“Kiyumbi tuendelee kutazama mechi ya Mbao”. Haya yalikuwa maneno ya rafiki yangu ambaye alikuwa ananisihi niendelee kukaa kwa ajili ya mechi ya Mbao.
Mechi ambayo ilikuwa inafuata baada ya mechi ya Simba kuisha. Simba ambayo ilikuwa inaonekana kama timu imara kwenye michuano hii ya sportpesa.
Timu ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa sana ya kuchukua kombe hili la sportpesa. Kutokana na sababu nyingi.
Moja, Simba ndiyo timu pekee kwenye michuano hii ya Sportpesa ambayo iko katika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Michuano mikubwa sana barani Afrika kwa ngazi ya klabu, hii ndiyo michuano ambayo ina pesa kubwa kuzidi michuano yote ya vilabu hapa Afrika.
Ukiachana na Gormahia ambayo iko kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika, Simba ndiyo ilikuwa inaonekana ndiyo timu tishio.
Pili, Simba ilikuwa na kikosi ambacho ni kipana na chenye wachezaji wengi bora. Tulitegemea hawa wachezaji wangekuwa chachu ya mafanikio ya Simba kwenye michuano hii.
Tatu, Simba huwa inajinasibu kila siku kuwa Simba katika uwanja wa Taifa ni ngumu kuifunga. Ni ngumu sana kupata ushindi mbele ya Simba kwenye uwanja wa Taifa.
Hiki kitu nacho kiliwapa imani watu wengi kuwa kwa sababu hili kombe liko katika uwanja wetu wa nyumbani hivo, timu zetu zitatumia nafasi hii kufanya vizuri.
Lakini ilikuwa tofauti kabisa na matarajio yetu. Kiasi kwamba mechi ya Simba na Bandari ilipoisha sikuona sababu ya mimi kuendelea kutazama mechi ya Mbao.
Rafiki yangu alinisihi sana niendelee kubaki tuwatazame Mbao. Nilikubali kishingo upande. Lakini kuna kitu cha tofauti ambacho nilikiona.
Nilimshukuru sana rafiki yangu kwa kunisihi niendelee kubaki kuendelea kutazama hiyo mechi kwa sababu ilinipa funzo moja kubwa sana.
Funzo lipi?, Nilijifunza kuwa Watanzania wengi wanapenda sana mpira kuliko tunavyofikiria. Wanapenda sana kuziona timu zetu zikifanya vizuri sana.
Lakini tatizo linakuja kwa timu zetu kuwaangusha Watanzania. Wengi wa watu ambao walikuwepo kwenye uwanja wa Taifa kwenye mechi ya Mbao walikuwa wanaipa ushirikiano mzuri sana Mbao.
Waliishangilia vizuri sana Mbao, kitu ambacho kilinishangaza sana. Ulitazama wakati wa penalti?, uliona nini?
Kipi kilikuwa kinakuvitia hasa hasa kutoia jukwaani?, uliona ambavyo Watanzania walivyokuwa wanashangilia kila Mbao walipokuwa wanafunga goli?
Uliona walivyokuwa wanaiombea Mbao ili iweze kushinda hiyo mechi ?, uliona jinsi walivyokuwa wanaumia kila Mbao walipokuwa wanakosa penalti?
Haya yalikuwa mapenzi makubwa sana kwa mpira wetu, siyo kwa Mbao pekee. Haya yalikuwa mahaba makubwa kwenye mpira wetu.
Hii ilikuwa ishara kubwa sana kuwa mashabiki wetu wanapenda sana mpira wetu. Wanaufikiria sana mpira wetu.
Wanatamani sana kuuona mpira watu ukifika mbali. Na hii siyo Mara ya kwanza tu. Hata kwenye mechi za Mtibwa Sugar za kimataifa.
Wengi walikuwa wanaiunga mkono sana Mtibwa Sugar. Walikuwa wanafurahia kuiona Mtibwa Sugar kila ilipokuwa inafunga goli.
Na walikuwa wanaumia kuiona Mtibwa kila ilipokuwa inafungwa. Hii ni dalili tosha kubwa kuwa Watanzania wanapenda mpira.
Tatizo linakuja kuwa mpira sisi hautupendi kabisa. Kwenye michuano ya Sportpesa iliyofanyika katika ardhi yetu imeonesha kabisa jinsi ambavyo mpira hautupendi.
Siku mbaya ilianza kwa Singida United kutoka, akaja Yanga. Mwisho wa siku Mbao na Simba nao wakatoka.
Ni wakati sasa kwa viongozi wa mpira wa miguu kuona mapenzi makubwa ambayo yanaoneshwa na mashabiki wa mpira wetu.
Mapenzi ambayo wanaweza kuyafanya yawe nguvu kubwa kwao wao kutengeneza timu ambazo ni imara , timu ambazo zinaweza kushindana sana na watu.
Timu ambazo zinaweza kutupa sifa kubwa sisi Watanzania. Timu ambazo zitaendana na mapenzi yetu. Haiwezekani sisi tukawa na mapenzi makubwa afu mpira wetu ukawa mbovu.