Wadau wa michezo Ulaya wanaonekana kuzidi kuweweseka, wasiwasi wao ukiwa kuyumba vibaya kifedha kutokana na janga la virusi vya corona linaloonekana kuendelea kung’ata kila uchao.
Kuna tishio katika mwenendo wa wadau, ikiwa ni pamoja na vyama na mashirikisho mbalimbali, yakiwamo yaliyopanga kupeleka wanamichezo kwenye michuano ya mwakani ya Olimpiki.
Vyama mbalimbali vimefichua kwamba vinakabiliwa na tishio kubwa kwa sababu ya janga hili la kimataifa lililosababisha Ubelgiji kufunga moja kwa moja ligi kuu yao na kutawaza mabingwa waliokuwa wanaongoza – Club Bruges waliotofautiana kwa alama 15 na Gent wanaoshika nafasi ya pili.
Wakati Hispania imehirisha La Liga kwa muda usiojulikana, Italia wanatarajia kuanza tena mwishoni mwa mwezi huku England wakikaa Ijumaa hii kujadiliana na klabu kuona hatima ya ligi hii maarufu zaidi iweje.
Vyama zaidi ya 10 vimeeleza hofu yao kwamba vitakuwa katika hali mbaya sana kifedha, kutokana na mechi au mashindano mbalimbali kufutwa au kusogezwa mbele, ikimaanisha kwamba vyanzo mbalimbali vya mapato vimeyeyuka.
Hali ni mbaya kwa sababu bado kuna wajibu wa kulipa wafanyakazi wao, wakati ambao wachezaji wa klabu nyingi wamekuwa hawataki kukubali kukatwa mishahara yao. Ofisa mtendaji mmoja alikiri kwamba katika mchezo wake, wanaweza kupoteza pauni zaidi ya milioni moja katika miezi sita ijayo ikiwa kufungiwa ndani kutaendelea.
Hivi majuzi UK Sport walituma fomu maalumu kwa kila chama kinachoandaa wachezaji wake katika michezo mbalimbali ya Olimpiki ili kubaini wanavyoathirika kifedha kwenye programu zao za kuwania medali kutokana na janga la COVID-19.
Wakuu hao wa michezo nchini Uingereza wanataka kujua wale watakaokuwa katika hali mbaya zaidi na wale wanaoweza kuwa katika mwelekeo wa kufilisika kwenye miezi mitatu ijayo.
Kila taasisi imetakiwa kufanya utaffiti wa kina na kueleza kwa uadilifu na ukweli hali yao kifedha ili kujua hali ya tatizo kama nchi kimichezo kwenye eneo la fedha. Walihojiwa pia ipi ingekuwa athari iwapo tatizo hili lingeendela kwa miezi sita kisha waeleze ni msaada gani kifedha wangehitaji. UK Sports wanasisitiza kwamba bado wangetaka kuwaunga mkono wale wote ambao wana uelekeo wa kuliletea taifa medali kutoka Tokyo.
Mwenendo huu wa Uk Sports unaonekana kupokewa kwa mikono miwili na wadau wengi, huku ofisa mtendaji mkuu mmoja akiwapongeza kwa kuchukua hatua mapema kwa ajili ya kuokoa michezo wakati huu mbaya kabisa usiopata kutokea kabla. Bado kuna wasiwasi kwenye sekta juu ya kupungua sana kwa mapato.
Ofisa mwingine mwandamizi anasema kwamba michezo inakabiliwa na wakati mgumu, kukitakiwa kuletwa uwiano – upande mmoja ikiwa ni jitihada za kujaribu kubaki hai na wneye afya dhidi ya homa hiyo kali ya mapafu. Kwa upande mwingine, ni kutotaka kuonesha kwamba wanadai kupita kiasi wakati huu mgumu ambapo serikali imetaka watu wabaki ndani mwao. Hawataki pia kupoteza michezo au taasisi zao kwa ukata.
“Hili suala ni zito sana na linavyozungukwa pia. Kuna upande wa kuhakikisha Idara ya Afya – NHS – inapewa rasilimali za kutosha kulinda afya za watu walioathirika au karibu nao lakini wakati huo huo tunataka kueneleza michezo na kwa hakika tunakuwa na wakati mgumu sana kurudia hali ya kawaida bila kuungwa mkono na walio juu,” akasema ofisa huyo.
Kwa kawaida vyama na mashirika ya michezo hupata sehemu ya fedha zao kutoka UK Sports ambao wametoa pauni milioni 374 kwa Chama cha Olimpiki na Chama cha Olimpiki ya Walemavu katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Walau hao hawafikiriwi kuwa katika hali mbaya sana.
Hata hivyo, michezo mingine na vyama vyao watakuwa katika hali mbaya zaidi na hiyo ni kama vile mbio za baiskeli, badminton, riadha, soka na mingineyo wana hali ngumu kwa sababu wamekuwa wakitegemea zaidi fedha zitokanazo na mapato ya televisheni, matukio yanayoitishwa, ada za uanachama na udhamini. Sehemu kubwa ya mapato hayo hayatapatikana ikiwa kutakuwapo mwendelezo wa kufungwa kwa shughuli za umma, ikiwamo michezo.
Ofisa mtendaji mkuu mmoja alisema matarajio yake ni kwamba michezo haitarejea katika hali ya kawaida hadi walau Septemba mwaka huu, akisema kwamba kuna shinikizo la nyongeza kwa sababu ya soko la udhamini wa Olimpiki na Olimpiki kwa Walemavu ambalo anasema halina nguvu kwa sasa.
Taasisi nyingine, kama Chama cha Riadha England na kile cha Uskochi – vinaelezwa kuwa na masikitiko kutokana na kushuka kwa ada ya uanachama kutoka kwa wanariadha wasiopweza kutumia miundombinu ya kwenye klabu zao kutokana na amri ya kila mtu kukaa na kujifungia nyumbani kwao.
Kadhalika bado haijajulikana iwapo vyama na mashirika ya michezo yanayopata fedha serikalini yangeweza kuendelea kuwalipa wafanyakazi wao au kuwaingiza kwenye program ambayo serikali hutoa kiasi kama fidia wakati wa hali kama hii isiyokuwa ya kawaida na yenye hasara kwao kimapato.