*Schneiderlin agoma kucheza Southampton
*Didier Drogba astaafu kucheza Ivory Coast
Arsenal wamepokea na kukubali ofa ya pauni milioni 15 kutoka Barcelona kwa ajili ya kumuuza nahodha wao, Thomas Vermaelen (28) aliyekuwa akitafutwa pia na Manchester United kuziba pengo kwenye beki ya kati.
Mchakato unaoendelea sasa ni kwa Vermaelen kuelewana na Barcelona juu ya stahili zake binafsi kama mshahara na posho nyingine na pia kuchukuliwa vipimo vya afya na wakikubaliana atatia saini rasmi kuondoka Emirates.
Man United waliacha kumfuatilia Mbelgiji huyo ambaye kwa sasa ni majeruhi baada ya Arsenal kutaka wabadilishane na mchezaji mwingine kutoka Old Trafford. Kadhalika kocha Arsene Wenger alikuwa amesema angependa kumuuza ng’ambo kuliko kwa timu ambayo ni washindani wao kwenye ligi kuu.
Kuondoka kwake kutakuwa mwisho wa safari yake ya miaka mitano London Kaskazini na Arsenal watakuwa wanatafuta nahodha mwingine. Alijiunga hapo akitoka Ajax kwa ada ya pauni milioni 10 na amecheza mechi 150 katika mashindano yote.
Hata hivyo, Vermaelen hakucheza mechi nyingi msimu uliopita baada ya kiwango chake kushuka na wakati mwingine akiwa majeruhi. Wenger pia alipendelea zaidi upili wa mabeki wengine wa kati, Laurent Konscielny wa Ufaransa na Per Metersacker.
Vermaelen anaweza kuwa beki wa pili wa kati kusajiliwa Barcelona baada ya yule wa Valencia, Jeremy Mathieu, wa kwanza kusajiliwa kwa ajili ya nafasi hiyo klabuni Barca tangu 2009.
MORGAN SCHNEIDERLIN AGOMA KUCHEZA SOUTHAMPTON
Masahibu yanazidi kuwapata Southampton, baada ya mchezaji nyota zaidi aliyebaki baada ya wengine kuuzwa, Morgan Schneiderlin kusema hawezi kucheza hapo kwa sasa.
Mfaransa huyo ameiambia klabu kwamba hayupo vyema kisaikolojia wala kiakili kucheza. Alikuwa anawindwa na Arsenal na Tottenham Hotspur kuimarisha maeneo ya kiungo, lakini klabu imekwua ikisema hauzwi.
Hiyo ni baada ya kuuza nyota wake watano kwa Arsenal, Liverpool na Manchester United na kulalamikiwa sana na washabiki na wadau wao, kwa sababu inaelekea kana kwamba klabu inasambaratika.
Schneiderlin (24) amepata kupewa onyo na kocha wake, Ronald Koeman baada ya kuandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba kazi kubwa iliyofanywa kuijenga Southampton imebomolewa kwa siku chache tu.
Koeman sasa amempa mapumziko ya siku mbili kwa ajili ya kutafakari hatima yake. Habari hizi zinakuja wakati mlinzi wa timu hiyo, Jose Fonte amekubali kuhuisha mkataba wake hadi 2017 na ametajwa kuwa nahodha kwa msimu ujao.
DROGBA AACHANA NA SOKA YA KIMATAIFA
Mchezaji mkongwe wa Ivory Coast, Didier Drogba ametangaza kujiuzulu kuchezea timu ya taifa hilo la Afrika Magharibi.
Drogba (36) alikuwa akidhaniwa kuondoka kwenye timu hiyo kutokana na umri wake huo, baada ya kucheza hapo mara 104 na kufunga mabao 65 katika kipindi cha zaidi ya miaka 12.
Mshambuliaji huyo wa kati amerejea Chelsea baada ya kuchezea Galatasaray ya Urusi kwa msimu mmoja. Baada ya kuondoka Chelsea 2012 alijiunga na klabu ya China ya Shanghai Shenhua. Amejaza mkataba wa mwaka mmoja Stamford.
Drogba amesema anaona fahari kuchezea taifa lake kwa muda wote huo na kuwa nahodha kwa miaka minane, akiipandisha nchi hiyo juu katika soka ya kimataifa na sasa ni nafasi ya kuachia wadogo. Amesema anatumaini uamuzi huo utamsaidia kuelekeza vyema nguvu zake kwenye ligi kuu baada ya kukosekana England kwa miaka miwili hivi.
Comments
Loading…