*Simba, Azam Ushindi Mwembamba
Michezo kadhaa ya mashindano ya VPL imepigwa hii leo kwenye viwanja tofauti. Simba, Yanga na Azam zimepata matokeo ya ushindi kwenye michezo yao,
Yanga wakiwafunga JKT Ruvu 4-0 ndani ya dimba la Uwanja wa Taifa huku Simba wakiibuka na ushindi mwembamba dhidi ya Kagera Sugar huko jijini Shinyanga kwenye dimba la Kambarage. Azam wameshinda 1-0 dhidi ya Mwadui FC.
Simon Msuva ndiye aliyeng’ara zaidi pale Yanga ilipowazamisha JKT akifunga mabao mawili huku Donald Ngoma na Gaba wakipachika mengine.
Mabingwa hao watetezi waliuanza mchezo huo kwa mashambulizi ya hatari kwenye dakika za awali yaliyowapelekea kupata bao la mapema mnamo dakika ya 11.
Ni Simon Msuva aliyefunga bao hilo la kwanza kwa ustadi kabisa akiunyanyua mpira juu ya golikipa na kuuzamisha wavuni bila kipingamizi. Kufuatia bao hilo timu hizo zilishambuliana kwa zamu huku Yanga wakifanya mashambulizi makali zaidi lakini golikipa Dihile alisimama imara langoni.
Dakika mbili kabla ya mchezo kwenda mapumziko Gaba akapokea pasi safi kutoka kwa Simon Msuva na kupiga mpira uliompita Dihile ambaye safari hii hakuwa na la kufanya, hivyo mpira huo ukatinga wavuni na kuwaweka Yanga mbele kwa mabao mawili.
Dakika sita baada ya kuanza kwa kipindi cha pili Msuva akapata nafasi ya kuiongezea Yanga bao la tatu baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Nonga lakini winga huyo akateleza na kushindwa kufanya lolote.
Dakika ya 63 ikamshuhudia mshambuliaji Donald Ngoma akiiandikia Yanga bao la tatu baada ya kuruka juu akiwa huru na kufunga kwa kichwa bao rahisi.
Bao hilo la Donald Ngoma liliwahakikishia Yanga ushindi hivyo wakaonekana kuridhika na ushindi huo kiasi cha kupunguza kasi ya mshambulizi huku JKT wakionekana kukata tamaa.
Dakika 90 za FIFA zikamalizika matokeo yakiwa 3-0. Hata hivyo ndani ya dakika za mwamuzi Simon Msuva aliyekuwa moto wa kuotea mbali kwenye mchezo wa leo akaipachikia Yanga bao la akimalizia kazi nzuri ya Deus Kaseke.
Huko Shinyanga Simba SC walishinda 1-0 dhidi ya Kagera Sugar. Ni mshambuliaji hatari kijana Ibrahim Ajib aliyefunga bao pekee la mchezo mnamo dakika ya 45.
Mshambuliaji huyo alikuwa sehemu kubwa ya mashambulizi ya Simba hasa kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo akishiriki kwenye mashambulizi kadhaa ya hatari kwenye dakika ya 5, ya 9 na ya 24 ambayo hata hivyo hayakukuzaa bao lolote.
Hta hivyo Ajib alikosa penati ambayo ingewaongezea Simba bao la pili dakika saba kabla ya mchezo kumalizika.
Azam FC nao wakiwa nyumbani wamepata ushindi wa 1-0 dhidi ya Mwadui FC. Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na mshambuliaji Kipre Tcheche.
Matokeo ya michezo hiyo mitatu yanawafanya Yanga waendelee kuwa kileleni mwa msimamo wakiwa na alama 43. Simba wanabaki kwenye nafasi ya pili wakiwa na alama 42. Azam wanabaki kwenye nafasi yao ya tatu wakiwa na alama 42 pia na michezo miwili mkononi.