Wachambuzi, mashabiki na baadhi ya wadau wa michezo wanamlaumu kocha huyo kumweka benchi golikipa wake namba moja…
KWA uraia wake ni Mhispania. Ni miongoni mwa makocha wa kigeni walioonesha umahiri katika Ligi ya England. Wapo makocha Wahispania ambao wamefanya vizuri kuliko Mikel Arteta, kwa mfano Rafael Benitez na Pep Guadriola majina makubwa yaliyoweka alama EPL. Wote wawili wameshinda mataji ya Ligi ya Mabingwa. ni Liverpool na Man City.
Ujumla wapo makocha kadhaa raia wa Hispania ambao wamezinoa timu za EPL kwa nyakati tofauti. Mikel Arteta kijana wa Arsene Wenger ameingia kwenye orodha, lakini anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuipa mafanikio Arsenal. Msimu uliopita Arsenal walikosa ubingwa katika dakika za majeruhi mbele ya Man City. Ulikuwa ushindani wa makocha wa Kihispania pekee.
Ushindani ambao bado ungalipo na kila mmoja anataka kuonesha ufundi wake na kuwa yeye ni maji marefu kwa mwingine. Msimu mpya wa 2023-2024 umeanza huku Mikel Arteta akiwa ameingia katika lawama na kelele zinazoelekezwa kwake ni nyingi.
Wachambuzi, mashabiki na baadhi ya wadau wa michezo wanamlaumu kocha huyo kumweka benchi golikipa wake namba moja, Aaron Ramsdale na badala yake kamsajili David Raya raia wa Hispania aliyekuwa akiidakia klabu ya Brentford. Hoja zinazoibuliwa ni kwamba Mikel Arteta anampendelea ndugu yake David Raya kwa vile wote ni raia wa Hispania. Kwamba Mikel Arteta ameamua kuwapunguzia England nguvu kwa kumweka benchi golikipa wao namba mbili wa timu ya taifa Aaron Ramsdale. Wengine wanasema hamtendei haki kipa huyo.
Kwa upande wake Ramsdale katika makala yake aliyoandika kwenye mtandao wa The Players Tribute amewahi kusema “Sijawahi kushangazwa na usajili wa mchezaji wa kushindana naye. Tangu siku ya kwanza nafahamu hilo linatokea, waleteni wote tushindane, nimekulia mazingira hayo, na nilishawahi kuambiwa sitoweza kufika mbali katika kandanda. Leo nipo EP.,”
Huo ndiyo mtazamo wa Ramsdale linapofika suala la ushindani. Maelezo aliyotoa ni marefu na mengi kuhusu maisha yake ya mpira hadi alipotakiwa na Arsenal kupitia Bukayo Saka. Lakini je ni kwanini Mikel Arteta amesajili kipa mwingine wakati anaye Ramsdale tena akiwa na kiwango bora? TANZANIASPORTS inaleta majibu ya uchunguzi wake kwenye usajili huo, hali halisi na makosa ya wanaomkosoa Arteta.
KWANINI DAVID RAYA AMESAJILIWA ARSENAL?
Hili ndilo swali la wengi, lakini jibu la haraka ni kuimarisha timu ya Arsenal. Jibu hilo linatokana na utaratibu wa timu kuimarisha vikosi vyake. Lakini sababu kuu ya usajili huu inaweza kuwa zaidi ya hapo. Kwanza David Raya anamzidi Ramsdale kwenye eneo la matumizi ya miguu akiwa langoni. Kwamba Raya anao uwezo mkubwa kupanda hata yadi 26 toka langoni na kutulia eneo ambalo wanazurura mabeki.
Kwa maana hiyo hii ni changamoto kwa Ramsdale kujifunza namna bora ya kufuata mbinu za kisasa za golikipa. Majukumu ya makipa kwa sasa yameongezeka, wao ni vyanzo vya mashambulizi na kupika mabao. Kwahiyo eneo hili limeonesha tofauti.
Hata hivyo Ramsdale si mbaya katika matumizi ya miguu akiwa langoni. Msimu wake wa kwanza akiwa Arsenal na hali aliyonayo sasa ni tofauti sana. Ramsdale wa sasa amebadilika na kujitahidi kutumia miguu pamoja na ukuchangamsha nafasi ya golikipa, na bila shaka benchi la ufundi limehusika.
SIRI KUU YA KUSAJILIWA DAVID RAYA NI HII
Ilikuwa takribani miaka 12 Arsenal hawakuwa kwenye kinyang’ayiro cha Ligi ya Mabingwa. wamepigania nafasi hiyo licha ya kukosa ubingwa wa EPL. Arsenal ya sasa inatafuta mataji manne; EPL,Carabao,FA na Ligi ya Mabingwa. kwa maana hiyo majukumu ya klabu yameongezeka kuliko misimu iliyopita ambako walikuwa na kazi ya kupigania mataji ya ndani pekee yake. Kwa maana Mikel Arteta anahitaji wachezaji waliotimia na mahiri katika kila eneo.
Kwa kuona njia ya kuimarisha safu ya ulinzi, ni muhimu kusajili golikipa wa kusaidiana na Ramsdale. Tathmini ya TANZANIASPORTS inaonesha kuwa isingewezekana kwa Aron Ramsdale kuwa golikipa namba moja kila mechi katika mashindano yote. Hebu fikiria Ramsdale akiumia, kisha Mikel Arteta akigeukia benchi lake ili kumwita golikipa namba mbili, huku akikabiliwa na mashindano hayo?
Hebu fikiria Ramsdale angecheza mechi zote bila kupumzika, bila shaka wangekaribisha makosa katika mechi nyingine kama ilivyokuwa kwa David De Gea. Makosa mengi aliyofanya langoni yalichangiwa na namna alivyotumika bila kupumzika hivyo uchovu nao ukamtafuna. David Raya amekuja Arsenal kuongeza nguvu ya kikosi hicho si kuchukua nambari ya mwenzake Ramsdale.
Usajili wa David Raya umeangalia ongezeko la Ligi ya Mabingwa, hivyo kila upande wanahitajika makipa timamu kuliko kumtegemea mmoja kuwa namba moja katika mechi zote na mashindano yote.
Comments
Loading…