NAFASI YA WASEMAJI WA VILABU NA MUSTAKABALI WA MICHEZO YETU
Vilabu vya michezo nchini Tanzania viko kwenye hali ya njia panda. Njia panda hiyo ni kuamua kwenda njia ipi baina ya njia kuu mbili. Njia ya kwanza kubaki kuwa ni vilabu vya wanachama ambapo wanachama ndio wanaokuwa wamiliki wa vilabu hivyo na njia ya pili ni vilabu hivyo kuamua kutafuta wawekezaji alafu ziuzwe hisa za klabu hiyo na kisha wawekezaji hao kuzinunua na hatimaye kuwa ndio wamiliki wa vilabu hivyo na baada ya hapo vilabu hivyo kuanza kuendeshwa na wawekezaji hao. Safari ya mabadiliko haijawa rahisi na imekuwa inakumbana na vikwazo vingi na mojawapo ya vikwazo ni kwamba wanachama wa vilabu hivyo hawako tayari kwa ajili ya mabadiliko ya kiumiliki na uendeshaji wa vilabu hivyo. Changamoto nyingine ni kwamba baadhi ya wawekezaji wamekuwa wanakuja na ofa ambazo hazikubaliki kwa hao wanachama wa hivyo vilabu. Nafasi ya msemaji wa klabu imetumika kama njia ya kutengeneza nembo ya vilabu/ taasisi za michezo ili kuongeza tija katika malengo ya vilabu hivyo.
Katika zama za nyuma ambapo nchini Tanzania vilabu vingi vya michezo vilikuwa vinamilikiwa na kuendeshwa na mashirika ya umma hakukuwa na msisitizo mkubwa sana juu ya nafasi ya msemaji wa klabu wala afisa hamasa mkuu wa klabu kwani vilabu tayari vilikuwa na msingi wa awali wa mashabiki kupitia wafanyakazi wa mashirika hayo ya umma na pia nembo za mashirika hayo ndio ilikuwa nguzo ya vilabu hivyo. Uendeshwaji wa vilabu hivyo haukuangalia sana faida kwani vilabu hivyo vilikuwa kama ni sehemu ya burudani ya wafanyakazi wa mashirika hayo. Baada ya kufanyika kwa mageuzi ya kiuchumi nchini Tanzania ambapo mashirika mengi ya umma yalibinifasishwa wamiliki wapya wa mashirika hayo hawakuona umuhimu tena wa kuwa na vilabu vya michezo kama ilivyokuwa katika siku za huko nyuma.
Zama mpya za uendeshwaji wa vilabu zikavifanya vilabu vinatakiwa viendeshwe kibiashara na hivyo kuhitajika hamasa mpya ya kuvifanya vilabu hivyo viwe na mashabiki ili viweze kufanya biashara kupitia nembo zao za kibiashara. Hapo ikaibuka upya umuhimu wa nafasi ya maafisa habari ambapo kwa muktadha mwingine wakawa nao wanafanya kazi za afisa hamasa. Katika mfumo wa vilabu vya soka nafasi hii kwa mwanzoni ilikuwa Zaidi ni nafasi ya kujitolea na kwamba wengi wa waliokuwa wanajitolea ima walikuwa wanalipwa kiwango kidogo sana cha pesa ama mda mwingine hawalipwi kabisa. Miaka ya 2010 kwenda mbele ndio nafasi ya wasemaji wa vilabu ilivyopamba moto kwani kuliibuka kizazi kipya cha wasemaji ambacho kilikuja na ubunifu wa hali ya juu ya kuvipamba vilabu vyao na pia wakawa wanafanya ziara kwa vyombo vya habari mara kwa mara kwa ajili ya kwenda kuvinadi vilabu vyao kwa umma.
Katika vilabu vya Yanga na Simba kulizuka mpambano wa ubishani katika usemaji baina ya Jerry Muro ambaye alikuwa ni msemaji wa Yanga na Haji Sunday Manara ambaye alikuwa ndiye msemaji wa klabu ya Simba. Mvutano wao ulileta chachu Fulani ya dabi za baina ya timu hizo na licha ya kwamba kuna nyakati waliwahi kutoleana kauli chafu lakini kwa namna moja ama nyingine waliongeza hamasa baina ya timu hizo mbili na halikadhalika kuifanya nafasi ya wasemaji ionekane uhai wake. Masau Bwire wa Ruvu Shooting na Thobias Kifaru wa Mtibwa Sugar nao halikadhalika walikoleza ladha ya usemaji wa vilabu.
Mageuzi yalivyozidi katika vilabu ambapo kukaibuka vilabu ambavyo vinamilikiwa na watu binafsi kwa asilimia 100 kukaleta aina mpya ya uendeswaji wa vilabu. Katika uendeshwaji huo wamiliki wengi wakawa hawataki kuwa na wasemaji ambao watakuwa na jina kubwa kuliko taasisi na baadhi yao wakaanza kupunguza bajeti za ofisi za idara ya habari na usemaji wa vilabu hivyo. Wamiliki wengi hupenda majina yao ndio yawe makubwa na sio majina ya wasemaji na huwapunguza nguvu wasemaji hao.
Michezo ambayo imekosa idara za habari ambazo ziko makini imejikuta inakosa ushawishi mongoni mwa wadhamini na halikadhalika hata hamasa ya watu kuhudhuria matukio yao ya michezo nayo imekuwa ni ndogo sana. Mchezo kama ngumi ambapo wamejitokeza baadhi ya mabondia ambao wamekuwa wanaweza kujisemea wenyewe umekuwa una nguvu sana. Bondia kama Karim Said maarufu kama Mandonga na bondia kama Abdallah Pazi maarufu kama Dullah Mbabe wamejiongezea umaarufu na mashabiki kutokana na ubunifu wao wa maneno ya kutia hamasa mashabiki kufuatilia mapambano yao.
Ni wazi kwa sasa suala la idara za habari na hamasa ni lazima taasisi za michezo ziwe nazo na ni lazima zipange bajeti kwa ajili ya idara hizo ili kuendana na soko la sasa la michezo lilivyo. Wamiliki na viongozi wa taasisi za michezo waache kuvinyima bajeti idara hizo kwani kwa kufanya hivyo wanajiumiza wao wenyewe.
Comments
Loading…