in , , ,

MIGUU YA NEYMAR HAINA DNA YA BALLON D’OR

Inawezekana ndiyo ndoto yake ya muda mrefu. Ndicho kitu ambacho anakitamani kila uchwao kuwa nacho katika mikono yake.

Amekipigania sana kwa muda mrefu, tena amepigana mbele ya mafahari wawili ambao waligana Ballon D’or ndani ya miaka kumi iliyopita (Cristiano Ronaldo akichukua mara 5 na Lionel Messi akichukua mara 5).

Hawa ndiyo watu ambao walifanikiwa kujitengenezea ufalme wao baada ya kuitumikisha miguu yao kila walipokuwa wanakanyaga nyasi.

Walihakikisha miguu yao iwe na ukomavu mkubwa, ukomavu ambao ulikuwa na manufaa kwao na timu ambazo walikuwa wanazichezea.

Watu wengi tulifanywa kuamini kuwa kama Cristiano Ronaldo au Lionel Messi akiwa uwanjani unatakiwa usubiri mpaka filimbi ya mwisho ya mwamuzi ndipo utoke na matokeo yako.

Hii ni kwa sababu miguu yao ilikuwa na ukomavu mkubwa, ukomavu ambao unakosekana katika miguu ya Neymar JR. 

Huyu ndiye aliyekuwa anaonekana ana uwezo wa kuleta changamoto kubwa katika tunzo za Ballon D’or.

Sanaa zake zilizopo ndani ya miguu yake zilitupa matumaini makubwa, tukawa tunasubiria siku ambayo atachukua mbele ya hawa mafahari wawili.

Na kuna wakati watu walidiriki kusema siku ambayo hawa mafahari wawili watakapoondoka ndiyo itakuwa siku ya Neymar JR kutawala kwenye utoaji wa tunzo hizi za Ballon D’or.

Uso wake, moyo wake umejaa matamanio makubwa kuhusu kuchukua tunzo hii lakini miguu yake inapingana na matamanio yake yaliyo moyoni mwake.

Hakuna ukomavu wowote ndani ya miguu yake. Amekuwa mtu wa kuchelewa kufanya maamuzi kipindi anapokuwa na mpira. 

Kichwa chake hutamani kuisurubisha miguu yake ifanye mambo kumi kwa wakati mmoja kila anapopokea mpira.

Hii tabia siyo rafiki kwa wachezaji ambao wanataka kuchukua Ballon D’or. Wachezaji wote ambao waliwahi kuchukua Ballon D’or miguu yao ilikuwa inafanya maamuzi bora yaliyokuwa na msaada kwenye timu zao.

Hii imekuwa tofauti na kwa Neymar JR, hawezi kufanya chochote bila kupiga chenga au kukokota mpira hata sehemu ambayo haitaji kufanya hivo.

Brazil iliwahi kuwa na KAKA , mchezaji wa mwisho wa Brazil kuchukua tunzo ya Ballon D’or, mchezaji ambaye alikuwa na sanaa miguuni mwake lakini alikuwa na maamuzi ya ukomavu.

Ronaldinho Gaucho alibarikiwa utajiri wa sanaa ya mpira kwenye miguu yake, lakini alijua kutenganisha wakati sahihi wa yeye kufanya sanaa na wakati sahihi wa yeye kufanya maamuzi muhimu ndani ya timu yake ndiyo maana alifanikiwa kubeba Ballon D’or. 

Hapa ndipo DNA ya Ballon D’or inapoanzia. Maamuzi muhimu na sahihi katika wakati sahihi yatakuwa Ballon D’or katika muda sahihi.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

YANGA IMESHINDWA KUTIBU KILEMA CHA AKILI

Tanzania Sports

Ronaldo kwenda Juventus