in , ,

TUTUMIE HATA KITABU CHA SAMATTA KWA KINA AJIB

Mbwana Samatta

Dibaji yake inavutia na haitofautiani sana na Dibaji za wachezaji wengi wa Tanzania.

Hakuzaliwa katika mazingira yenye utajiri mkubwa, hata hakufanikiwa kuwa kwenye vituo vya kulelea na kukuza vipaji.

Kwa kifupi ametokea kwenye mazingira halisi ya kitanzania.

Mazingira ambayo vijana wengi hupitia. Mazingira ambayo yalimpa nafasi ya kucheza chandimu.

Ndiyo mazingira yetu haya, fahari yetu wakati tukiwa watoto ilikuwa kucheza mpira wa makaratasi.

Mpira ambao tuliucheza kutokana na uelewa wetu sisi. Hatukuwa na kocha wala kiongozi yoyote mkubwa mwenye uelewa mkubwa wa mpira.

Tulijiongoza wenyewe, tukajifundisha wenyewe hata mbinu za kucheza mpira zilitokana na akili zetu ambazo tulizipa nafasi ya kutufundisha.

Ni mazingira ambayo yalitujenga kujituma na kutokata tamaa kwa wale ambao walikuwa na nia ya kucheza mpira.

Ni ngumu sana kuendelea kuwa na ndoto ya kucheza mpira wakati unacheza peku bila viatu hata viwanja vyetu vilikuwa vimejaa michanga mingi.

Lakini kwa sababu mpira ulikuwa moyoni kwa baadhi ya watu ndiyo maana hawakukata tamaa.

Ajib
Ajib

Leo hii tunamuona Mbwana Ally Samatta, chimbuko la vijana ambao walianza kucheza wakiwa peku na kwenye viwanja vyenye michanga mingi.

Mazingira haya kwake hayakuwa kama kizingiti kumzuia kusonga mbele ili kukamilisha ndoto zake.

Aliyatumia mazingira haya kama kiunzi, aliruka kila kiunzi ili kufikia safari ambayo alikuwa anaiota kuifikia.

Hakukatishwa tamaa na kitu chochote, moyoni mwake aliamini ipo siku jua litachomoza upande wake.

Kila alipokuwa anarudi nyumbani, usiku wake aliota njozi akiwa anacheza kwenye uwanja mkubwa usio kuwa na michanga tena miguu yake ikiwa imefunikwa na viatu vizuri.

Hakuishia kuota njozi peke yake, kila muda alikuwa anakimbia kuelekea njozi zake zilipo.

Hakusubiri kabisa kuona njozi zikimkimbilia yeye, ila alizikimbilia kwa nguvu na kutokata tamaa.

Aliamini mpira ndiyo utakuwa maisha yake na kwa kifupi ndiyo utakuwa mkombozi wake cha muhimu alichokuwa anatakiwa kuwa nacho ni kujituma kwa juhudi kubwa ili kuzifikia njozi zake zilipokuwepo.

Vijana wengi hutamani maisha yao yaishie Simba au Yanga. Kwao wao hapa ndipo mwisho wa ndoto zao kwenye mpira.

Tunatofautiana kuwaza na inawezekana kuna watu wanawaza sahihi au siyo sahihi, hakuna aliye mkamilifu kwenye uso huu wa dunia, ndiyo maana hata Mungu alipoumba vitu vyote alisema hiki ni chema kasoro mwanadamu.

Hatukuumbwa kama wema hivo ni ngumu kwetu sisi kuishi maisha yenye usahihi lakini ni rahisi kwetu sisi kuishi kwenye maisha bora kwa sababu tulipewa nguvu za kutengeneza ubora wetu.

Ni ngumu sana kwa mcheza mpira kupata ubora wa maisha yake akiwa Kariakoo(Simba na Yanga).

Kwenye hivi vilabu mara nyingi kwa wachezaji wenye maono makubwa hutimia kama daraja la kwenda sehemu ambayo ni bora.

Ndiyo maana tulimuona Shaban Nonda akiitumia Yanga kama njia ya kwenda Ufaransa.

Aliamini kuwa Yanga haikuwa sehemu nzuri na bora ya kuweka makazi ila ilikuwa ni sehemu ambayo itatumika kama njia ya kwenda sehemu ambayo ni bora kuzidi Yanga.

Alikuwa na maono, hakuwa anacheza mpira kwa kujifurahisha pekee aliona kuwa kuna siku nguvu za kucheza mpira zitaisha na atatakiwa kutumia pesa ambazo alizipata kwenye mpira ili kujikimu.

Pesa hizo zinapatikana Simba na Yanga? , hapana shaka jibu la swali hilo ni hapana. Na ndilo jibu ambalo Mbwana Samatta alilitoa baada ya kujiuliza mara mbili mbili kichwani mwake.

Aliona Simba haina pesa za kumfanya awe na maisha mazuri kipindi atakapostaafu.

Aliwatazama wachezaji wa zamani maisha ambayo wanaishi. Maisha ambayo hayakuwapa hata nafasi za wao kupata hata pesa za kujitibu kipindi walipokuwa wanaumwa.

Maisha ambayo yaliwasababisha wao wasipate nafasi hata ya kuishi kwenye nyumba bora.

Haya maisha ndiyo yalikuwa yanamuumiza sana Mbwana Samatta, aliiogopa kesho. Hakutaka kuishi kwa kutamani tu maisha mazuri ila aliishi kwa kuyatafuta maisha mazuri.

Mazoezi na nidhamu ikawa silaha yake. Alielewa ni kipi alichokuwa anakifanya, ndiyo maana wakati Patrick Phiri alipokuwa amepanga mazoezi ya timu yaanze saa moja asubuhi, alimkuta Mbwana Samatta ameshalowa jasho kwa kufika mapema mazoezini kwa ajili ya mazoezi binafsi.

Aliheshimu na kukifanyia kazi kila alichokuwa anashauriwa kuhusiana na kipaji chake, kwa kifupi aliamua kuchagua aina ya marafiki wa karibu wa kuishi naye.

Jicho lake liliitizama zaidi kesho yake kuliko sehemu ambayo alikuwa amesimamia. Swali kubwa lililokuwa linazunguka kichwani mwake ni sehemu ipi atakuwepo kipindi jua la kesho litakapochomoza?

Swali hili lilimpa hofu ya kuiogopa kesho yake, alicheza kwa kujituma kila alipoingia uwanjani. Hakusikiliza kelele zilizokuwa zinamsifia jukwaani, alizitumia kama kelele ambazo zilikuwa zinamfukuza eneo ambalo alilokuwepo.

Ndiyo maana kwenye mechi kati ya Simba na TP Mazembe alijituma kuonesha uwezo wake kwa wakati ule.

Uwezo ambao uliwafanya TP Mazembe wamchukue. Ikawa ndiyo ukarasa wake mpya. Ukurasa ambao ulimfungulia njia ya kucheza KR Genk.

Leo hii anaonekana kama Mfalme katika nchi ya Ubelgiji. Anajituma bila kuchoka na anaonekana hajafika sehemu ambayo anatamani kuwepo.

Maono yake yapo kwenye ligi kubwa ndiyo maana kila akiingia uwanjani anaonesha kitu kikubwa tofauti na alichokionesha Jana.

Uso wake una njaa, miguu yake inatamani kucheza ligi kubwa na anaona ni dhambi kubwa ambayo ataifanya kama atastaafu mpira bila yeye kucheza moja ya ligi kubwa ulaya ndiyo maana msimu huu kaifungia KR Genk magoli 7 kati ya michezo 7.

Hii ndiyo njaa ambayo wachezaji wetu wanatakiwa kuwa nayo. Hawatakiwi kubweteka. Waumizwe sana na mafanikio ya watu wengine.

Kila muda huwa tunatumia mifano ya kina Cristiano Ronaldo kuwahamasisha lakini mfano Mbwana Samatta ni mfano bora kuzidi mifano yote kwa sababu amepitia maisha ambayo wengi tumepitia na leo hii hayupo sehemu ambayo alikuwepo jana.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

YANGA NA MTIBWA, KONDOO ALIYETOKA USINGIZINI NA KONDOO ALIYE MALISHONI

Tanzania Sports

KUNA WAKATI MANARA ANAJING’ATA ULIMI WAKE