Sifa kubwa ya Yanga ni rekodi yake ya kushinda mechi za ugenini. Yanga wameshinda mechi 6 ugenini katika mashindano ya CAF hali ambayo inawaweka matumbo joto vigogo wa soka Afrika…
JICHO la kiufundi kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika inaonesha kuwa kuna hofu kubwa kwenye mashindano hayo na kwamba hakuna mwenyewe mwenye uhakika wa kunyakua taji hilo. Mjadala unaoendelea kila upande kuanzia kusini mwa Afrika, kaskazini, magharibi na Mashariki kuna kila dalili michuano hii kuchukua sura mpya kuliko misimu iliyopita. TANZANIASPORTS katika tathmini yake imeonesha kuwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndiyo yenye mvuto Zaidi, huku timu mbalimbali zikiwa na wasiwasi juu ya kuibuka kwa umwamba wa vilabu vya Tanzania. Aidha, TANZANIASPORTS inafahamu kuwa katika michuano hiyo zipo timu zinatakiwa kulipa kisasi kutokana na kutolewa katika hatua ya mtoano, makundi na fainali.
KISASI CHA YANGA, SIMBA
Mabingwa wa soka Tanzania, Yanga wana kisasi na timu za Algeria, ambako wamepangwa na CR Belouizdad ya Algeria. Msimu uliopita wa 2022-2023, Yanga walikubalia kipigo cha bao 1-0 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam katika mchezo wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Katika mchezo wa fainali ya pili (marudiano), Yanga walitandaza soka safi nchini Algeria na kuwazaba wenyeji USM Alger kwa bao 1-0 lililofungwa na beki wake wa zamani Djuma Shaban kwa njia ya tuta. Kipigo walichopata USMA bado kinawatia kiwewe timu za kiarabu na kuona timu za Tanzania ni tishio na zinatoa vipigo nje na ndani. Yanga kwenye mashindano hayo waliwahi kuwachapa timu kongwe ya Club Africain ya Tunisia ikiwa nyumbano kwao. Kipigo hicho na kile cha fainali ya pili dhidi ya USMA kimetoa ujumbe kuwa timu za Tanzania sasa zinanyoa na kutembeza vipigo. Kwa maana hiyo Yanga wanaingia kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa wakwa miongoni mwa timu tishio na ikiwa na rekodi nzuri kushinda ugenini. Katika kundi lao Yanga wataungana na CR Belouizdad(Algeria), Madeama (Ghana) na Al Ahly (Misri).
Kwa upande wao Simba watakuwa na kisasi kikwali dhidi ya klabu ya Jwaneng Galax ya Botswana. Mabingwa hao wa zamani wamewahi kutupwa nje katika mashindano ya CAF na klabu hiyo ngeni barani Afrika. Licha ya ushindi wa mabao 2-0 jijini Gaborone, lakini ikaja kukubali kipigo cha mabao 3-1 kwenye dimba la Benjamin Mkapa. Msimu huu Simba wapo katika kundi moja na Jwaneng Galax, Asec Mimosas na Wydad Casablanca. Simba wana kisasi kingine dhidi ya Wydad Casablanca kwani ndiyo timu iliyowatupa nje ya mashindano. Katika mchezo wa kwanza Simba waliibuka na ushindi wa 1-0, kabla ya kukubali kipigo kama hicho nchini Morocco na kusababisha mchezo wao kwenda kwenye hatua ya matuta. Simba walitolewa kwa njia ya matuta na Wydad Casablanca hivyo nao wana kisasi na timu hii. Kwanza Simba wanatakiwa kuwaadabisha Jwaneng Galaxy kwa kipigo kikali, lakini wanatakiwa kuwa waangalifu kwa sababu walishashinda mabao mengi lakini wakashindwa kumalizia mkia kwenye mchezo wa marudiano. Kwa vyovyote vile Jwaneng Galax inafahamu inawindwa na wababe wa Afrika Simba na wanajua kutakuwa na mechi kali hivyo lazima watajiandaa. Jwaneng wataingia wakiwa na uzoefu kidogo kuliko walipokutana na Simba kwa mara ya kwanza.
Wakubwa wanaona aibu
Kufungwa kwa USM Alger na Club Africain kwenye uwanja wa nyumbani msimu uliopita na Yanga ni ujumbe kuwa timu za Tanzania ni moto wa kuotea mbali. TANZANIASPORTS imefuatilia mijadala mbalimbali kuhusiana na makundi ya Ligi ya Mabingwa kwenye kwenye nchi za Morocco na Algeria, Yanga wanasifiwa na kuhofiwa kuwa moja ya timu za kuogopwa. Sifa kubwa ya Yanga ni rekodi yake ya kushinda mechi za ugenini. Yanga wameshinda mechi 6 ugenini katika mashindano ya CAF hali ambayo inawaweka matumbo joto vigogo wa soka Afrika. Nchini Ghana mjadala mkubwa ni Yanga itakapopetana na Medeama, ambapo mashabiki wameingiwa hofu juu ya timu hii.
Simba nao hawako mbali, kwa sababu wanazo rekodi nzuri dhidi ya Wydad Casalanca na Al Ahly. Licha ya kufungwa msimu uliopita katika hatua ya robo fainali, bado Simba ni timu iliyojenga jina kubwa miongoni mwa vigogo, ambako wengi wamekuwa wakihofia timu hiyo. Katika uwanja wake wa nyumba Simba imekuwa ikihakikisha inashinda mechi zote, huku Al Ahly na Wydad zikiwa ni miongoni mwa timu zilizopata vipigo. Kwa msingi huo, ingawa Simba na Al Ahly hawapo kundi moja, lakini ni dhahiri hali ya mambo imekuwa ikiwasumbua vigogo wa soka, na sasa wanaona aibu kukutana na timu hizo. Wanatakiwa kujiandaa mara mbili Zaidi ya miaka ya nyuma kwenye mashindano hayo.
Hasira za mashabiki
Bila shaka yoyote mashabiki wa Simba wana hasira dhidi ya Jwaneng Galaxy, kwahiyo wataweza kujaza uwanja au kuzomea na kufanya mbinu za kuwateteresha wachezaji wa klabu hiyo kwa sababu watataka kulipa kisasi. Hali kadhalika, Yanga washabiki wao watakuwa na hasira la CR Belouizdad kwa vile nayo inatoka Algeria hivyo kisasi cha kukosa kombe la mbele ya USM Alger kitahamia kwa ndugu zao wa Belouizdad.
Comments
Loading…