Ni timu mbili zenye miundo tofauti. Ni timu mbili zinazocheza kwa staili ya aina yake. Ni timu mbili zenye presha kubwa katika soka la Bongo. Ni timu mbili ambazo zinajaribu kuondokana na ufukara wa kiuchumi kwa kukaribisha wawekezaji na kuunda taasisi imara. Ni timu mbili zenye mastaa kibao kutoka nje ya nchi. Ni timu mbili ambazo ni kioo cha soka la Bongo. Hizo ndizo sifa za Simba na Yanga zilizokutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao unafungua pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa bao pekee la Fiston Mayele aliyepokea pasi kutoka kwa Farid Mussa.
Katika mchezo huo Simba walikuwa walewale, wakicheza pasi fupi fupi, kuandaa mashambulizi kutoka nyuma, kwenda langoni mwa Yanga. Kwa Yanga walikuwa mahiri katika maeneo ya winga na mabeki wa pembeni. Beki wa kulia Djuma Shaban na winga wa kulia Jesus Moloko walimsumbua kiasi cha kutosha beki wa kushoto wa Simba Mohammed Hussein, huku SHomari Kapombe akikumbana na shughuli pevu ya kumzuia winga wa kushoto Farid Mussa na beki wake Kibwana Shomari.
Tofauti za timu hizo ni kwamba Simba wanaendeleza falsafa yao ya kuonesha wanachokicheza, lakini Yanga bado hawaonekani kucheza kitimu kama walivyo wapinzani wao. Yanga waliweka ukuta mgumu kuanzia safu ya kiungo ambako walikuwepo Khalid Aucho na Yannick Bangala, kisha kiungo mshambuliaji akakaa Feisal Salum.
YANGA YA USHINDI
Wakati pekee ambao Yanga ilikuwa imecheza kwa utulivu ni kipindi cha pili baada ya kuingia Yacouba Sogne. Kuna pasi 12 mfululizo zilipigwa bila Simba kugusa. Lakini wakati huo tayari Yanga walikuwa wameshapata bao.
Yacoube ni mchezaji mzuri kwa vile anaweza kukaa na mpira, kusaidia ulinzi na anapenda kushambulia akitokea pembeni kushoto. Ujuzi wake katika kushambulia na kuweka mpira katika himaya yake ni sawa na kile anachokifanya Farid Mussa au Jesus Moloko.
Uwezo wa Yanga kucheza kwa utulivu kama Simba bado haujafika. Wachezaji wake wanaonekana wanatafuta namna ya kufahamiana vizuri. Lakini wana silaha kali mno za kuifunga timu yoyote. Silaha yao ya kwanza ni Feisal Salum, hapo ndipo Yanga ya ushindi inaposukwa.
Kama sio umahiri wa Taddeo Lwanga kutumwa kazi ya kumdhibiti Fei Toto nadhani Simba wangepata shida kubwa mno katika mchezo huo. Matokeo ya kazi aliyotumwa Lwanga yalionekana kwa faulo alizochezewa Fei Toto tangu mwanzo hadi pale mwamuzi Ramadhani Kayoko alipomlima kadi nyekundu Lwanga ikiwa ni hitimisho lake la kazi chafu alizopewa na Didie Gomes.
Silaha ya pili ya Yanga ya ushindi ni mawinga wake wa kulia na kushoto. Nafasi hizo ndizo zilikuwa zikisisimua kuona shughuli ilivyokuwa ikifanyika kiasi kwmaba benchi la ufundi la Simba likamtoa Mohammed Hussein. Mo Hussein ni bonge la beki, ameimarisha uwezo na uzoefu wake una pa faida kubwa.
Silaha ya tatu ni uwezo wa golikipa Djigui Diarra ambaye anacheza kama makipa wa kisasa. Djigui anaweza mkubwa kupiga pasi kuwafikia walengwa ili kuanzisha mashambulizi, anacheza kama sentahafu ikiwemo kuosha hatari langoni mwake.
Silaha ya nne ni eneo la kiugo wakabaji; Yannick Bangala na Khalid Aucho. Wakati Bangala anao uwezo wa kupanda mbele kupiga mashuti lango la adui, Aucho anabaki nyuma kulinda ukuta wake. Mgawanyo wa majukumu hayo unawapa nafasi nzuri Yanga ya kujigawa kimajukumu. Na endapo timu hii ikicheza kwa utulivu na mwelekeo wa uhakika basi itakuwa moto wa kuotea mbali.
Eneo la mwisho ni safu ya ushambuliaji, ambako Fiston Mayele hakuhitaji nafasi nyingi ili kufunga mabao. Nafasi aliyopata na uamuzi wa haraka aliofanya ulimpatia bao lililowapa uongozi Yanga. Hii ni aina ya washambuliaji wanaohitaji nafasi chache sana, kisha wanatimiza majukumu yao. lakini mabailiko yao ya kumwingiza Herieter Makambo ni ujumbe kuwa wanayo machaguo mazuri katika eneo hilo.
Udhaifu pekee uliojitokeza ni eneo la ulinzi wa kati, ambalo walimu wana kazi ya kufanya kuwaambia namna ya kuwazuia wapinzani mapema kabla hawajafika langoni mwao. Kazi ya namna hiyo pale Yanga hufanywa na Abdalah Shaibu, lakini kutokana na ushindani uliopo Dickson Job na Bakari Mwamnyeto wanatakiwa kukumbusha kuzuia hatari mapema kabla haiatokea.
Vilevile Yanga wanaonekana kukosa beki wa kushoto hali ambayo walimu wanamtumia Kibwana Shomari ambaye kimsingi ni beki wa kulia. Kwa msimu mzima sio rahisi kutegemea beki wa bandia ingawa anacheza vizuri, hivyo wanapaswa kuepuka hatari hiyo. Pia wanapaswa kumwandaa Ramadhan Kabwili na Eric Johora wakati wowote kwa kuwapanga baadhi ya mechi ili kumpumzisha Djigui na kuimarisha viwango vya eneo hilo.
SIMBA YA BURUDANI
Simba wanacheza kwa kujiamini. Wanacheza kama mabingwa. Wanacheza kwa uzoefu. Maingizo mapya yanaonesha kuwa yanafaa kuziba mapengo ya Luis Miquissone na Cletous Chama. Ni Simba ileile inayocheza soka la burudani kuanzia kwa golikipa wake anayejiamini mno Aishi Manula hadi safu ya ushambuliaji.
Ni kweli Chris Mugalu alikosa nafasi kadhaa, lakini huyu ni mshambuliajihatari ambaye anaweza kuimaliza timu pinzani wakati wowote. Simba wanapanga mashambulizi kutokea
nyuma, wanajikusanya, wanawajibika pamoja kuanzia katikati kwenda kushoto,kulia,pembeni na safu ya ushambuliaji.
Uzuri ni kwamba Sadio Kanoute ameonesha thamani yake angalau kwa muda mfupi. Kanoute anajua namna ya kusukuma timu iende mbele,anailinda sambamba na Taddeo Lwanga. Kimsingi Taddeo Lwanga alifanya kazi chafu zote muhimu na kumfanya Kanoute awe anaelekea lango la adui zaidi kuliko kubaki pembeni yake.
Kanoute ni mwepesi,ana mshuti,ana muono mzuri, lakini anahitaji muda tu kuchezeshwa kwenye mfumo wa Simba iwe 4-2-3-1 au 3-2-4-1 na mwingine achaguao mwalimu wao. Hii ni Simba ileile ya burudani,haijapoteza mwelekeo wake bali wanaonekana kujua wanafanya nini. Kilichobaki ni mwalimu kuwafanya watekeleze majukumu yao kwa ufasaha. Kinachoweza kuaangusha ni pale watakaposhindwa kupachika mabao. Timu isipopachika mabao inajiweka katika shinikizo kutokana na kosa kosa hizo ikiwemo kupungua kujiamini mchezoni.
MBABE WA NGAO YA JAMII
Simba imeshindwa kuweka rekodi mpya ya kutwaa taji hilo mara tano mfululizo, baada ya kulichukua tangu mwaka 2017 hadi 2020. Rekodi zinaonesha kuwa sasa Yanga wameshinda Ngao ya Jamii mara sita. Mwaka 2001 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2002 na 2003 mshindi alikuwa Simba. Mwaka 2004 mechi hiyo haikuchezwa. Mwaka 2005 mshindi alikuwa Simba. Mwaka 2006-2008 mechi hiyo haikuchezwa.
Mwaka 2009 mshindi alikuwa Mtibwa Sugar. Mwaka 2010 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2011 na 2012 mshindi alikuwa Simba. Mwaka 2013 na 2014 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2015 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2016 mshindi alikuwa Azam FC.
Takwimu zinaonesha kuwa Simba na Yanga zimewahi kuchukua kombe hilo mara tatu mfululizo. Yanga walifanya hivyo mwaka 2013, 2014 na 2015. Nao Simba wakajibu mapigo kwa kuchukua mara nne mfululizo mwaka 2017, 2018, 2019,2020. Na sasa Yanga wamechukua taji hilo mara ya sita mwaka 2021.
Comments
Loading…