in , ,

Tumeacha kujadili UBOVU wa vilabu vyetu, tumehamia kwa WAMBURA

Tanzania ni moja ya nchi ya matukio sana, na huwa inaendeshwa na matukio sana. Tena matukio ya ajabu ajabu.

Matukio ambayo mara nyingi hututoa kwenye reli ya kujadili vitu vya maana na wengi hujikuta tunaanza kujadili vitu vya ajabu.

Ndivyo tulivyo, na ndivyo tulivyoumbwa!. Na tumeshindwa kabisa kubadilika sisi kama sisi. Tumeamua kujichagulia dunia yetu.

Dunia ya ajabu sana. Dunia ya kupenda vitu vya ajabu sana na kuvipuuzia vitu vya muhimu vyenye kuleta tija.

Leo hii michuano ya Sportpesa inaendelea hapa hapa nyumbani kwetu. Kwenye ardhi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Lakini vilabu vyetu vimeonekana dhaifu sana katika uwanja wetu wa nyumbani. Unaweza ukaanza kutetea kwa kunikumbusha ushindi wa Mbao na Simba jana.

Na mimi nitakuuliza wameshinda katika mazingira gani ?, mazingira ambayo yanatufanya tuonekane ni wenyeji wa michuano hii?.

Ni kweli tunatumia vizuri neno “uwanja wa nyumbani?”, wakati natazama mechi ya Simba na AFC Leopards nilikuwa najiuliza mwenyeji ni Leopards?

Alikuwa anacheza kama yupo nyumbani. Alikuwa amejitawala vizuri na alimpa mtihani mkubwa Simba ambaye alikuwa nyumbani.

Hakukuwepo na ile faida ya kuwa Simba alikuwa nyumbani. Vivo hivo kwa Mbao. Waliwaliwa sana na Gormahia ya Kenya.

Wakenya walionekana wao ndiyo wenyeji wa mechi hii. Walionekana ule uwanja wa Taifa , Benjamin Mkapa aliwajengea wao.

Hakutujengea sisi kabisa, ndiyo hata mechi za awali tulishuhudia Yanga na Singida United wakitolewa kwenye michuano hii.

Siyo kutolewa tu, walitawaliwa kwenye michezo yao. Yani sisi tunaonekana watumwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani.

Tunaonekana watumwa mbele ya mashabiki wetu. Utumwa huu haujaanza kwenye michuano ya Sportpesa.

Msimu huu Mtibwa Sugar amefungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani na SC Villa kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Yanga msimu jana naye alipata matokeo mabovu sana katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.

Leo hii kila Mtanzania hawezi kusahau kipigo ambacho Simba alipewa na As Vita wiki iliyopita kwa kufungwa magoli 5-0.

Kipigo kikubwa sana na cha aibu tena kwenye ngazi ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Michuano ambayo tunaamini timu zinazofika huko huwa ni timu bora.

Lakini ni Tanzania pekee ambayo inachukuliwa kama nchi ambayo imepeleka timu dhaifu kwa sababu ya kipigo kizito kama hicho.

Huu ndiyo mjadala ambayo unatakiwa kujadiliwa kwa upana katika Taifa letu. Mjadala ambao una manufaa mapana ya mpira wetu.

Kwanini sisi ?, wapi tunakwama?, tufanye nini?. Tuachane kabisa na mijadala ya siasa ya mpira. Tujikite hapa kwenye ufundi.

Tusijaribu hata kidogo kuukwepa au kuukimbia ukweli ambao uko wazi kabisa na kujifichia kwenye migogoro ya kina Michael Wambura.

Tuko kwenye dunia ambayo tunatakiwa kupuuzia sana kujihusisha na kuipa nguvu na wakati mwingi migogoro ambayo.

Tunatakiwa kuhubiri mafanikio, na kuwaacha wale ambao wanagombana. Watakaa wenyewe watamalizana.

Sisi tujikite kujadili kwanini tunafanya vibaya dhidi ya timu za kimataifa. Hiki ndicho kitu cha muhimu kinachotakiwa kujadiliwa kwa upana kila siku kuliko kuwajadili migogoro.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Kumbe JOSE MOURINHO alishindwa kuishi na wachezaji wa ‘INSTAGRAM’

Tanzania Sports

Watanzania tunapenda mpira, lakini mpira hautupendi