“Mtoto jino linamuuma sana”. Hii ndiyo kauli ya kwanza ya mke wangu asubuhi ya leo.
Niliinama kutafakari kauli yake, kauli ambayo kila asubuhi huwa inapita kwenye ngoma ya masikio yangu.
Kauli inayonikera na kunipa mawazo sana na kuna wakati mwingine huruma huwa inaniingia sana kwa sababu ya maumivu anayoyapata mtoto wangu.
Kujali kwangu kulionekana kwa kumnunulia dawa za kutuliza maumivu. Kila uchwao nilikuwa mteja mzuri kwenye maduka ya madawa. Nilikuwa mteja mahiri, ilikuwa ni ngumu kupitisha siku bila kwenda duka la dawa kununua dawa ya kutuliza maumivu ya jino la mtoto wangu.
Nilijua hiyo ndiyo dawa tosha, tena ilinipa imani kipindi ambacho nilikuwa namuona anacheza kwa furaha mara baada ya kumpa dawa ya kutuliza maumivu.
“Kuna dawa nimeziweka mezani chukua umpe”-hili ndilo lilikuwa jibu langu kwa mke wangu baada ya kuniambia kuhusu maumivu ya jino la mtoto wangu.
“Hivi mume wangu tutakuwa tunampa dawa ya kutuliza maumivu mpaka lini?”. Aliniuliza swali ambalo jibu lake lilikuwa gumu kwa sababu tumetumia muda mwingi sana kumpa dawa za kutuliza maumivu lakini hakuna mabadiliko yoyote ndani yake.
Akili yangu ilikuwa inaniaminisha kuwa dawa za kutuliza maumivu ni tiba bora kuliko tiba yoyote. Tabasamu alilokuwa anatoa mtoto wangu kipindi nilipokuwa nampatia dawa za kutuliza maumivu lilikuwa tabasamu ambalo lilikuwa linaniaminisha kuwa huo ndiyo uponaji.
Niliamini kupitia dawa zile kwa sababu sikuwa na elimu ya ziada ya dawa ya jino. Nilikuwa na kilema cha akili.
Akili yangu ilikuwa haitaki kabisa kujifunza kitu cha ziada, ilikuwa inaamini kwenye uwezo wangu wa mwisho wa kufikiria.
Sikutaka kuishughulisha akili yangu tena iwaze kitu kipya, niliiamini akili yangu kuliko kitu chochote, hakuna mtu ambaye angekuja kuniaminisha kitu kingine tofauti na kitu ambacho nilikuwa nakiamini.
Niliamini kupitia kutumia dawa za kupunguza maumivu katika kutibu jino la mtoto wangu, lakini mke wangu aliamini dawa nyingine ambayo ilikuja kuwa tiba sahihi ya ugonjwa wa mtoto wangu.
Aliamini tiba sahihi ya jino ni kuling’oa. Ndicho kitu alichoƙifanya. Alifanikiwa kwenye hicho kitu, mtoto hakusumbuliwa tena na jino. Sikuwahi kusikia kelele za mtoto kulalamika kuhusu jino, hata safari zangu za kwenda kwenye maduka ya madawa zilisimama.
Hii ni kwa sababu mzizi wa tatizo ulikuwa umeshatolewa. Nilitumia akili na muda wangu mwingi kupoza tatizo na kuacha kutoa mzizi wa tatizo.
Hapa ndipo linapokuja tatizo la ufanisi hafifu wa taasisi mbalimbali kipindi zinapokutana na matatizo mbalimbali.
Hawatumii muda mrefu kufikiria namna sahihi ya kutoa mzizi wa tatizo. Mawazo yao huishia namna ya kupata pesa za kutuliza tatizo husika.
Leo hii Yanga wanalia, hawana pesa za kufanya usajili bora utakaowasaidia katika michuano mbalimbali. Hawana pesa hata za kulipa mishahara ya wachezaji wao.
Akili yao inamuwaza Manji, kwao wao wanaamini kuwepo kwa Manji ndiko kutatibu tatizo kuu la klabu yao.
Wanaamini katika kumtengeneza mtu imara na kusahau kuwa kutengeneza taasisi imara kutakuwa tiba kuu ya tatizo lao kuu.
Dawa za kupunguza maumivu wanazipenda sana, na wanaziamini sana. Leo hii Manji atarudi kama mwenyekiti wa klabu, atatumia pesa zake kuisaidia Yanga, hii itakuwa tiba la tatizo la Yanga?
Manji ataondoka Yanga akimaliza muda wake wa uongozi, hatoongoza milele. Akiondoka Yanga itakuwa katika mazingira yapi mwisho wa siku?
Kwanini wasitengeneze mazingira bora ambayo yatamfanya Manji aje kibiashara, aweke pesa zake kibiashara ili yeye anufaike na klabu pia inufaike ?
Tukiendelea kumtengemea mtu mmoja imara na kuacha kufikiria kutegemea mfumo mmoja imara tutakuwa vilema wa akili katika maisha yetu.