu yetu ya Taifa.
Wazir Jr ambaye alimaliza ligi kuu ya Tanzania bara msimu jana akiwa na zaidi ya magoli 10 na akipigana kwa kiasi kikubwa kuisaidia Mbao FC ibaki kwenye ligi kuu ingawa haikuwezekana, Wazir Jr huyo hayupo tena Yanga SC.
Wazir Jr yule ambaye alikuwa anafunga sana hayupo tena Yanga SC kwa sababu mpaka sasa ameifungia Yanga SC goli moja tu kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC FC kwenye uwanja wa CCM Kirumba.
Uwanja ambao yeye anaamini ndiye mfalme mkubwa wa uwanja huo. Mfalme huyu kwenye msimu jana wa ligi kuu Tanzania bara alikuwa na mikimbio mizuri sana akiwa na mpira.
Habari mbaya ya kusikitisha ni kuwa mpaka sasa hivi mikimbio hii ya Wazir Jr haipo kwenye ligi kuu Tanzania bara. Nikuulize wewe unayesoma hapa mikimbio hiyo unaiona akiifanya akiwa na jezi ya Yanga SC?
Bila shaka jibu ni hapana, kama jibu ni hapana tunatakiwa kujiuliza tena hili swali, yuko wapi Wazir Jr? Jangwani pamekuwa na ukame mkubwa kwake.
Hana maji pamoja na chakula cha kutosha akiwa jangwani. Kuna hatari ya yeye kufa kwa sababu ya kukosa chakula na maji akiwa jangwani.
Wazir Jr anahitaji sana chakula na maji hapo jangwani. Anahitaji chakula na maji ili akili yake itulie na irudi kwenye kucheza mpira. Akili yake ifikirie tena namna ya kuziadhibu nyavu za wapinzani.
Kwa sasa Yanga SC haina washambuliaji bora ambao wanaweza kumweka benchi Wazir Jr. Kwenye jitihada za Wazir Jr ni ngumu kukaa benchi mbele ya Michael Sarpong.
Yupo wapi Wazir Jr kipindi hiki ambacho Michael Sarpong hafungi? Au ugeni wa jiji la Dar es Salaam unamfunika Wazir Jr? Bado analitembelea jiji la Dar es Salaam na akimaliza ndiyo atawekeza nguvu kwenye kikosi cha Yanga SC?
Tunamtafuta Wazir Jr baada ya kumpata tumuoneshe video za michezo ya msimu jana alipokuwa Mbao FC na baada ya kumaliza kumuonesha tumuulize swali moja upo wapi Wazir Jr?