Kuna wakati kila nikifumba macho yangu, masikio yangu huwa yanasikia sauti za majonzi lakini sina uhakika kama nyuso za hao watu huwa zina majonzi kama sauti zao zinavyokuwa na majonzi.
Wengi wanatamani siku moja wasikie vigelele na siyo majonzi tena kwenye nyumba inayoitwa Azam FC. Wenye nyumba mpaka muda huu washavuka salama Misri ila safari yao ya kwenda Israel (Kanani) ina mashaka.
Kila sauti inatamani Azam FC ifike Israel (Kanani). Kila sauti inatoa lawama kwanini mpaka leo hii Azam FC imeshindwa kufika Israel (Kanani). Wana kila kitu cha kuwafikisha huko.
Ukiisikiliza sauti hii itakuambia tatizo ni makocha wanaoletwa hawana viwango vikubwa. Kabla hujamaliza kuisikia hiyo sauti kuna sauti nyingine itakuambia tatizo wachezaji hawajitumi.
Kuna sauti nyingine itakuambia Azam FC haina mashabiki wengi, mashabiki ambao wanaweza kutia presha kubwa kwa wachezaji ili wajitume na wapate matokeo kwa ajili ya timu.
Wakati unakuna kichwa kuna sauti nyingine itakuambia Azam FC haina mtendaji mkuu bora wa klabu yani C.E.O. Mtendaji mkuu ambaye anaweza kuyabeba maono ya klabu na kuyafikisha sehemu kubwa.
Wakati unafikiria kuhusu hilo la mtendaji mkuu kuna sauti nyingine inasikika ikizungumzia wamiliki wa klabu kama wao ndiyo tatizo. Wamiliki wanawasikiliza na kuwadekeza wachezaji na kuna wakati hawaelewani wao kwa wao.
Sauti zote hizi lengo lake ni moja tu. Azam FC kufika Israel (Kanani). Azam FC wanaonekana wana ncha kali lakini ncha ya marefu yao imekuwa fupi sana. Tangu wapande ligi kuu mwaka 2004 wameshinda ligi mara moja tu ndani ya miaka 20.
Mafanikio yao makubwa kwenye mashindano ya CAF ni wao kufika hatua ya pili ya michuano hiyo ndani ya miaka 20. Hiki kitu kinawaumiza wengi sana kwa sababu Azam FC wanaonekana wana ncha kali na marefu yao yanatakiwa kuwa marefu.
Tatizo la sauti hizi zinazohoji kwanini Azam FC hawajafika Israel (Kanani) mpaka muda huu hazipati majibu sahihi kutoka kwa wahusika na ndiyo maana sauti hizi zinabaki zikijipa majibu wenyewe.
Hakuna sauti kutoka Azam FC ambayo ishawahi kutoka nje na kujibu hizo sauti. Nafikiri kwa sasa ni muda sahihi kwa Azam FC kuzijibu hizi sauti kwa vitendo.
Azam FC wao ndiyo wanaojua tatizo ni nini. Hawatakiwi kutuambia. Wajaribu kulitatua tatizo lao wenyewe kisha watujibu kwa vitendo. Watanzania wengi wanatamani Azam FC ifanikiwe lakini Azam FC inaonekana inalazimishwa kufanikiwa na Watanzania.
Uongozi unatakiwa urudi kwenye chumba cha maamuzi na kuchora upya tena ramani ili tuone timu nyingi zikifanya vyema kwenye mashindano ya CAF. Siku tukifanikiwa kuingiza timu tatu kwenye makundi ndiyo siku ambayo tutakuwa tumekaribia kubeba kombe la CAF.