Jumamosi hii ni siku kubwa katika soka kwani miamba wa Hispania, Real Madrid na Atletico Madrid wanavaana kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
Ni historia ya aina yake, kwani zinakutana timu kutoka jiji moja. Atletico wanaingia kwenye hatua muhimu baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Hispania, ikiziacha Barcelona na Real chini yao.
Wakati Diego Simeone akijaribu kukuza wasifu wake zaidi baada ya kuwabomoa Chelsea kwao katika hatua ya nusu fainali. Kwa upande mwingine, Carlo Ancelloti atataka kulinda heshima yake na Los Blancos kwa kuwavisha taji la Ulaya ambalo miaka iliyopita halikuwapa shida kulitwaa.
Atletico watakuwa na hofu kama watakuwa na Diego Costa aliyewasaidia upachikaji mabao, kwani ametokea kuwa majeruhi mara kwa mara.
Hata hivyo wanaweza bado kujidai kwani walipowaaibisha Barca na kutwaa ubingwa wa La Liga hawakuwa naye; aliumia awali. Real wanatamba kwa nyota wao, Cristiano Ronaldo, Gareth Bale walio ghali kuliko timu nzima ya Atletico na wachezaji wengine wengi wazoefu kimataifa.
Mwaka jana fainali ya UCL ilikuwa ya timu za nchi moja – Bayern Munich na Borussia Dortmund za Ujerumani. Bayern walitwaa kombe kabla ya kuvuliwa ubingwa na Real msimu huu kwenye nusu fainali. Kabla ya kutwaa taji Bayern walifungwa kwa mikwaju ya penati na Chelsea katika fainali iliyofanyika kwenye dimba lao la Allianz Arena, Ujerumani.
Comments
Loading…