Wadhamini wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) wamelikalia kooni shirikisho hilo wakitaka upelelezi wa kina juu ya kashfa za rushwa zinazoliandama.
Fifa wapo katika shinikizo kubwa kwamba wajumbe wake kadhaa walipokea mlungula kutoka kwa Kamati ya Maandalizi ya Qatar ili nchi hiyo iandae michuano ya Kombe la Dunia 2022.
Makamu Rais wa Fifa aliyefukuzwa, Mohammed bin Hammam ndiye anayedaiwa kuweka mkakati na kugawa mamilioni ya dola, tiketi za kushiriki michuano hiyo, suti na kukirimu wajumbe kwenye miji ya kitalii na hoteli za kifahari za Doha.
Wadhamini hao wakubwa ambao ni tegemeo kubwa kwa Fifa katika kuendesha shughuli zake ni
Sony, Adidas, Coca-Cola, Visa na Hyundai/Kia ambao wameutaka uongozi wa Rais Sepp Blatter kushughulikia suala hilo na kupata utatuzi wa kudumu.
Pamekuwa na miito kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali kutaka ama Qatar wapokonywe nafasi hiyo au kura irudiwe lakini taifa hilo dogo la Kiarabu linakana katakata kutoa rushwa kwa namna yoyote.
Hao ni wadhamini watano kati ya sita wa Fifa, abapo walioamua kukaa kando ni Emirates Airline ambao ni mali ya falme hiyo na hawatarajiwi kuingilia kwa vyovyote zaidi ya kuiunga mkono serikali ya nchi yao.
Qatar walichaguliwa Desemba 2010 kuwa wenyeji wa michuano hiyo, wakishinda nchi nyingine zilizotaka kuandaa ambazo ni Australia, Japan, Marekani na Korea Kusini.
Miongoni mwa wanaodaiwa kupewa mlungula huo ni
Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou ambaye amekanusha yeye au wajumbe wa Afrika kupokea rushwa.
Takwimu husika zimepatikana kutokana na kunaswa mawasiliano mbalimbali kati ya Bin Hammam na wajumbe wa mkutano huo wa Fifa, ikiwa ni pamoja na barua pepe.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron amesema angependa nchi yake kuandaa iwapo Qatar watapokonywa, Naibu Waziri Mkuu wa Uingereza, Nick Clegg amependekeza Qatar wavuliwe uenyeji huyo, jambo linaloungwa mkono na Chama cha Soka (FA) cha England.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini aliyeipigia kura Qatar naye anasema ikithibitika rushwa ilitembea lazima kura irudiwe. Wanasheria wa Fifa wanaendelea na kazi ya uchunguzi wa kina.
Comments
Loading…