UZOEFU wa mtu katika shughuli zozote za kiutawala una mchango wake. Uongozi wa Taasisi yoyote lazima ufanye mambo yake kwa utulivu hata kama wanakuwa kwenye mawimbi makali ya kiutendaji na uendeshaji. Mchezo wa soka unahitaji sana ustahimilivu na kudhibiti kila wimbi linalotikisa vilabu duniani. TANZANIASPORTS inaunga mkono mafunzo ya uongozi wa michezo au Soka kote duniani unaofanywa na Shirikisho la Soka la Dunia, FIFA. FIFA Kwa kutambua umuhimu huo ndiyo maana inaendesha warsha na mafunzo sehemu mbalimbali.
Mathalani ninaishi katika nchi ambayo ina mafanikio makubwa ya mpira wa miguu ikiwemo kunyakua Kombe la Dunia. Jiji kama London lina timu kali kama vile Arsenal, na Chelsea. Pia Tottenham Hotspur F.C. Inayopitia kipindi kigumu kwa sasa. Hizo ni timu zilizopita vipindi vigumu lakini uongozi haukuwa wa papara na kukosa ustahimilivu. Imani wanayokuwa nao viongozi ndiyo chachu ya mashabiki kuendelea kuunga mkono timu zao.
Tukirudi nyumbani Tanzania, klabu ya Yanga ina historia kubwa na maarufu nchini. Katika miezi kadhaa mashabiki wa Yanga wamepunguzwa Imani sababu ya uamuzi unaochukuliwa na viongozi. Kwa mwenendo walioanza nao, ulikuwa muhimu na ulipewa Kila aina ya pongezi baada ya mafanikio kadhaa. Hata hivyo uongozi huo ghafla umetumbukia katika njia ya Manchester United ambao wamekuwa wakihaha kuiweka sawa klabu yao. Yanga si kama Manchester United katika hali ya maendeleo ya kimpira lakini zote ni Taasisi za soka zenye heshima.
Ukiwatazama mashabiki wa Yanga na matamshi yao Kila mara timu ilipocheza ni dhahiri Ile Imani waliyokuwa wamejengewa imepungua. Sababu za kupungua ni hali ya mambo ikiwemo kutimuliwa Miguel Gamondi. Mashabiki walimpenda, walimwamini na kuamini yeye ndiye anaweza kuwapa furaha zaidi.
Hata hivyo maisha ya Soka yanabadilika, na uongozi ukamwajiri Sead Ramovic. Kazi kubwa ya kwanza ya uongozi ilikuwa kuwaaminisha mashabiki na wanachama wao kuwa Ramovic alikuwa chaguo sahihi. Hali kadhalika Ramovic alikuwa na kibarua cha kutakiwa kuonesha thamani yake kuwazidi watangulizi wake Gamondi na Nabi au kuendeleza mafanikio Yale. Imani ya wanachama na washabiki haiwezi Kuja kirahisi ndiyo maana Sead Ramovic alilazimika kuondoka pale alipopata ofa ya klabu ya Algeria, Belouzdad. Hatujui kama ni Ramovic alipeleka maombi ya kazi Algeria au Belouzdad walileta maombi hayo. Propaganda kwenye mpira huwa inafanya kazi kwahiyo habari tuliyonayo ni kwamba Belouzdad waliweka mezani Dola 40,000 kwa mwezi.
Kufika hatua hiyo unaona dhahiri hali ya Yanga na uongozi wake inapoteza utulivu. Yanga walishamwonesha Dunia Sead Ramovic ambaye alikuwa klabuni hapo kwa siku 82 tu. Bila shaka Sead Ramovic alikuwa hajiamini Tena na alijua kuna mlima mrefu kuwapa furaha Wana Yanga.
Hivi sasa Yanga wana kocha mpya akitokea Singida Black Stars. Katika mazingira hayo, maelfu ya mashabiki na wanachama wanakuwa wamwchanganyikiwa huku kocha mpya anakuwa na deni kubwa ambalo linahitaji muda kuwavuta wana Yanga. Timu hiyo imezoea shangwe lakini ujio wa makocha na kubadilisha badilisha mifumo kila mara inawagharimu wachezaji pia.
Wakati Yanga wakiajiri kocha mpya wakanikumbusha ajira ya kocha Ruben Amorim wa Manchester United. Wakati Ruben Amorim akiajiriwa aliambiwa lazima ajiunge na klabu hiyo mapema badala ya mwezi Julai. Wenyewe wana msemo wao kuwa “now or never”. Ilikuwa fursa inayoonesha wazi kulikuwa na papara katika ajira yake. Manchester United walifanya hivyo wakati wakiwa na kaimu kocha mkuu Ruud van Nistelrooy.
Ni kama ilivyo Yanga walivyoajiri kocha mpya nao wamepita njia ileile ya papara, wakati wanaye kocha Abdulhalim Moalin. Moalin ana uzoefu na Ligi Kuu Tanzania akiwa amezifindisha Azam Fc na KMC ya Kinondoni.
“Kwa wakati huu timu angeachiwa Kocha Moalin amalize nayo ligi, kama kulikuwa na plan za kocha mpya, viongozi wangechukua kidogo angalau wawe na machaguo mengi ya kocha yupi anafaa kuja kufundisha mpira. Huyu kocha wa sasa wa Yanga ni kama kaja kutubomolea msingi anaanza ujenzi upya. Yanga haikuhitaji msingi mpya, kwani Ina wachezaji wengi Wazuri,” amesema kocha mmoja ambaye amewahi kuinoa klabu ya Yanga.
Matokeo ya papara za uongozi wa Yanga unakuja pale wanachama na washabiki wanapolazimika kuanza upya kumwamini kocha. Angalau Moalin angaweza kuwavutia kiimani na kifalsafa kuliko kocha mpya ambaye amekuja kuanza upya maisha ya klabu ya Yanga. Katika mazingira hayo, wachezaji wanakuwa hawaelewi msingi wa kwanza wa Klabu kwani Kila mara wanabadilishiwa kocha. Msimu huu wanafundishwa na kocha wa tatu kuliko watani wao wa jadi Simba ambao wametulia na kocha wao Fadlu Davids. Haina maana Kwamba matokeo mabaya yangekuwepo wangetulia naye, lakini kikosi Chao kimetulizwa sababu hawana papara katika ajira ya Walimu.
Ni muhimu viongozi wa Yanga wasije kurudia makosa haya wakati mwingine. Ni muhimu kuchukua Manchester United kama shamba darasa lao katika uendeshaji wa makosa hususani ajira za makocha.
Comments
Loading…