INAWEZEKANA napinda kona, lakini naamini niko kwenye mstari. Wiki iliyopita, wakati nikiwa kwenye majukumu ya kupitia habari hizi na zile, nilikutana na habari ya Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania, FAT baadaye TFF, Muhidin Ndolanga akitangaza tarehe ya uchaguzi wa Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam, DRFA.
Kwa Ndolanga atakumbukwa kwa mengi hasa ile siku watu walivyokesha pale Golden Tulip katika uchaguzi wa 2004 wa TFF. Ndolanga ndiye mwenyekiti wa uchaguzi na ndiye aliyetangaza tarehe ya uchaguzi wa DRFA, kuwa utafanyika Oktoba 12.
Swali linakuja. Hii DRFA itakuwa ikifanya kazi gani?
Tunaangalia kwa uchache yaliyomo na kuifanya DRFA kuonekana βsi mali kituβ kwa sasa. Itakumbukwa mwaka 2007 wakati mashindano ya U17 ya Copa Coca Cola, mkoa wa Dar es Salaam uligawanyika katika mikoa ya Ilala, Temeke na Kinondoni, na wakatoa timu zao. Kinondoni ilitwaa ubingwa baada ya kuichapa Ilala mabao 3-1.
Mwaka huu, mashindano hayo hayo, yamefanyika kwa mkoa wa Dar es Salaam kugawanywa katika mikoa ya Ilala, Temeke na Kinondoni na hata vyama vya soka katika maeneo hayo, TEFA, Temeke, KIFA, Kinondoni na IDFA kwa Ilala kupewa majukumu kamili ya kusimamia timu kama ilivyokuwa ikifanya mikoa mingine.
Yakaja mashindano ya Kombe la Taifa. Mkoa wa Dar es Salaam uliokuwa unashikilia ubingwa ukavunjwavunjwa na kuwa katika mikoa mitatu, ya Ilala, Temeke na Kinondoni. Temeke iliondolewa kwa kuingiza wachezaji siyo na kubakia Ilala na Kinondoni.
Katika mashindano hayo, Mikoa ya Kinondoni na Ilala iliingia fainali na Ilala kushinda mabao 5-0. Hiyo inaonyesha kwamba DRFA haikuwa na nafasi kuanzia Copa Coca Cola hata mashindano ya Kombe la Taifa, kwa kuwa kila wilaya ilipewa hadhi ya mkoa, ikapewa na fungu lake la maandalizi.
Sasa ukiangalia hawa jamaa wa DRFA, wanachaguana kwa kipi? Naamini Shirikisho la soka Tanzania, TFF tayari limesharidhia uwepo wa kanda za mkoa wa Dar es Salaam nikiwa na sababu zilezile za Kombe la Taifa na Copa Coca Cola. Huwezi kusema kwamba hiyo ilikuwa kama majaribio, naamini iko hivyo na itaendelea hivyo.
Hii ni sawa na mambo yanayotokea katika maeneo yetu ya kazi kwamba umekuwa unafanya kazi kwa muda mrefu, lakini unaonekana hufai, huambiwi isipokuwa unaona tu mtu unaambatanishwa, umfundishe kazi kesho na keshokutwa mkataba unavunjwa.
Kwanza, kwa Dar es Salaam ya KIFA, TEFA na IDFA kupewa mamlaka kamili itakuwa imeasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua masuala ya soka katika maeneo husika. Imeelezwa kuwa Ilala ndiyo yenye timu nyingi za Ligi Kuu, Kinondoni ina maendeleo katika soka ya madaraja ya chini lakini Temeke iko kimya.
Kwa kuangalia haya, itakuwa changamoto kwa vyama vya soka katika maeneo hayo kuinua soka kwa upande wake. TEFA iko nyuma, lazima ijiulize sababu za kuwa hivyo, kwanini haina timu ya Ligi Kuu na ina maeneo mengi ya viwanja vya michezo.
Nyingine itajiuliza, kwanini hakuna Ligi ya wanawake kama KIFA inavyofanya, wanaweza kujipanga na hata katika kufikia makubaliano fulani, hakuna sababu ya kusubiri kibali cha DRFA, ni wilaya yenyewe kama mkoa kumaliza taratibu zake ali mradi inafuata taratibu.
DRFA ambayo sasa ni kama kibogoyo kwa kuwa vyama vina mamlaka kamili isipokuwa hayataki kuwekwa wazi, wanaweza kubakia kama waratibu tu wa mkoa kisera lakini si kiutendaji, wilaya zinabakia kama watendaji wakuu.
Kwa kuangalia historia, viongozi wa DRFA waliokuwa madarakani, hawakuwa na mipango endelevu ya kuendeleza soka mkoani na badala yake tangu wakati huo kulikuwa na michezo iliyokuwa ikikutanisha timu za wilaya za vijana kama Ilala, IDIYOSA, Temeke, TEDIYOSA na Kinondoni, KIDIYOSA. Hivi vyama ni nguvu za wilaya.
Kila mara DRFA imekuwa ikisubiri mapato ya mechi. Mara nyingi utawakuta viongozi wake wako milangoni Uwanja wa Taifa wakifanya kazi ya kusimamia milango na kuhakikisha fedha zinapatikana nyingi ili na wao wapate fungu lao kubwa. Kama mtu anabisha ajitokeze!
Itakumbukwa pia kulikuwa na mwenyekiti mmoja wa DRFA, (namuhifadhi) alikuwa siku za mechi, mapema tu keshafika lango la nyuma ya jukwaa kuu ambako kingilio chake ni kikubwa, ilifika wakati aligombana hata na waandishi wengi wa habari waliokuwa wanataka kuingia kufanya kazi ya kuripoti akilazimisha walipe.
Hayo yalikuwa ya wakati huo, sasa katika hili la teni pasenti ya geti sina hakika sana kama fedha hizo bado zinakwenda DRFA ama la. Ok, wataingia madarakani hao watakaochaguliwa, kwa hiyo watakuwa wanafanyia nini hizo pasenti tunazoambiwa zinakwenda mkoani?
Kwa upande mwingine, kama viongozi wakiwa wanawaza teni pasenti ya geti, kweli atakuwa na mpango wa kuendeleza soka?
Bado kuna uwanja mpana wa kuangalia historia. Kuna mipango gani ambayo DRFA imeshafanya ama inafanya kwa maendeleo ya soka mkoani? Kuna shule ngapi ama vituo vingapi vya soka ambavyo DRFA imesimamia na vikasimama na hata ikatoka kifua mbele kwamba ni mikono yake?
Katika uandishi wa habari, kuna maneno ambayo tunayaita βpassengersβ kwamba yawepo, yasiwepo neno litaeleweka, sasa hivi ndivyo ilivyo kwa DRFA kwamba ipo, haipo lakini soka katika mikoa-kanda hii mitatu itachezeka. Sasa utasema DRFA kweli wanahitajika kuwepo hapa.
Katika gazeti moja kulikuwa na habari kuanza kwa mizengwe kuelekea kwenye uchaguzi wa DRFA, na siku moja kabla kulikuwa na habari kwamba watu wanategeana kuchukua fomu za uongozi ambazo zinaanzia Sh200,000.
Inawezekana kweli watu wanashindwa kuchukua fomu, pengine kweli inawezekana hawana hizo hela, lakini wenye kuchekecha mambo wanawaza, kweli unawania DRFA ili kufanyike kitu gani wakati TFF yenyewe imeridhia kuwepo na mikoa na ndiyo maana Copa Coca Cola 2007 bingwa ni mkoa wa Kinondoni na Kombe la Taifa 2008 bingwa wake ni Ilala.
Inawezekana vile vile watakaoingia madarakani wakaja na mipango mingine mipya kabisa, ikiwemo kujenga vituo vingi vya soka, viwanja na mengine kwa maendeleo ya soka, lakini kwa historia bado inahukumu na si kwa DRFA pekee.
Kama wangekuwa watu wengine tungekubali lakini kwa watu wetu hawa hawa wanaojiita βwatu wa mpiraβ huku TFF ikizibariki wilaya za mkoa wa Dar es Salaam kuwa mikoa, hatudhani kama kutakuwa na kitakachofanyika zaidi ya kurudi kule kule kwenye pasenti ya geti.
Comments
Loading…