*Ni ushamba. Watu na akili zao timamu wanahesabu Yanga au Simba ina wachezaji wangapi kwenye timu ya taifa!
WATANZANIA wa kizazi hiki,tofauti na wa enzi ile, hawajui maana ya timu ya taifa. Kwa watanzania wengi wa leo, timu ya taifa maana yake ni wachezaji wa Yanga na Simba waliomo ndani na si timu moja ya vijana wa kitanzania wenye sifa za kuchezea timu hiyo bila kujali wanatoka timu gani. Hapo, uliopo si utanzania bali uyanga na usimba.Enzi zile za timu ya taifa, kwa mfano, iliyoimbwa na Moro Jazz Band mwaka 1972, watanzania walikuwa wanawapenda na kuwathamini wachezaji wao wote kwa usawa. Wachezaji wetu wote kama walivyotajwa na Moro Jazz ya Mbaraka Mwinshehe kwenye wimbo wake wa kuitakia heri FAT na wachezaji hao mwaka 1972 walikuwa:-(Omari) Mahadhi (African Sports ya Tanga), Elias (Michael), (Yanga). hao walikuwa makipa. Akafuatia kutajwa (Hassan) Gobbos (Yanga)Wakafuata (Omari) Zimbwe (African Sports, Tanga), Mweri (Simba) (Tanga). Wakatajwa zaidi (Mohammed) Chuma (Nyota ya Mtwara) na (Mohammed) Msomali (Cosmopolitan, Dar). Kisha wakafuata Abdulrahman (Juma) (Yanga), Sunday (Manara) (Yanga) na Willy (Mwaijibe) (Simba). Wakatajwa baadaye (Abdallah) Kibaden (Simba) na Kitwana (Manara). Wakamaliziwa (Kassim) Manga (Morogoro), (Gibson) Sembuli (Yanga) na (Nassoro) Mashoto (Zanzibar).Kwenye timu hii iliyotajwa na Moro Jazz, ambayo, ukimuondoa Mashoto, ndiyo ilikuwa kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara kilichocheza Chalenji mwaka 1971 nchini Kenya na wenyeji kubeba kombe la mashindano ya timu nne za Kenya, Uganda, Tanzania Bara na Zanzibar, kulikuwa na wachezaji sita wa Yanga,Simba wawili, Cosmo mmoja na waliobaki walitoka Tanga watatu, Morogoro, Mtwara na Zanzibar mmoja mmoja.Sababu ni kwamba kwanza, kipindi hicho Yanga ilikuwa nzuri zaidi ya Simba (Sundeland Sports Club mpaka mwaka 1971), ikichukua ubingwa wa nchi hii mfululizo tangu mwaka 1969 na hivyo kucheza mashindano ya ubingwa wa Afrika mfululizo ambapo mwaka 1969 ilitolewa kwa kura ya shilingi na Asante Kotoko ya Ghana, kiungo Abdulrahman Juma mkali wa kuchonga kona, mpachika mabao, hasa ya kichwa, Kitwana Manara, beki kisiki Hassan Gobbos na kipa asiyefungika kirahisi Elias Michael walishiriki pambano hilo la kihistoria lililoanzia Kumasi, Ghana na kumalizikia Dar es Salaam, Tanzania ilikorushwa shilingi baada ya sare ya mechi hizo mbili.Chipukizi Gibson Sembuli kutoka Morogoro na chipukizi Sunday Manara waliingizwa Yanga kuanza kusuka kikosi cha baadaye, hasa baada ya wazoefu kadhaa kuonekana wanakaribia ukingoni mwa utoaji wa huduma kama mkali Maulid Dilunga ambaye tangu mwaka 1971 mpaka mwaka 1972 alikosa namba kwenye timu ya taifa lakini alipoibuka mwaka 1973 akafanya mambo yaliyomwezesha kuchaguliwa kwenye timu ya Afrika iliyoenda Mexico kwa ziara ya kimichezo. Pamoja naye kwa hapa kwetu alichaguliwa pia kipa Omar Mahadhi.Sababu ya pili ni kwamba Simba, iliyokuwa inajisuka upya tangu mwaka 1971 kwa kuingiza chipukizi wengi ili kuvunja ufalme wa Yanga wa miaka mingi nchini, ilikuwa na chipukizi wawiliambao walikuwa na sifa ya kuchezea timu ya taifa miongoni mwa chipukizi kama hao wawili Abdallah Kibaden na Willy Mwaijibe kutoka Dar es Salaam. Ukiacha hao waliokuwa na sifa ya kuchezea timu ya taifa, chipukizi wengine wa Simba walikuwa Haidar Abeid toka Shinyanga, Khalid Abeid toka Mwanza (hawa si ndugu), Adam Sabu, Shaaban Baraza na Omar Choggo toka Morogoro na wengine wengi. Kweli, miaka miwili baadaye, chipukizi hawa walibeba ubingwa wa Tanzania na mwaka uliofuata 1974 walibeba ubingwa wa kwanza wa mashindano ya kwanza ya vilabu bingwa vya Afrika Mashariki na kufika nusu fainali ya ubingwa wa Afrika. Hii ni faida ya kusuka kikosi cha vijana na kukilea.Sababu ya tatu ni kwamba wachezaji wote toka mikoani na Zanzibar walikuwa wa viwango vikubwa kustahili kuchezea timu hiyo. Kwa mantiki hiyo, hiyo ilikuwa timu ya taifa kikweli na Watanzania waliipenda mno bila ubaguzi wa wachezaji. Hali ya Watanzania kuithamini bila ubaguzi timu yao ya taifa iliendelea hivyo miaka ya 1980 ikiwa na wachezaji wengi wa Pan African, Yanga na Simba huku Mwanza kwa Pamba na Ruvuma kwa Majimaji kukianza kutoa wachezaji kwa timu hiyo. Hali ilikuwa shwari mpaka miaka ya 1990 na mabadiliko ya ushabiki wa wachezaji wa timu ya taifa kulingana na wanachezea klabu zipi yalianza taratibu miaka ya 2000 na sasa utaratibu huo wa kijinga umekomaa mno miaka hii ya 2010.Ni ushamba. Watu na akili zao timamu wanahesabu Yanga au Simba ina wachezaji wangapi kwenye timu ya taifa! Watu hawa sijui wangesemaje wakati Simba, ikiwa chini ya kocha toka Yugoslavia ya wakati huo, Dragam Popadic, ilijaza zaidi ya asilimia 90 ya wachezaji kwenye timu ya taifa kutokana na ubora wa wachezaji wa timu hiyo waliopikwa na kocha huyo. Hakuna aliyekasirika wa upande wa Yanga kwani wachezaji hao wote walistahili kuchezea timu hiyo.Watanzania wengine wa leo wa tabia hii wangefanyaje pale timu ya taifa ilipokuwa chini ya kocha Sunday Kayuni ilipokuwa na wachezaji karibu wote wa Yanga kutokana na kocha huyo kuwapika mwenyewe wachezaji hao akiwa nao Yanga na kweli walipikika vizuri. Hakuna aliyelalamika wa upande wa Simba kwani wachezaji hao walikuwa viwango kweli kweli.Leo hii Simba wakizidi kidogo tu idadi kwenye timu ya taifa, vita toka mashabiki wa Yanga wakiizomea timu yao ya taifa! Hivyo hivyo kwa mashabiki wa Simba Yanga inapokuwa na wachezaji wengi wanaostahili kabisa kuchezea timu ya taifa. Huu ni ushamba uliopitiliza. Hatuwaoni wenzetu wa Hispania mashabiki wa Real Madrid, Atletico Madrid, Malaga, Real Betis , Rayo Vallecano, Valencia, Levante, Real Sociedad,Getafe, Sevilla na zote unazozifahamu ambao wanaishangilia timu yao ya taifa kwa nguvu zote licha ya kujaza wachezaji wa Barcelona ambao kwa kweli ni wachezaji wa Hispania wenye viwango vya juu vya kustahili kuchezea timu ya taifa. Wanaipenda timu yao ya taifa kwa dhati bila kujali imejaza wachezaji wa timu moja pinzani kwenye ligi kuu yao ya La Liga.Watanzania inabidi tujifunze kwamba anayeweza anaweza tu hata kama humpendi. Hivi kwa sasa utawaacha kweli kwenye timu ya taifa wachezaji hawa wa Simba, ili kuwafurahisha mashabiki wa Yanga, kutokana na viwango vyao kina kipa Juma Kaseja, beki Shomari Kapombe, beki Amir Maftah,viungo wa kati Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba na Jonas Mkude pamoja na kiungo wa pembeni Mrisho Ngassa?Timu ya FIFA ya kufikirika (Dream Team) imeundwa na wachezaji hawa wanaocheza ligi ya Hispania tu kutoka mataifa machache tofauti; kipa Iker Cassilas (Real Madrid, Hispania). Mabeki Daniel Alves (Barca,Brazil), Sergio Ramos(Real Madrid, Hispania),Gerald Pique (Barca, Hispania) na Marcelo (Real Madrid,Brazil).Viungo ni Xabi Alonso (Real Madrid, Hispania), Xavi (Barca,Hispania) na Andres Iniesta (Barca, Hispania). Wapachika mabao ni Lionel Messi (Barca, Argentina), Cristiano Ronaldo (Real Madrid, Ureno) na Radamel Falcao (Atletico Madrid, Colombia)Ukifanya mchanganuo wa wachezaji hao utapata majibu yafuatayo:-(1) Ligi wanayocheza:- wote La Liga ya Hispania(2) Klabu wanazochezea:-Barca watano (5), Real Madrid watano(5) na Atletico Madrid mmoja (1)(3) Mataifa wanakotoka:- Hispania sita(6), Brazil wawili (2),Argentina mmoja (1), Ureno mmoja(1) na Colombia mmoja(1)Kwa hiyo wote ni wa Ligi Kuu ya Hispania,wengi ni wa Barcelona na Real Madrid na wengi ni wa Hispania lakini ni timu ya Dunia. Miongoni mwa hao hutasema kwamba kuna asiyestahili kuwemo kwenye timu hiyo lakini utasema kwa usahihi kwamba wapo waliostahili kuwemo lakini hawamo. Na hii haiepukiki kwani nafasi zilizostahili ni 11 tu na zote zimejaa.Kwa funzo hili watanzania tubadilike kwa kuipenda timu yetu ya taifa hata ikiwa ya Simba tupu au Yanga tupu kulingana na ukubwa wa viwango vya wachezaji watakaochaguliwa kuichezea timu yetu hiyo.
in Sport, Sports News
Comments
Loading…