*Liverpool, Norwich zachanua EPL
*Mancini aitwa na Galatasaray
*Moyes aweweseka na Man U
Mkenya Wilson Kipsang ameweka rekodi mpya ya dunia katika mbio za Marathon kwa ushindi mkubwa nchini Ujerumani.
Kipsang aliongoza msururu wa Wakenya watano waliofanya vizuri kwenye mashindano hayo kwa upande wa wanaume wakichukua tatu bora na wanawake mbili.
Kipsang alikamilisha mbio zake Jumapili hii jijini Berlin kwa kukimbia kwa saa mbili, dakika tatu na sekunde 23.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 31 amevunja rekodi kwa kupunguza sekunde 15 kutoka kwa aliyekuwa akiishikilia, Patrick Makau, naye wa Kenya aliyoiweka mwaka 2011.
Hiyo ni rekodi ya nane ya dunia huko Berlin katika kipindi cha miaka 15, ikijiimarishia hadhi yake kama jukwaa la dunia linalopata mwendo kasi zaidi miongoni mwa washiriki wa mbio ndefu.
Kenya ilizidi kutamba huko Berlin, kwani mwanariadha wake, Eliud Kipchoge alishika nafasi ya pili kwa kukimbia kwa muda wa 2:04:05, akiboresha rekodi yake ya awali kwa saa moja unusu.
Kenya ilizidisha tambo kwani hata nafasi ya tatu ilichukuliwa na raia wake, Geoffrey Kipsang — ambaye hata hivyo hana uhusiano wowote na Wilson na huyo alikimbia kwa muda wa 2:06.26.
Kwa upande wa wanawake, Florence Kiplagat wa Kenya pia alishika nafasi ya kwanza kwa kukimbia kwa muda wa 2:21:13, ikiwa ni dakika moja na nusu zaidi ya rekodi aliyopata kuweka kabla. Mkenya mwingine, Sharon Cherop alikuwa wa pili kwa kukimbia kwa muda wa 2:22:28.
Mjerumani Irina Mikitenko alimaliza akiwa wa tatu ambapo katika umri wake wa miaka 41 aliweka rekodi kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 40 duniani akikimbia kwa muda wa 2:24:54, dakika moja haraka zaidi ya rekodi iliyokuwapo awali.
LIVERPOOL, NORWICH MAMBO SAFI
Liverpool na Norwich zimefanya vyema kwenye mechi zake Jumapili hii kwa kupata ushindi wakitoka kwenye vipigo.
Mabao mawili ya Luis Suarez na moja la Daniel Sturridge yametosha kukoleza moto wa Liverpool na kuzidi kuwaweka pabaya Sunderland ambao hawana kocha.
Akicheza mechi ya pili baada ya kurejea kutoka kwenye adhabu ya kukosa michezo 10, Suarez alifunga mabao mawili katika dakika ya 36 na 89 akiongeza kwenye lile la Sturridge la
dakika ya 28 dhidi ya Sunderland.
Kwa ushindi huo, Liverpool waliokuwa wameanza ligi vyema kuliko timu nyingine yoyote kabla ya kuja kupoteza mechi, sasa wanashika nafasi ya pili wakifungana pointi na Tottenham Hotspur walio nafasi ya tatu kwa upungufu wa mabao ya kufunga.
Sunderland kwa upande mwingine wamebaki mkiani mwa ligi na pointi yao moja kutokana na mechi sita.
Katika mechi nyingine, Norwich wanaofundishwa na Chris Hughton walifanikiwa kupata ushindi wa pili tangu kuanza ligi hii, ambao ulikuwa muhimu kwani umewaondoa kwenye eneo la hatari.
Wakicheza nyumbani kwa Stoke, Norwich walipata bao la mapema katika dakika ya 25 kupitia kwa Jonny Howson na wakalilinda hadi mwisho.
Kocha wa Stoke, Mark Hughes anasema wachezaji wake hawakufanya vizuri na katika ligi kuu asiyefanya vyema huadhibiwa, akasikitikia hali iliyowapata wachezaji wake.
Ushindi wa Norwich umewapandisha hadi nafasi ya 14 wakati Stoke wakiwafuata katika nafasi ya 15 wote wakiwa na pointi saba.
kwa matokeo hayo na mengine ya Jumamosi,
Arsenal wanaendelea kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili huku, nafasi ya nne wakiwapo Chelsea, wakifuatiwa na Southampton, Manchester City, Hull, Everton, Villa, West Brom, Cardiff, Man United, Swansea, Norwich, Stoke, Newcastle, West Ham, wakati tatu za mwisho ni Fulham, Crystal Palace na Sunderland.
MANCINI AELEKEA GALATASARAY
Kocha wa zamani wa Manchester City, Roberto Mancini ameanza mazungumzo na mabingwa wa Uturuki, Galatasaray ili kuchukua nafasi iliyo wazi ya kocha.
Klabu hiyo yenye makao yake makuu jijini Instanbul imethibitisha kwamba Mancini (48) amefanya mazungumzo na wakurugenzi wake, na Mancini mwenyewe alikuwa kwenye picha ya pamoja na Lutfi Aribogan, ikidhaniwa mambo yalikuwa yakienda vizuri.
Kocha huyo Mtaliano hana kazi tangu alipopoteza kibarua chake Man City mwishoni mwa msimu uliopita na anadhaniwa atachukua nafasi ya kocha aliyefukuzwa hapo Galatasaray wiki iliyopita, Fatih Terim. Alifukuzwa baada ya kukataa kuongeza mkataba hata kabla ya alio nao haujaisha.
Galatasaray wameanza vibaya ligi ya nchini Uturuki , wakishinda mechi moja tu kati ya tano walizocheza.
Hata kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Galatasaray walikung’utwa na Real Madrid kwa mabao 6-1. Katika kundi lao wapo pia Juventus na FC Copenhagen.
MOYES AWEWESEKA LIGI YA MABINGWA
Baada ya kupoteza mechi tatu katika Ligi Kuu ya England, Kocha David Moyes wa Manchester United ameeleza wasiwasi wake juu ya timu yake kuweza kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Moyes ametoa maneno hayo muda mfupi baada ya timu yake kugungwa na West Bromwich Albion, ambayo haikutarajiwa kabisa kupata ushindi katika dimba la Old Trafford, maana hawajawahi tangu mwaka 1978.
Moyes alisema kwamba wanahitaji kuwa na wachezaji wenye hadhi kubwa kama watano au sita, akidai kuna klabu nyingine zinao lakini Mashetani Wekundu hawana.
Moyes alichukua nafasi ya Sir Alex Ferguson aliyestaafu mwisho wa msimu uliopita, ambapo Moyes alisusua kufanya usajili na akapata mchezaji mmoja tu, naye ni Marouane Fellaini katika dakika za mwisho za dirisha la usajili.
Moyes alipendekezwa kwa Bodi ya Wakurugenzi wa Manchester United, lakini hata katika mechi za majaribio hakufanya vyema.
Comments
Loading…