Kuanzia mwezi mei katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania huwa kunakuwa na taratibu za kuanza mashindano ya Umiseta katika kanda za wilaya na hatimaye mikoa. Na huwa zinatanguliwa na Umitashumta kabla hazijaanza UMISETA. Hakika hakuna mashindano ya makubwa na ya mda mrefu yanayowahusisha vijana wadogo katika nchi ya Tanzania kama hayo. Mashindano hayo huwa yako chini ya ofisi ya raisi tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) ambayo ndio huwa inaratibu mashindano hayo katika ngazi zote. Michezo mbalimbali huchezwa katika mashindano haya kama vile: soka, mpira wa pete, volleyball, basketball, riadha, michezo ya jadi, michezo ya walemavu,tenisi ya meza na mengineyo.
Hakuna mashindano makubwa ya vijana katika taifa la Tanzania makubwa kuyazidi mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA kwani mashindani hayo hukusanya wanamichezo kuanzia wachezaji, makocha, marefarii na maafisa michezo kutoka kila pande za nchi na kukusanyika katika mkoa mmoja ambapo huenda na kucheza michezo tofauti katika siku ambazo zimepangwa mashindano hayo yachezwe.mashindano hayo huwa yana msisimko kwa wanafunzi ambao huwa wanacheza na baadhi yao huwa kumbukumbu za matukio katika mashindano hayo hudumu kwa miaka mingi katika vichwa vyao. Katika siku za huko nyuma mashindano hayo yalikuwa yana mvuto mkubwa sana na katika miaka ya kati msisimko ulipungua na kuna mda yalikuwa hayachezwi na baada ya miaka kadhaa yalirudishwa tena na wakati yamerudishwa msisimko wake ulikuwa umepungua kidogo kutokana na kwamba yalikuwa hayajachezwa kwa miaka kadhaa. Katika ngazi za mikoa mashindano haya huwa chini ya kamati za michezo za mikoa na katika ngazi za wilaya mashindano hayo maandalizi yake huwa chini ya kamati za mashindano za wilaya. Kamati hizi ndizo ambazo huratibu maandalizi yote ushiriki kuanzia kwenye ngazi za kata mpaka kitaifa. Mikoa ambayo hufanya vizuri katika mashindano haya huwa maa nyingi ina uongozi mzuri na ulio na mipango endelevu katika kamati zake za michezo. Halikadhalika mikoa ambayo huwa haifayi vizuri sana basi kamati zake za michezo huwa sio imara sana.
Katika miaka ya huko nyuma ambapo taifa letu lilikuwa katika mfumo wa ujamaa mashindano kama haya yalikuwa yana lengo kubwa la kujenga uzalendo na yalikuwa hayana mitazamo ya kibiashara. Kwa sasa nchi mfumo wa soko huria ndio ulio kwenye hatamu na kwa hivyo hata sekta ya michezo nayo imeanza kufuata kanuni za soko huria hivyo basi mashindano kama haya yanatakiwa yajipange upya ili kuendana na wakati kwani kwa sasa michezo nayo imekuwa ni biashara na ni bidhaa kama zilivyo bidhaa zingine kwa hiyo inatakiwa iwe yenye kuuzika na hivyo kuzalisha vipato na hatimaye kuzalisha ajira za kudumu na za mda mfupi. Ili kuelekea huko kamati za mashindano za mikoa zinatakiwa zifanye mambo yafuatayo:
1. Kuchagua watu sahihi kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo. Kamati za michezo zinatakiwa ziandae mchakato wa kuchagua watu sahihi wenye vigezo vya kuendesha mashindano ya kuchagua wachezaji kwenye ngazi za wilaya mpaka mkoa. Kuna malalamiko mengi kutoka kwa wadau mbalimbali kwamba katika ngazi za kata na tarafa huwa ni watu ambao weledi wao ni mdogo na wachezaji mara nyingi huchaguliwa kwa matakwa yao na wala sio kwa uweledi wa kimichezo. Makocha wa timu za wilaya na mikoa nao halikadhalika wamekuwa wanachaguliwa watu ambao wako karibu na maafisa michezo wilaya na hii kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wanalalamikiwa kwamba wanasababisha mikoa isifanye vizuri katika mashindano ya kitaifa.
2. Kuchagua michezo sahihi kwa ajili ya kushiriki mashindano hayo. Kamati za michezo za mikoa zinatakiwa ziangalie kwa mazingira waliyonayo ni michezo ipi ambayo inayofaa kushiriki na ipi wanaweza kujiandaa vizui ili wapate matokeo mazuri katika mashindano ya kitaifa.
3. Kutafuta udhamini wa vyombo vya habari katika mashindano hayo. Kamati za mashindano za mikoa zinatakiwa zitafute vyombo vya habari vya mitandaoni ambavyo viko katika mikoa yao. Vyombo hivyo vinatakiwa viwe vinaripoti habari za mashindano kuanzia wilaya mpaka mikoa na katika vyombo hivyo watoe taarifa za wanamichezo ambao wanafanya vizuri kwenye vyombo vyao kwa ajili ya kuwabidhaisha(brand). Taarifa hizo ambazo zitakuwa zinatolewa zitasaidia hata wanamichezo hao kujulikana Zaidi na zaidi.
4. Kualika vilabu vya michezo kuangalia wachezaji. Kwa michezo ambayo tayari imeshaanza kuwa ya kulipwa kama vile soka. Kamati za mashindano za mikoa zinatakiwa zitangaze kwamba wachezaji waliwepo katika vikosi vya timu zao za mkoa kwa ajili ya kuangalia namna ya kuwasajili ili kuwaendeleza.
5. Kuwaalika mawakala wa wachezaji kutafuta wachezaji wanaochipukia. Mawakala wa wachezaji wanatakiwa wawepo ili kuangalia vipaji ambavyo wanavyoweza kuingia navyo mikataba ili huko mbeleni kufanya nao kazi. Mawakala watasaidia pia kutoa uzoefu kuwa ni wachezaji gani wana dalili ya kuja kuwa wachezaji wakubwa katika siku za huko mbeleni.
6. Kuwaandaa kisaikolojia wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo kufanya vizuri na hata baada ya mashindano kuendelea kujiweka vizuri. Kunahitajika kuwa na semina fupi za mazungumzo na wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo katika ngazi tofauti ili wajue kwamba fursa hiyo ni kubwa sana na fursa hiyo inaweza kuwafanya waonekane na kupata fursa kubwa Zaidi katika michezo kwa hiyo wanatakiwa wajitume kwa nguvu kubwa sana. Na pia zifanyike semina za kutuliza akili zao baada ya mashindano ili waweze kujitunza na pia kujiweka sawa kiakili ili waweze kushiriki mashindano mengine makubwa huko siku za usoni.
Comments
Loading…