Unai Emery anafahamika kama bingwa mara nne wa Kombe la Europa League akiwa na Sevilla na baadaye Villareal.
LIGI KUU England imemalizika. Wenye kucheka wamecheka, wenye huzuni wamehuzunika, lakini wenye matumaini nao wapo. Mabingwa wanajulikana pamoja na wawakilishi wa mashindano ya kimataifa kutoka England. Makocha ndiyo wenye kuumizwa na vichwa namna watakavyorejea msimu mpya wa 2023/2024.
Kila msimu unakuwa na rekodi za aina yake, na kuwaachia mashabiki na mshangao. Miongoni mwa timu ambazo zimeleta mshangao ni Aston Villa. Hii ni klabu kongwe katika Ligi Kuu England. Ni timu ambayo ina historia kuwa miongoni mwa miamba barani Ulaya.
Aston Villa walianza msimu 2022/2023 wakiwa na kocha wao mzawa Steven Gerrard. Kocha huyo ni nyota wa zamani wa Liverpool, alijiunga na Aston Villa akitokea Ligi Kuu Scotland ambako alikuwa na mafanikio mazuri.
Gerrard alifuata nyayo za kocha wake wa zamani Brendan Rodgers ambaye aliamua kurejea Ligi Kuu England kwa kujiunga na Leicester City lakini baada ya misimu kadhaa alitumuliwa klabuni. Steven Gerrard naye alikuwa na matumaini makubwa tangu alipojiunga na Aston Villa lakini mambo hayakumwendea vizuri.
Uongozi wa Aston Villa ukaamua kumfukuza kazi na kumwajiri Unai Emery. Ajira ya Unai Emery ilikuwa na maana kubwa kwake kwa kurejea EPL kwa mara ya pili baada ya kuchemsha akiwa Arsenal.
Unai Emery anafahamika kama bingwa mara nne wa Kombe la Europa League akiwa na Sevilla na baadaye Villareal. Ni kocha wa makombe la Europa League lakini hakufua dafu alipokuwa akinoa Arsenal kabla ya kufukuzwa.
Lakini ujio wa pili EPL ulikuwa na maana nyingine kwa Unai Emery. Alijiunga na timu ambayo ilikuwa inahangaika kuepuka kuwa miongoni mwa zitakazoshuka daraja. Aston Villa ilikuwa inashikilia nafasi ya 14 katika msimamo wa EPL wakati Unai Emery alipoichukua.
Hapakuwa na matarajio makubwa kutoka kwa Unai Emery zaidi ya kuongoza timu hiyo isishuke daraja. Pengine wengi waliamini timu hiyo ingekuwa inapigania kubaki EPL. Hata hivyo imewashangaza wengi kwa mafanikio aliyopata Unai Emery.
Kocha huyo aliibadilisha kabisa Aston Villa na hivi leo imekuwa timu yenye kuwajaza mataumaini makubwa mashabiki wake na wapenzi wa mpira wa miguu. Kama nilivyoeleza mwanzoni, wakati Unai Emery anachukua kibarua cha kufundisha Aston Villa ilikuwa nafasi ya 14 katika msimamo wa EPL.
Nafasi hiyo ilikuwa na maana Aston vIlla walikuwa wanapigania kutofika eneo la hatari la timu zinazoshuka daraja. Hata hivyo mabadiliko yaliyotokea kwa Aston Villa yameleta habari nyingine kabisa kwa wapenzi wa soka.
Aston Villa imerudi katika mashindano ya Ulaya ambako ilikuwa imepoteana kabisa. Rekodi zinaonesha kuwa Aston Villa ilishiriki mashindano ya Ulaya mara ya mwisho mwaka 2010. Kwa maana hiyo Aston Villa imehangaika kwa kipindi cha miaka 13 kujaribu kufurukuta kuwakilisha England kwenye mashindano ya Ulaya.
Wakati msimu huu 2022/2023 umemalizika wikiendi iliyopita, Aston Villa wamemaliza kwa kushika nafasi ya 7 ya msimamo wa EPL. Kwa kushika nafasi hiyo ina maana msimu ujao 2023/2024 Aston Villa itakuwa miongoni mwa timu zinazowakilisha EPL kwenye mashindano ya Ulaya.
Manchester City, Arsenal, Manchester United na Newcastle United zote zitawakilisha kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa. Wakati Brighton na Liverpool zitawakilisha kwenye mashindano ya Europa League. Aston Villa watawakilisha kwenye mashindano ya Conference League.
Huu unaweza kuwa msimu wenye mafanikio na bila shaka viongozi wa Aston Villa wanakiri kuwa uamuzi wao kumwajiri Unai Emery pengine ulichelewa kwani wangeweza hata kushiriki Europa League msimu ujao.
Aston Villa watakuwa na matumaini makubwa kutoka kwa Unai Emery kwa vile yeye ni kocha wa makombe ya Ulaya hasa Europa League, hivyo kombe la Conference League haitakuwa tatizo kwake.
Kwanza mashabiki watapata burudani ya ziada kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Villla Park. Pili klabu yenyewe ina uhakika wa kuongeza mapato yao kupitia mashindano ya Conference League. Vilevile wachezaji wana uhakika wa kupata bonus kutokana na mafanikio hayo pamoja na ushiriki kwenye Conference League.
Ni dhahiri kuwa Unai Emery amekuwa lulu si kwa Aston Villa peke yao, bali hata timu zile zinazohangaika angalau kufuzu mashindano ya Europa League au Conference League, ambapo zingetamani kupata huduma ya kocha huyo.
Kuirudisha Aston Villa kwenye mashindano ya Ulaya kunairejeshea heshima waliyojijengea miaka 1980 na 1990 ambako ilikuwa miongoni mwa timu kabambe EPL. Walikuwa timu yenye ushindani na ubora. Pengine kufuzu ni hatua ya juu, hivyo mabosi wa Aston Villa hawatarajii kuona kocha huyo akinyanyua kwapa za kutwaa Conference League, lakini wanatamani kuona timu yao ikiwa bingwa.
Kwa kuongeza usajili na namna Unai Emery anavyoweza kuwavutia wachezaji wazuri ndicho kitu cha kwanza ambacho wanaweza kukifanya kwa ajili ya kuimarisha timu yao. Swali linalobaki sasa, ni namna gani makombe aliyotwaa Unai Emery kule Sevilla na Villareal yataweza kumiminika Aston Villa? Je mafanikio hayo yanawezekana na ataifikisha hatua gani timu hiyo? Hayo na mengine yanasubiriwa kwa hamu. Unai Emery apewe maua yake angali hai. Kila kocha anapenda sifa hizo na kupewa maua yake. Nao wachezaji wanapenda sifa zao, hivyo wapewe maua yao.
Comments
Loading…