Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wameendelea kuukaribia ubingwa wa mashindano hayo baada ya jioni hii kuwalaza Toto Africans 2-1 ndani ya dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza.
Yanga waliuanza huo mchezo kwa mashambulizi makali kwenye kipindi cha kwanza wakishindwa kuzitumia nafasi kadhaa za kufunga mabao kutokana na umahiri wa mlinda mlango wa Toto Mussa Mohammed.
Mnamo dakika ya 39 Toto Africans wakaandika bao la kuongoza kupitia kwa William Kimanzi akiunganisha kwa kichwa safi kona ya Abdallah Seseme. Bao hilo lilidumu mbaka pale mwamuzi alipopuliza kipenga cha mapumziko.
Yanga walikianza kipindi cha pili wakitafuta nafasi ya kurejesha bao kwa kasi. Ndani ya dakika tano za kipindi cha pili Amissi Tambwe akafanikiwa kuwarejesha Yanga mchezoni baada ya kuchomoa bao kwa kichwa akiunganisha krosi ya Donald Ngoma. Bao hilo ni la 19 kwa mshambuliaji huyo msimu huu.
Bao hilo liliwapa morali vinara hao wa Ligi Kuu Bara na wakaendelea kutafuta bao la ushindi lakini Toto Africans wakasimama vyema kulinda bao lao. Hata hivyo ndani ya dakika ya 77 Juma Abdul akawapatia Yanga bao la kuongoza akimalizia mpira uliochezwa na golikipa akiokoa shuti la Simon Msuva.
Mwalimu Hans van der Pluijm akafanya mabadiliko ya wachezaji watatu kwa pamoja kufuatia bao hilo.
Akawatoa Deus Kaseke, Amissi Tambwe na Haruna Niyonzima na kuwaingiza Matheo Anthony, Thabani Kamusoko na Malimi Busungu kuchukua nafasi zao.
Jitihada za vijana wa mwalimu John Tegete kusawazisha bao hilo hazikuweza kufanikiwa na hivyo Yanga wakafanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu na kuwa na jumla ya alama 65 wakiendelea kujiimarisha kileleni baada ya kucheza mchezo wao wa 26.
Mchezo wa kesho kati ya Azam walio kwenye nafasi ya pili na alama 58 dhidi ya Simba walio kwenye nafasi ya tatu na alama 57 utaamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakuwa na nafasi ya kuendelea kuwafukuza Yanga kwenye mbio za ubingwa.