in , , ,

UZEMBE UNAPOMSHIKISHA SINGANO MAMILIONI YA LEWANDOWSKI

Januari 2014 Robert Lewandowski alisaini mkataba wa kuhamia Bayern Munich kwa uhamisho huru. Baada ya msimu wa mwaka huo kumalizika akahamia rasmi Bayern kama mchezaji huru akitokea Dortmund.

Dortmund walikuwa mamekula hasara kwani hawakupokea hata senti kwenye uhamisho huo kwa kuwa Lewandowski alikuwa amemaliza mkataba nao.

Kocha Jurgen Klopp na bodi ya klabu ya Dortmund hawakupenda hili li litokee. Ila swala lenyewe lilikuwa nje ya uwezo wao. Awali waligoma kumuuza mchezaji huyo kwenda Bayern kwa kuwa walikuwa wameshapoteza nyota wao kadhaa akiwemo Kagawa na Mario Gotze.

Mapema 2013 Dortmund ilijaribu kumshawishi Lewandowski arefushe mkataba wake ambao ulikuwa unaishia Juni 2014. Juhudi hizo ziligonga mwamba kwani Lewandowski aligoma akishinikiza kuhamia Bayern. Mwishoni mwa msimu wa 2012/13 walikataa kumuuza kwa kuwa bado walihitaji huduma yake.

Wakawa tayari kupata hasara na wakaipata baada ya Lewandowski kuhamia Bayern kwa uhamisho huru mkataba wake ulipomalizika Juni 2014.

Sababu zinazopelekea mchezaji kuachwa huru na klabu yake kwenye soka la Ulaya ni pale klabu yake aliyoichezea inapokuwa haimuhitaji tena anaposhuka kiwango au/na kuwa na umri mkubwa. Miroslav Klose alihamia Lazio kwa uhamisho huru akitokea Bayern Munich 2011 mkataba wake na Bayern ulipomalizika.

Hakuwa akihitajika tena Bayern. Hakuwa tena na chochote cha kuwashawishi Bayern wambakize Allianz Arena kwa kuwa tayari alikuwa na miaka 33 na kulikuwa na washambuliaji vijana mahiri kama Mario Gomez na Thomas Muller. Mtazame pia Kevin Davies. Alisajiliwa na Bolton kama mchezaji huru baada ya Southampton kumtema kwa kuwa kiwango chake kiliporomoka.

Kwa Singano hali imekuwa tofauti kwenye soka la hapa nyumbani. Wiki chache zilizopita alihamia Azam FC kama mchezaji huru kwa dau la shilingi milioni 50 huku akilipwa mshahara wa shilingi milioni 2 kwa mwezi.

Mchezaji mahiri na mwenye umri mdogo anahama kwa uhamisho huru huku klabu yake ya awali Simba SC ikiwa bado inamuhitaji. Tumeshindwa kuiga namna ya klabu za Ulaya zinavyoendeshwa. Namna wanavyoweza kutawala mikataba ya wachezaji. Hili ni tatizo kubwa kwetu.

Singano
Singano

Simba SC ilishindwa kutawala mkataba wa mchezaji huyo na kupelekea kudhuru maslahi ya klabu. Ni uzembe kuacha kurefusha mkataba wa mchezaji mapema kabla ya msimu wa mwisho wa mkataba wa mchezaji ikiwa klabu bado inamuhitaji. Inasemekana Simba waligushi mkataba.

Walishindwa nini kurefusha mkataba wa mchezaji huyo mapema ili kulinda maslahi ya klabu? Ulaya mikataba ya wachezaji mahiri hurefushwa mapema mno kiasi cha hata misimu miwili kabla ya kufikia mwishoni. Real Madrid Septemba 2013 ilirefusha mkataba wa Christiano Ronaldo ambapo sasa utamalizika 2018. Mkataba wake wa awali ungemalizika 2015.

Kwa uwezo wa Ronaldo, thamani yake na jinsi anavyohitajika Bernabeu mkataba wake ukarefushwa mapema. Barcelona pia walifanya kama hivyo kwenye mkataba Lionel Messi Mei 2014.

Ni mara chache mno mchezaji mahiri anapohama kama mchezaji huru kwenye soka la Ulaya. Mfano Robert Lewandowski alipohamia Bayern Munich. Swala la Lewandowski kama nilivyolichambua hapo juu lilikuwa tofauti kidogo.

Dortmund walijikuta wanakosa la kufanya baada ya Lewandowski kugoma kurefusha mkataba akishinikiza kuhama. Lewandowski alihamia Bayern kwa uhamisho huru na kutia mfukoni pesa kibao za miamba hiyo ya Ujerumani. Kwa Singano kulikuwa na uwezekano wa kurefusha mkataba wake mapema.

Siamini kuwa swala hilo lilikuwa nje ya uwezo wa Simba SC. Ila uzembe na ujanja ujanja umeifanya Simba kushindwa kutawala mkataba wa Singano na hatimaye imekula hasara.Kutokana na uzembe na ujanja ujanja Singano anatia mfukoni pesa za Lewandowski.

[email protected]

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Delph atua Man City

Arsenal wachukua Barclays