Robo fainali ya kwanza kwa michuano ya mwaka huu ya Kombe la Dunia imemalizika kwa Ujerumani kuwafungisha virago Ufaransa.
Bao la mapema la Mats Hummel lilitosha kuwavurugia mwanzo mzuri vijana wa Didier Deschamps ambao walitandaza soka zuri muda wote.
Bao hilo lilitokana na rafu ya Paul Pogba iliyozaa mpira wa adhabu ndogo, kisha mabeki wa Ufaransa wakazubaa kuuwahi angani, akiwamo Rafael Varane.
Hummel anayetafutwa kwa udi na uvumba na Manchester United kutoka Borussia Dortmund alitumia wasaa huo, dakika ya 12, kumtungua kipa Hugo Lloris anayekipiga Tottenham Hotspur.
Ujerumani walicheza kwa kujilinda vyema na kutawala kiungo ambapo waliokoa mipira mingi ambayo akina Karim Benzema, Mathieu Valbuena, Patrice Evra, Blaisie Matuidi na wengine waliyoelekeza kwao.
Ufaransa walianza kipindi cha pili kwa kasi kubwa lakini umaliziaji ulikuwa tatizo, kwani hata walipofanikiwa kuwapita mabeki, kipa Manuel Neuer alikuwa kikwazo kikubwa.
Sekunde chache kabla ya mchezo kumalizika Benzema nusura afunge baada ya Wafaransa kugongeana, lakini Neuer tena alipangua kwa kuugonga tu mpira huo.
Joachim Low, kocha wa Ufaransa, amefanikiwa kuwaingiza Wajerumani nusu fainali, wakiweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufika hatua hiyo katika fainali nne mfululizo.
Ushindi huo umekuwa faraja kwa Wajerumani ambao walitoa taarifa kwamba wachezaji wake saba walikuwa wanaumwa, baada ya kushambuliwa na homa na mafua.
Deschamps alikuwa amesema kabla kwamba anawahofia Wajerumani kwamba wangewagonga kwa vile wana uzoefu mkubwa wa mechi kubwa kuliko wao. Baada ya mechi Antoine Griezman wa Ufaransa aliishia kulia kama mtoto mdogo na kubembelezwa na wenzake.
Comments
Loading…