in , , ,

WYDAD CASABLANCA NA HESHIMA LIGI KUU TANZANIA

UBORA wa Ligi unapotangazwa unavutia pande nyingi katika kutafuta vipaji na fursa pamoja na kuchunguza kujua siri za kupanda kwake. Katika takwimu za soko hivi sasa kuanzia CAF na Taasisi nyinginezo Ligi Kuu Tanzania inapatikana katika 10 bora za Afrika.

 Kutajwa kuwa miongoni mwa Ligi bora kumetokana na sababu nyingi ikiwemo kushiriki mashindano ya Kimataifa na kupata matokeo mazuri. Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Yanga wameweka rekodi za kujivunia kushiriki mara kwa mara na kuwapa changamoto vigogo wa Soka Afrika. Timu mbalimbali ikiwemo Al Ahly, Sfaxien, Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates, Kaizer Chiefs, Raja Casablanca, Pyramid, na nyinginezo zimefika kucheza nchini katika mashindano ya CAF. Ushiriki mzuri ndiyo sababu ya kuinua kiwango cha Ligi. 

Hata hivyo hivi karibuni klabu ya Wydad Casablanca imetuonesha namna wanavyoiheshimu Ligi Kuu Tanzania. Hii inaleta tafsiri kwamba kutajwa katika nafasi 10 bora maana yake kunachochea timu mbali kutupia jicho katika vikosi vya Ligi Kuu. 

Mpira wa miguu unahusishwa na utawala mzuri, utaaalamu, uvumbuzi wa vipaji pamoja na kuunda timu bora. Hivyo basi vilabu mbalimbali vinafanya jitihada kuhakikisha wanachunguza vipaji vilivyopo Ligi. Wataalamu wa kusaka vipaji wanavutiwa kujua nini hasa linachoendelea kwenye Ligi hii hadi ikatajwa mbabe mbele ya zingine zilizokuwa maarufu miaka ya nyuma kama vile Zambia, DRC, Ghana, Nigeria na hata Cameroon. 

WACHEZAJI WA KIGENI

Wasaka vipaji wamebaini kuwa ubora huo pia unapata mchango kutoka kwa wachezaji wa kigeni. Wapo wachezaji kutoka Mataifa mbalimbali ikiwemo Ghana, Nigeria, Cameroon, Afrika kusini, Zambia, Zimbabwe, Burkina Fasso kwa kutaja chache. Wachezaji wa kigeni wametoa mchango mkubwa katika vipaji vya Kitanzania ikiwemo kuving’arisha na hivyo kusababisha vilabu vya nje kuwinda wachezaji wenye vipaji hapa nchini. 

KUONEKANA AFRIKA 

Ni dhahiri pia Soka la Tanzania linapiga hatua katika kuwavikia wengi na ili kufikia maendeleo ya kandanda lazima timu ziwe zinashiriki mashindano ya CAF ambayo ni jukwaa muhimu la kuonesha vipaji. Kuonekana kwa wachezaji pia kinatokana na mchango wa haki za Televisheni ambapo mechi mbalimbali zinaoneshwa kwenye viwanja vya Ligi Kuu na kutangaza vipaji vinavyoshiriki. Kwahiyo Azam Tv wanatoa mchango mkubwa kwenye kuonesha Ligi hii kwani hata vipaji ambavyo havishiriki mashindano ya CAF vinaweza kupewa heshima na kununuliwa. 

UJIO WA PILI WA WYDAD

Simon Msuva alikuwa staa wa Wydad Casablanca kabla ya kuachana na timu hiyo. Kipaji chake kilionekana mbele ya maelfu ya mashabiki wa Kiarabu ambao walivutiwa naye na kuona kuwa Tanzania Kuna vitu muhimu vya kuangalia ikiwemo ni mchezo wa Soka. 

Kwa mara ya pili Wydad Casablanca wamekuja kufanya usajili kwenye Ligi Kuu Tanzania. Safari hii wamemsajili staa wa Fountain Gate, Selemani Mwalimu. 

Huyu ni mchezaji ambaye alikuwa anahusishwa kusajiliwa na timu kadhaa hapa nchini ikiwemo Yanga na Simba. Tetesi za usajili ambazo zimekuwa zikiibuliwa na wadau na watu walioko kwenye Kamati za usajili zilieleza kuwa mchezaji huyo ni miongoni mwa wanaotajwa mara nyingi katika usajili wa timu mbalimbali. 

Seleman Mwalimu ametoka katika klabu ya  Fountain Gate na kujiunga na Wydad Casablanca ya Morroco katika usajili ambao umeibua sura nyingine ya Ligi Kuu Tanzania. Pengine huu ni usajili bora kwa Seleman Mwalimu na kwa maendeleo ya Soka la Tanzania.

JE NINI SIRI YA WYDAD CASABLANCA?

Wakati usajili huu unaweza kuondoakana kama kitu cha kawaida kwenye Soka Lakini inaonesha mabadiliko makubwa kutoka kuwachukua wachezaji wa Kitanzania kisha kuwafanyia majaribio kama wanafaa au la, hadi kuwasajili moja kwa moja.

Hapo ndipo unaweza 

 ukajiuliza Wasaka vipaji (Scout) wa Wydad Casablanca walimuona wapi Seleman Mwalimu kama mchezaji hitaji lao? Je walimuona akicheza Ligi ya Mabingwa Afrika? Jibu ni hapana. Je, walimuona Seleman Mwalimu akicheza Kombe La Shirikisho Barani Afrika? Jibu pia linakuwa hapana.

Hata hivyo jambo moja ambalo lipo dhahiri shahiri ni kwamba  Wasaka vipaji wa Wydad Casablanca walimuona Seleman Mwalimu akiwa ndani ya kikosi cha  Fountain Gate akicheza Ligi Kuu ya NBC ya Tanzania. Hii ni Ligi ambayo inaoneshwa na Kituo cha Televisheni cha Azam TV.

Hii inathibitisha wazi kabisa Ligi Kuu imestahili  kushika namba 4 barani Afrika kama mojawapo ya Ligi 10 bora na zenye mvuto wa kutazamwa na na wadau mbalimbali duniani. 

Kimsingi usajili wa Seleman Mwalimu unaonesha kuwa sio jambo la kawaida timu kama Wydad Casablanca ambayo Juni mwaka huu itacheza Klabu Bingwa ya Dunia inamsajili mchezaji wa Fountain Gate ya Tanzania. Bila shaka yoyote washabiki na wadau wa Soka watafurahishwa na usajili huu. Tena usajili wa kushtukiza kwani Wydad Casablanca hawakwenda kuwinda Saini ya wachezaji wa timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho badala yake wamemtazama nyota huyo kama ndiye mchezaji anayeweza kutanua changamoto yao katika upachikaji wa mabao. Kilichobaki sasa ni kwa Seleman Mwalimu mwenyewe kuwa Balozi mzuri wa Ligi Kuu kama ilivyokuwa kwa Simon Msuva aliyewakilisha vema Soka la Tanzania katika Ligi Kuu ya Morocco. 

JE SELEMAN MWALIMU NI MCHEZAJI WA AINA GANI?

Kwanza tufahamu kuwa huyu ni mshambuliaji. Ni mchezaji ambaye anacheza kwa kazi moja tu; kupachika mabao Kwa ajili ya timu yake. Kazi yake ni kumalizia krosi, pasi na mapishi yote ya kusaka manao.  Ni mshambuliaji ambaye katika Ligi anaweza kukupatia mabao 15. Lakini pia ni mshambuliaji mwenye uwezo wa kupiga mashuti makali langoni na kupambana na mabeki. Ni mshambuliaji wa asili kuliko wale wanaopangwa kama njia ya kutimiza idada yao hata kama wao sio nambari 9 asilia. Ni wakati wa Seleman Mwalimu kudhihirisha kuwa Ligi Kuu Tanzania ina washambuliaji wakali na wenye ubora unaoipaisha Ligi hiyo na kuwa miongoni mwa kumi zenye mvuto na ubora Afrika. 

Heko Seleman Mwalimu. Kila la heri.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

AMORIM NA RASHFORD NI KAMA PAKA NA PANYA

Tanzania Sports

ARSENAL UBINGWA WAO UPO KWENYE MECHI ZA KIUME